BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

UNYWAJI WA POMBE KWA MWANAUME NAMNA UNAVYODUMAZA FAMILIA

Udumavu ni tatizo ambalo linaweza kumkabili mtoto akiwa tumboni au baada ya kuzaliwa na hasa siku 1000 zinazohesabiwa tangu mama kupata ujauzito. Ingawa tatizo linatajwa kuwa linapungua kutokana na elimu inayoendelea kutolewa, bado wapo watoto wanaoendelea kukabiliwa nalo.

Mkoa wa Dodoma, ni miongoni mwa maeneo nchini yanayotajwa kuandamwa na tatizo ingawa takwimu mpya zinaonesha tatizo linapungua kutokana na elimu inayoendelea kutolewa. Ofisa Lishe wa Mkoa wa Dodoma, Mary Boniventure ananukuu takwimu mpya za mwaka 2015/2016 zinazoonesha tatizo la udumavu limepungua kutoka asilimia 56 za mwaka 2010 hadi asilimia 36.5.

Hata hivyo, katika kuelezea hiyo asilimia 36.5, Boniventure anaainisha mazingira yanayochangia udumavu katika mkoa huo. Anataja ulaji duni ndani ya siku 1,000 za mwanzo tangu kutungwa kwa mimba hadi umri wa miaka miwili, kuwa ni miongoni mwa sababu zinazochangia tatizo.

Boniventure anaweka wazi kwamba, baadhi ya familia zimekuwa zikijikuta zikipata lishe duni huku akinamama na watoto wakiwa waathirika wakubwa wa hali hiyo tofauti na wanaume.

Imebainika baadhi ya wanaume hujipendelea kwa kula vyakula vyenye virutubisho vingi kama vile nyama wakiwa kwenye minada na vilabu vya pombe wakati watoto na akinamama walio nyumbani hukosa fursa hiyo. Ofisa huyu wa lishe anaelezea tatizo hili akisema, udumavu ni zaidi ya urefu mdogo.

”Ukuaji duni wa kimwili na kiakili,kupungua kwa uwezo wa kufikiri na kufanya kazi,” anasema.

Hali hiyo husababisha mtoto kuwa na maendeleo duni shuleni, utoro na kuacha shule. Kwa upande wa watu wazima wanaokabiliwa na udumavu, uzalishaji wao huwa duni ofisini na hata kwenye shughuli nyingine za kiuchumi kama vile kilimo, ufugaji na ujasiriamali. Pia tatizo hilo hufanya mtu awe na uwezekano mkubwa wa kupata magonjwa. Watoto kuugua mara kwa mara (kinga mwili).

Boniventure anasema kwa wanawake waliodumaa wana uwezekano mkubwa wa kupata matatizo wakati wa kujifungua ikiwemo kupata watoto wenye uzito pungufu.

Kiuchumi kipato cha mtu mdumavu kinapungua kwa asilimia 20. Athari za udumavu kwa mtu binafsi, mtoto, kijana, mtu mzima, kwa jamii na taifa kwa ujumla ni kubwa.

“Inaweza kuonekana ni kitu cha kawaida katika jamii hasa katika jamii za watu wafupi. Udumavu ni matokeo ya utapiamlo sugu, dalili hazishitui au kutisha jamii,” anasema.

Aidha udumavu huweza kutokea mtoto akiwa tumboni au baada ya kuzaliwa. Hali hii inaweza kuzuilika kwa kuhakikisha mtoto anapata virutubishi ndani ya siku 1,000 tangu ujauzito kutungwa.

Siku 1,000 tangu kutungwa ujauzito hadi mtoto anapotimiza miaka miwili ni kipindi muhimu sana kwa sababu ni katika kipindi hicho cha ujauzito, mtoto anakua kwa haraka zaidi na ana mahitaji makubwa ya virutubishi.

Uharibifu utakaosababishwa na utapiamlo katika kipindi hicho cha miaka miwili haurekebishiki katika kipindi chote cha uhai wake hivyo kumfanya mtu mzima mdumavu. Zipo athari za utapiamlo kwa maendeleo ya ubongo na uwezo wa kujifunza kwani vitamini na madini yanahitajika kwa maendeleo mazuri ya ubongo.

“Ubongo wa mtoto hukua kwa haraka sana wakati wa ujauzito na katika miaka miwili ya kwanza ya uhai wake,” anasema.

Pia utapiamlo wakati wa ujauzito hadi mtoto anapotimiza miaka miwili unasababisha uharibifu wa kudumu, usioweza kurekebishwa katika maendeleo ya mtoto. Aidha hupunguza ufanisi wa mtoto wa kujifunza shuleni na kwingineko.

“Watoto wenye tatizo hili huwa na ugumu sana katika kuelewa na huwa hawapendi shule na hivyo kuongeza tatizo la utoro, mtoto wa namna hii hata uelewa wake ni mdogo unaweza ukamtuma maji akaleta fagio,” anasema.

Upungufu wa madini joto hupunguza kiwango cha uwezo wa akili ya mtoto kwa alama 10 hadi 15. Anasema utapiamlo baina ya wanawake walio katika umri wa kuzaa wa miaka 15 hadi 49, kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2010, hali ya kitaifa ni upungufu kwa asilimia 37 na Dodoma ina upungufu wa asilimia 33. Pia hali ya kitaifa ya upungufu wa madini joto ni asilimia 30 na Dodoma ina upungufu wa asilimia 28.

Vile vile upo uhusiano wa uzalishaji wa chakula na udumavu kwani hata mikoa inayozalisha chakula kwa wingi pia ina kiwango kikubwa cha udumavu.

Vilevile, miongoni mwa mambo yanayotakiwa kufanyika ili kuzuia udumavu ni pamoja na kuboresha chakula cha nyongeza kwa watoto wa umri wa miezi 6 hadi miaka miwili.

Matunzo na ulishaji wa mtoto wakati wa ugonjwa, kwa maana ya kumpa mtoto vinywaji kwa wingi kama vile maziwa, togwa, juisi halisi na maji husaidia kukabili tatizo.

Njia nyingine ni kumpa mtoto vyakula laini (vilipondwa) na vilivyoboreshwa (kuongezwa maziwa, karanga, nyama, samaki, soya, mafuta. Pia kuzuia magonjwa kwa watoto, kutumia huduma za afya, chanjo zote, utumiaji wa vyandarua, matone ya vitamini A , dawa za minyoo husaidia kukabili tatizo.

Uhamasishaji unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee katika miezi sita ya mwanzo ni njia nyingine ya kukabili udumavu kwa watoto. Lishe ya mjamzito na anayenyonyesha inapaswa iboreshwe.

“Mtoto anyonyeshwe mara nyingi kadri anavyohitaji,” anasema. Ofisa Lishe huyo wa Mkoa wa Dodoma, Boniventure anasema mkoa wa Dodoma umedhamiria kuimarisha ulishaji wa watoto wachanga na wadogo.

Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Lishe kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii , Dk Vincent Assey anasema madhara ya lishe duni yamekuwa yakichangia kuongezeka kwa magonjwa mbalimbali na hata kudidimiza nguvu kazi ya taifa kwani watu wenye tatizo hilo wanakuwa na ufanisi duni ikiwemo kuchoka haraka.

Dk Assey anasema moja ya tatu ya watoto wenye umri wa miezi sita hadi 56 wana upungufu wa virutubisho.

Anasema takwimu za kidunia zinaonesha watoto milioni tatu hupoteza maisha duniani kutokana na madhara ya lishe duni huku Tanzania ikiwa na zaidi ya watoto milioni mbili walio hatarini. Anasema inawezekana kumaliza tatizo hilo ifikapo mwaka 2020 kutokana na kuwa na mikakati kamambe.

"Tuna matumaini ifikapo mwaka 2020, hali inaweza kubadilika. Tunataka kuhakikisha viwanda vinaendelea kuzalisha vyakula vyenye virutubishi," anasema.HABARILEO.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: