BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KUONGEA SANA KUMBE KUNAWASAIDIA WANAWAKE KUJIEPUSHA NA VIFO VYA KUJIUA

Wataalamu wanasema mwanamke kawaida huongea maneno 45,000 hadi 50,000 kwa siku na mwanaume maneno 15,000.

Kumbe uzungumzaji huu wa maneno mengi umekuwa dawa kwao kwa sababu takwimu zinaonyesha kuwa wanaoongoza kujiua ni wanaume, huku sababu kuu ya kujinusuru na hilo kwa wanawake ikiwa ni kuzungumza, kulalamika na kujadili masuala yao wakiwa peke yao.

Taarifa iliyotolewa na Shirika la Afya duniani (WHO), inaonyesha kuwa mtu mmoja hufa kwa kujiua kila baada ya sekunde 40.

Katika ufafanuzi wa taarifa hiyo imebainisha kuwa wanaume wengi hujiua zaidi ya wanawake hawa wenye umri kati ya miaka 45 hadi 50, huku katika nchi zinazoendelea wanaume wa umri huo wanaojiua ni mara tatu zaidi ya wanawake.

Mtaalamu wa saikolojia wa jijini Dar es Salaam, Abdulkadir Ayoub anaitaja sababu kuu ya wanawake kunusurika kujiua ni kutoa hisia zao tofauti na wanaume.

Anatolea mfano iwapo mwanamke ameumizwa ni rahisi kulalamika kwa jamii, iwe kwa kufoka au taratibu, kushitaki kwa wakubwa wa familia, huku hali ikiwa tofauti kwa wanaume ambao hugugumia na matatizo yao.

“Siyo rahisi mwanaume amfumanie mwanamke halafu alalamike, atakachofanya kuchukua uamuzi mgumu wa kulipiza kisasi kati ya wawili hao, akiwa hana uwezo wa kuchukua hatua yoyote atafikiria kujiua.

“Sababu ni kuwa wanaume kimila na desturi ndiyo wenye uamuzi, wanaonekana kukubaliwa na familia zaidi kuliko wanawake, hivyo ikitokea akalalamika ataonekana hafai, jambo wasilolitaka liwatokee, ” anasema Ayoub.

Mtaalamu wa saikolojia aliyejitambulisha kwa jina moja la Frank anasema kuwa kujiua hutokana na msongo wa mawazo.

Anasema kujiua kisaikolojia kuna hatua nne au tano. Mwisho ni ile inayomfanya mhusika kuhisi ametengwa na jamii na kuamua kutafuta suluhisho.

“Anakuwa hana nia ya kutenda tendo la kujiua, lengo lake ni kutafuta suluhisho, hilo suluhisho ndiyo huishia kujiua, ” anasema Frank.

Frank anasema kinachowanusuru wanawake kuchukua hatua hiyo ni kuwa wepesi wa kuzungumza matatizo yao, iwe kwa rafiki mmoja, wawili au hata jamii inayowazunguka.

Anasema sababu nyingine ni kuwa karibu na familia ikiwamo watoto, ndugu, mume, hivyo anapotaka kufanya jambo lolote baya litakalohatarisha maisha yake hufikiria familia kwanza.

Dk Yeam Bunting mtaalamu wa saikolojia kutoka nchini Sierra leone aliyeshiriki kwenye tafiti mbalimbali za masuala ya saikolojia, aliwahi kuliambia Jarida la Expo Times kuwa mapenzi ya wanawake kwa familia hasa watoto huwaepusha na uamuzi mbaya ikiwamo kujiua.

Dk Bunting aliliambia jarida hilo kuwa mbali na mapenzi kwa familia wanawake pia ni wazungumzaji kupita kiasi hasa wanapokasirika, hivyo nguvu wanayotumia kuzungumza hupunguza machungu.

“Kwa kawaida mwanamke hata akiwa mpole, lazima linapokuja suala gumu kulimaliza huzungumza na mtu anayemuamini, hilo huwasaidia kupunguza maumivu yao.

“Mwanamume ni ngumu kusema linalomtatiza, hutafuta ufumbuzi mwenyewe na ndipo husababisha kujiua”.

WHO inataka kupunguza kiasi cha vifo kwa asilimia 10 ifikapo 2020, wakisisitiza kunahitajika elimu zaidi mashuleni.

Ripoti hiyo ya miaka 10 ya uchunguzi wa vifo duniani kote pia ilibaini karibu watu 800,000 hujiua kila mwaka na ikitajwa kuwa sababu kubwa ya vifo kwa vijana wenye miaka kati ya 15 hadi 29.

Robo tatu ya vifo hivyo vilikuwa katika mataifa yenye kipato cha chini na cha kati. Ripoti hiyo imesema kupungua kwa uwezekano wa kupata silaha na kemikali zenye sumu zimeonyesha kupunguza idadi ya wanaojiua.

Pia, kuanzisha mkakati wa kitaifa wa kupunguza watu wanaojiua ulikuwa unafanya kazi vizuri, lakini umeundwa katika nchi chache.

Mkurugenzi Mkuu wa (WHO), Dk Margaret Chan anasema unyanyapaa wa jamii dhidi ya magonjwa ya akili unaonekana kuzuia watu kutafuta msaada na humsababishia mtu kujiua.

Anasema asilimia 75 ya vifo hivyo hutokea katika nchi zenye kipato cha chini na kati.

WHO imeeleza kuwa kumekuwa na ongezeko la asilimia 38 katika viwango vya kujiua nchi za Afrika.

Vitu vinavyotajwa kutumiwa kujiua ni dawa hatari, sumu za kuulia wadudu na silaha za moto.

Dk Alexandra Fleischmann, mtaalamu wa Idara ya Afya ya Akili na madawa ya kulevya wa WHO anashauri hatua madhubuti zichukuliwe kulipinga jambo hilo kuanzia ngazi za familia, mitaa.


“Hapo zamani ilikuwa kujiua ni mwiko hasa katika jamii za Afrika, lakini miaka 10 iliyopita jambo hilo limekuwa na kawaida na limeongezeka kwa kiasi kikubwa. 

Shirika hilo limebainisha sababu mbalimbali zinazochangia kujiua ikiwamo maradhi kama matatizo ya mishipa ya fahamu, saratani na maambukizi ya VVU.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: