
Msemaji wa Jeshi la Polisi, SSP Advera Bulimba
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi nchini limeonya wananchi kujiepusha na vitendo vyovyote vitakavyoathiri amani iliyopo wakati huu dunia ikielekea kuuaga mwaka 2015 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2016.
Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyosambazwa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, SSP Advera Bulimba imesema, polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi hapa nchini vimejipanga kukabiliana na vitendo vyovyote vya uhalifu, hususani katika kipindi hiki cha kuelekea mkesha wa mwaka mpya, vinadhibitiwa katika mikoa yote.
Aidha taarifa hiyo imesema, ulinzi umeimarishwa kwenye maeneo yote ya kuabudia, fukwe za bahari, sehemu za starehe na maeneo mengine yote ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi limetoa tahadhari kwa wananchi wote kuwa makini na kuchukua hatua stahiki za haraka kwa kutoa taarifa pindi watakapoona viashiria vyovyote vya uhalifu katika maeneo yao ya makazi au maeneo ya biashara kupitia simu za polisi nambari 111 au 112.
Aidha, jeshi hilo limewatahadharisha watumiaji wa barabara kuzingatia sheria za usalama hususani madereva. Taarifa hiyo iliyotolewa na SSP Bulimba imewataka wananchi kuacha tabia ya kuchoma matairi barabani pamoja na kupiga mafataki.MWANANCHI DIGITAL
0 comments:
Post a Comment