BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MAHAKAMA YATOA HATI YA KUKAMATWA KWA MBUNGE TUNDU LISSU

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imetoa hati ya kukamatwa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu.

Aidha, mahakama hiyo imeamuru wadhamini wake kufika mahakamani hapo kujieleza kwanini wasilipe fungu la dhamana, jumla ya Sh. milioni 20, baada ya mshtakiwa huyo kushindwa kufika kusikiliza kesi yake jana bila ruhusa.

Lissu anakabiliwa na mashtaka ya uchochezi kupitia gazeti la Mawio, kwa pamoja na wenzake watatu.

Awali, mahakama hiyo chini ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba iliwataka washtakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaotoka katika taasisi zinazotambulika, watakaosaini hati ya dhamana yenye thamani ya Sh. milioni 10 kila mmoja. Walitimiza masharti hayo.

Amri hiyo ilitolewa jana na Hakimu Simba baada ya upande wa Jamhuri kudai kuwa kesi hiyo ilipangwa jana kutajwa lakini mshtakiwa wa nne - Lissu - hakuwepo mahakamani.

Hata hivyo, alijitokeza mdhamini wake mmoja kati ya wawili, Robart Katula na kudai kuwa mshtakiwa huyo anaendesha kesi ya uchaguzi Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza.

Ndipo Hakimu alihoji kwa nini mshtakiwa amesafiri na kuacha kuhudhuria kesi yake bila kuomba kibali cha mahakama yake.

"Hii sasa dharau... Lissu kila wakati inapopangwa kesi yake mahakamani anashindwa kuhudhuria bila kutoa sababu ama kuomba ruhusa ya mahakama," alisema Hakimu Simba.

"Kama asingekuwa nje kwa dhamana angefanyaje? Angetumia busara kuomba ruhusa".

Wakili wa Serikali Patrick Mwita aliomba mahakama hiyo kutoa hati ya kukamatwa mshtakiwa.

Hakimu Simba alikubali ombi la Jamhuri na kutoa amri ya kukamatwa mshtakiwa na wito kwa wadhamini kufika mahakamani Novemba 21, kujieleza kwa nini wasilipe fungu la dhamana dhidi ya mshtakiwa kwa kushindwa kuhudhuria kesi yake.

Mbali na Lissu, washtakiwa wengine ni, Wahariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina na Jabir Idrisa na mchapaji wa magazeti, Ismail Mehboob.

Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa kati ya Januari 12 hadi 14, mwaka huu, jijini Dar es Salaam, Lisu na wenzake walikula njama ya kuchapisha chapisho la uchochezi katika gazeti la Mawio lenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar’.

Pia Lissu na wenzake walidaiwa Januari 14, mwaka huu, Dar es Salaam, kwa nia ya kuleta chuki na uchochezi kati ya wananchi na mamlaka halali ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, walichapisha chapisho hilo lenye uchochezi.

Aidha, Lissu alidaiwa siku hiyo kinyume cha sheria na bila ya mamlaka waliwatishia na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar wasiweze kuingia kwenye marudio ya Uchaguzi Mkuu. Washtakiwa walikana mashtaka hayo kwa nyakati tofauti na wako nje kwa dhamana.MTANZANIA
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: