
Rais Dk John Pombe Magufuli.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli amefanya uteuzi wa makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu 50 katika wizara mbalimbali, akimbakisha kwenye nafasi yake, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.
Katika uteuzi huo, baadhi ya makatibu wakuu pia wamebaki kwenye wizara na amewaacha baadhi yao ambao amesema watapangiwa kazi nyingine.
Walioachwa ni pamoja na Dk Donnan Mmbando(Afya), Balozi Liberata Mulamula(Mambo ya Nje), Omari Chambo (Nishati na Madini), Jumanne Sagini (Tamisemi) na Joyce Mapunjo (Afrika Mashariki).
Katika uteuzi huo alioutangaza jana, makatibu wakuu wakiwa 29 na naibu makatibu wakuu 21, Rais Magufuli alimteua Peter Ilomo kuendelea kuwa Katibu Mkuu Ikulu, Dk Laurian Ndumbaro ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora.
Katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Katibu Mkuu ni Mhandisi Mussa Iyombe akisaidiwa na naibu makatibu wakuu wawili, Dk Deo Mtasiwa (Afya) na Bernard Makali (Elimu).
Mbaraka Wakili ameteuliwa katibu mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais akisaidiwa na Mhandisi Ngosi Mwihava wakati katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge, Sera, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu), Rais ameteua makatibu wakuu watatu ambao ni Erick Shitindi (Kazi na Ajira), Mussa Uledi (Bunge) na Dk Hamis Mwinyimvua (Sera).
Katika Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi pia ameteua makatibu wakuu watatu, Dk Florence Turuka (Kilimo), Dk Maria Mashingo (Mifugo), Dk Yohana Budeba (Uvuvi)
Wizara nyingine ambayo Rais Magufuli ameteua makatibu wakuu watatu ni Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ambazo zitaongozwa na Mhandisi Joseph Nyamuhanga (Ujenzi), Dk Leonard Chamuliho (Uchukuzi), Profesa Faustine Kamuzora (Mawasiliano) wakati Mary Sassabo anakuwa Naibu Katibu Mkuu (Mawasiliano).
Katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Katibu Mkuu anakuwa Dk Yamungu Kayandabira na naibu wake ni Dk Moses Kusiluka.
Meja Jenerali Gaudence Milanzi anakwenda kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii akisaidiwa na Anjelina Madete. Katika Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ameteua makatibu wakuu wawili, Dk Adelhem Meru (Viwanda) na Profesa Adolf Mkenda (Biashara na Uwekezaji) na watasaidiwa na Mhandisi Joel Malongo.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi atakuwa Maimuna Tarishi akisaidiwa na naibu makatibu mkuu wawili, Profesa Simon Msanjila, Dk Leonard Akwilapo wakati katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ameteua wawili, Dk Mpoki Ulisubisya (Afya) na Sihaba Nkinga (Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto).
Profesa Elisante Ole Gabriel Mollel anaendelea kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo akisaidiwa na Nuru Halfan Mrisho huku katika Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Mbogo Futakamba akiteuliwa Katibu Mkuu na Mhandisi Kalobero Emmanuel naibu wake.
Katika Wizara ya Nishati na Madini, Rais Magufuli amemteua Profesa Justus Ntalikwa kuwa Katibu Mkuu akisaidiwa na naibu wawili, Profesa James Mdoe na Dk Paulina Pallangyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria anakuwa Profesa Sifuni Mchome akisaidiwa na naibu wawili, Suzan Mlawi na Amon Mpanju wakati Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani anakuwa Jaji Meja Jenerali Projest Rwegasira akisaidiwa na Balozi Hassan Yahaya.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango ataendelea kuwa Dk Silvacius Likwelile akisaidiwa na manaibu watatu, Dorothy Mwanyika, James Dotto na Amina Hamis Shaban.
Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa aliyeteuliwa ni Dk Aziz Mlima (Katibu Mkuu) na Balozi Ramadhan Mwinyi (Naibu Katibu Mkuu), wakati Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, ameteuliwa Job Masima kuwa Katibu Mkuu akisaidiwa na Immaculate Peter Ngwale.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amemteua Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Eliakimu Maswi kuwa Kaimu Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), huku akitengua uteuzi wa Naibu Kamishna wa Mamlaka hiyo, Lusekelo Mwaseba ambaye atapangiwa kazi nyingine. Maswi aliwahi pia kuwa katibu mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini. MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment