BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KITENDAWILI KIMETEGUKA !! KASSIM MAJALIWA NDIYE WAZIRI MKUU AKIRITHI MIKOBA YA MIZENGO KAYANDA PINDA !.


Miongoni mwa watu wanaotajwa katika kinyang'anyiro cha kuteuliwa kuwa waziri mkuu ni mbunge wa Ruangwa, Kassim Majaliwa.

RAIS John Magufuli leo anatarajiwa kukata mzizi wa fitina wakati jina la mteule wake kwa nafasi ya Waziri Mkuu litakaposomwa bungeni na Spika wa Bunge, Job Ndugai na kisha kuthibitishwa kwa kura na wabunge.

Gumzo la nani atakuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dk Magufuli, limekuwa kubwa kabla na hata baada ya kuanza kwa vikao vya Mkutano wa Kwanza wa Bunge la 11 Jumatatu wiki hii ambalo juzi lilimchagua Ndugai kuwa Spika wake.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 51 (1), inasema: “Kutakuwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano atakayeteuliwa na Rais kwa kufuata masharti ya ibara hii na ambaye kabla ya kushika madaraka yake ataapa mbele ya Rais kwa kiapo kinachohusika na kiti cha Waziri Mkuu kitakachowekwa na Bunge.”

Aidha, Kifungu cha (2) cha Ibara hiyo kimeweka masharti kwamba mapema iwezekanavyo na kwa vyovyote vile ndani ya siku 14 baada ya kushika madaraka yake, Rais atamteua mbunge wa kuchaguliwa kutoka katika Jimbo la Uchaguzi anayetokana na chama cha siasa chenye wabunge wengi zaidi bungeni au kama hakuna chama cha siasa chenye wabunge wengi zaidi, anayeelekea kuungwa mkono na wabunge walio wengi kuwa Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu huyo, kwa mujibu wa kifungu hicho, hatashika madaraka yake mpaka uteuzi wake uwe umethibitishwa na Bunge kwa azimio litakaloungwa mkono na kura za wabunge walio wengi. Kwa kuzingatia Ibara hiyo, Spika Ndugai leo asubuhi anatarajiwa kwenda katika Ikulu ya Chamwino, Dodoma kupewa jina hilo ndani ya bahasha na Dk Magufuli, na jina hilo litathibitishwa kwa kupigiwa kura na wabunge, ambapo kwa mujibu wa ratiba tukio hilo litafanyika alasiri.

Ndugai atafanya hivyo kama walivyofanya waliomtangulia; Pius Msekwa ambaye mara mbili katika Ikulu hiyo alipewa bahasha na Rais Benjamin Mkapa ikiwa na jina la Frederick Sumaye; Samuel Sitta ambaye Desemba 2005 alipewa jina la Edward Lowassa na Rais Jakaya Kikwete na kisha Februari 2008 akapewa jina la Mizengo Pinda.

Novemba 2010, Kikwete alimpa Anne Makinda tena jina la Pinda ambaye alishika nafasi hiyo baada ya kujiuzulu kwa Lowassa. Waziri Mkuu mteule huyo akishathibitishwa na Bunge ataapishwa kesho na kuwa Waziri Mkuu wa 11 wa Tanzania.

Atakuwa na madaraka ya udhibiti, usimamizi, utekelezaji wa siku hadi siku wa kazi na shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na kuwa Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni.

Wabunge wenyewe wamekuwa na mtazamo tofauti kuhusu nani anaweza kushika wadhifa huo mkubwa, wakitaja sifa za mtu anayestahili, lakini wengine wakienda mbali zaidi wakitaja majina ya wahusika.

Vigogo wanaotajwa zaidi Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini yapo majina ya watu maarufu waliokuwa mawaziri katika Serikali ya Awamu ya Nne wanaopewa nafasi kwamba Rais anaweza akachomoa jina kutoka miongoni mwao.

Mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe anatajwa zaidi kama miongoni mwa majina yanayoweza kufikiriwa kwa nafasi hiyo kutokana na wakati fulani kufanya kazi na Magufuli katika Wizara ya Ujenzi akiwa Naibu Waziri. Wanamueleza Mwakyembe kama msomi na mtendaji ambaye wanaelewana vyema na Magufuli, hivyo itakuwa rahisi kumsaidia katika utekelezaji wake. Amepata kuwa Waziri wa Uchukuzi na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ambaye ni Mbunge wa Musoma Vijijini, naye anatajwa kwamba anafaa kushika nafasi hiyo, huku akitajwa kwamba ni mtu ambaye falsafa ya Rais Magufuli ya Hapa Kazi Tu anaweza kuitekeleza kwa ufanisi na hana utani.

Pia Mbunge wa Isimani, William Lukuvi ambaye ameshika nafasi nyeti katika Awamu ya Nne ikiwamo ya Mnadhimu wa Serikali bungeni na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ni kigogo mwingine anayetajwa zaidi akielezwa ana uzoefu mkubwa na anayeweza kutekeleza vyema usimamizi wa serikali bungeni.

Pia kundi hilo la vigogo yapo majina ya Dk Diodorus Kamala ambaye amepata kuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki na baadaye balozi na Lazaro Nyalandu aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii nao wakichomoza.

Kundi la Vijana Kundi lingine ambalo linapewa nafasi kubwa kwamba huenda akawa miongoni mwao ni la vijana ambao wameonesha uwezo mkubwa katika Bunge lililopita. Mbunge wa Bumbuli, January Makamba aliyekuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia pamoja na Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha, wanaongoza kundi hili.

Mwigulu na Makamba pia wanaelezwa walifanya kazi kubwa katika kampeni kwa kujenga mikakati ya ushindi na pia wanaelezwa wanakubalika zaidi kwa Dk Magufuli. Hata hivyo, changamoto ya umri bado ni kikwazo kwani wote hawazidi miaka 45, ingawa nafasi ya Uwaziri Mkuu hilo halizingatiwi.

Kundi mbadala Wabunge wameegemea katika majina maarufu, lakini yapo majina mengine si maarufu, lakini yanazungumzwa kwamba pengine anaweza Waziri Mkuu kupatikana miongoni mwao.

Mbunge wa Makete, Dk Norman Sigalla anapewa nafasi kwamba kama Rais akiamua kuteua Waziri Mkuu kutoka katika kundi mbadala, basi ana nafasi kubwa kutokana na elimu yake na pia uzoefu. Dk Sigalla amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya mbalimbali nchini, lakini ni kijana ambaye utendaji wake umeelezwa upo vizuri.

Kundi hilo mbadala pia anaingia Mbunge wa Muheza, Adadi Rajabu ambaye amepata kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na pia Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe. Uzoefu wake huo serikalini na baadaye katika masuala ya kidiplomasia, ni miongoni mwa sifa zilizomfanya atajwe kwa nafasi hii.

Mawaziri Wakuu waliopita Mawaziri Wakuu 10 waliopita ni Mwalimu Julius Nyerere, Rashidi Kawawa, Edward Sokoine (wote marehemu), Cleopa Msuya, Salim Ahmed Salim, Joseph Warioba, John Malecela, Sumaye, Lowassa na Pinda.

Wanayosema wabunge Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), alisema anaamini atapatikana Waziri Mkuu ambaye wabunge watamheshimu na atashangaa akiteuliwa mtu ambaye hasa ni Waziri Mkuu na sio kivuli cha Waziri Mkuu. Mbunge wa Kavuu, Dk Prudenciana Kikwembe (CCM) alisema akipatikana Waziri Mkuu mfuatiliaji itakuwa nzuri zaidi.

Mbunge wa Mpwapwa, George Lubeleje (CCM) alisema anahitajika msomi na anayeijua vizuri Tanzania mwenye uwezo wa utendaji na atakayeendana na kasi ya Magufuli huku akitaja sifa ya ziada ni kujulikana kimataifa.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: