BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

Mambo matano yaliyotikisa mwaka mmoja wa Rais Magufuli

Licha ya mafanikio makubwa ya Rais John Magufuli katika mwaka wa kwanza wa utawala wake, pia amekumbana na changamoto nyingi zilizotikisa Serikali yake.
Mambo matano makubwa yameingia katika kumbukumbu ya mwaka wa kwanza wa Rais Magufuli kama changamoto kuu zilizomkabili.

Bomoabomoa
Jambo la kwanza ambalo lilitikisa Serikali ya Rais Magufuli ni uamuzi aliochukua mwanzoni mwa utawala wake wa kuendesha kampeni ya kuondoa watu waliojenga katika maeneo yasiyoruhusiwa.


Bomoabomoa hiyo iliendeshwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam Januari, mwaka huu.


Kisiasa ilikuwa ni kampeni mbaya iliyoendeshwa kinyama bila kujali utu na hivyo kuishushia umaarufu Serikali ya Awamu ya Tano kwani watu wengi walioathirika walikuwa ni masikini na ndiyo waliomchagua Rais Magufuli wakitegemea utetezi, lakini wakawa waathirika wa kwanza wa utawala huu.


Bomoabomoa hiyo ililenga nyumba zilizojengwa mabondeni, kwenye fukwe za bahari ya Hindi, kingo za mito na maeneo ya wazi, waliokumbwa na bomoabomoa hiyo walilalamika kuwa hawakupewa taarifa na wala kuandaliwa sehemu mbadala ya kuhamia.


Baadhi ya wakazi ambao nyumba zao zilikuwa katika mpango wa kubomolewa ilibidi wakimbilie mahakamani kupata amri ya kusimamisha bomoabomoa hiyo.


Chombo kimoja cha habari kilionyesha kuwa nyumba 16,000 ziliwekewa alama ya kutakiwa kubomolewa na 700 zilivunjwa.
Sijui jambo gani lilitokea, lakini baada ya vikao vya kushauriana iliamriwa kusimamisha bomoabomoa hiyo.


Hata hivyo, wengi walikwisha kuathirika na baadhi ya waliobomolewa mpaka sasa wanahangaika. Bomoabomoa ile ilikuwa ni kampeni yenye lengo zuri, lakini ilifanyika kwa papara na bila kuzingatia utu.

Matangazo ya Bunge ‘live’
Ilianza kwa tangazo la Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kuwa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) halitarusha tena matangazo ya Bunge moja kwa moja, bali watarekodi na kurushwa usiku.


Sababu za uamuzi huu ilitajwa kuwa ni bajeti na pili ilionekana kuwa watu wengi wanafanya kazi mchana kwa hiyo hawapati nafasi ya kuona matangazo hayo. Kwa kurushwa usiku wengi wangeangalia.


Nape pia aliwahakikishia Watanzania kuwa hawataingilia vyombo binafsi ambavyo vingependelea kuendelea kurusha matangazo hayo.


Wengi walipinga uamuzi huo kwa sababu ni wao TBC wenye jukumu la msingi la kuwafikishia matangazo hayo wananchi, lakini Serikali ikang’ang’ania uamuzi wake, licha ya kujitokeza kwa taasisi binafsi zilizokuwa tayari kudhamini matangazo hayo kupitia TBC.


Wananchi wakaendelea kuangalia Bunge kupitia vituo binafsi. Hiyo ilikuwa Januari mwaka huu.
Hata hivyo, kikao kilichofuata cha Bunge Aprili, Serikali ikaja na uamuzi uliodhihirisha malengo yake ya kweli.


Ikaanzishwa studio rasmi ya Bunge ambayo ndiyo pekee itakayowajibika kurekodi matangazo na wengine watachukua matangazo hayo aidha ya moja kwa moja au yaliyorekodiwa kutokea huko.


Uamuzi huo, kama ilivyotegemewa haukupokelewa vyema na wadau wengi, licha ya Serikali kuutetea kwa hoja nyingi ikiwamo madai kuwa ndiyo utaratibu wa mabunge ya Jumuiya ya Madola na kwamba matangazo ya mchana yanafanya watu wasifanye kazi.


Hata hivyo, ukweli kimsingi ni kuwa hatua ile ililenga kudhibiti taarifa za Bunge, wananchi waone kile tu ambacho Serikali inataka wakione na kile ambacho haitaki watu wakione basi kiondolewe. Kuhariri siyo tatizo, bali tatizo ni nani anahariri na kwa malengo gani?


Baadaye Serikali ililegeza msimamo kwa kusema wataruhusu vituo vya redio nchini, kurusha matangazo ya vikao vya Bunge moja kwa moja, ingawa bado udhibiti upo kwa studio ya Bunge ambayo kimsingi inaonekena inadhibitiwa na Serikali.

Mgogoro wa sukari
Mgogoro huu unatajwa kuwa ulitokana na hatua ya Rais Magufuli wa kuzuia uingizwaji wa sukari kutoka nje ya nchi kwa kile kilichotajwa kuwa ni kulinda viwanda vya ndani. Mgogoro huu ulitikisa kuanzia Mei.


Baada ya marufuku ya kuagiza sukari kilichofuata ni uhaba mkubwa wa bidhaa hiyo, huku Serikali ikituhumu wafanyabiashara wakubwa kuficha sukari na Rais Magufuli akitishia kuwa angewachukulia hatua kali wahusika.


Msako mkali wa bidhaa hiyo ulioendeshwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) na Jeshi la Polisi ukaanza katika maghala ya wafanyabiashara wakubwa kitaifa, kimkoa na katika ngazi ya wilaya huku baadhi ya maeneo uonevu mkubwa ukifanyika.


Baadhi ya wafanyabiashara walijikuta kwenye matatizo, kwa sababu tu ya kukutwa na bidhaa hiyo kwenye maghala hata kama walikuwa wanauza.


Hata hivyo, waathirika wakubwa wa mgogoro ule walikuwa ni wananchi ambao walijikuta wakinunua bidhaa hiyo katika baadhi ya maeneo hadi Sh4,000 kwa kilo moja, zaidi ya mara mbili ya bei elekezi iliyotangazwa na Serikali ambayo ilikuwa ni Sh1,800.


Haishangazi basi majibu ya utafiti wa Twaweza uliotolewa Septemba 15 ulioitwa “Rais wa watu? Tathmini na matumaini ya raia juu ya Serikali ya Awamu ya Tano,” Watanzania wengi waliohojiwa walisema hatua ya Rais Magufuli ambayo hawakuipenda zaidi ni kuzuia uingizwaji sukari kutoka nje na bei elekezi.


Jitihada za kuitafuta sukari ilipofichwa na Serikali kuagiza nyingine hatimaye ilimaliza tatizo, ingawa ni mgogoro utakaokumbukwa na wengi. Serikali ilipata somo kubwa mara nyingine uamuzi ufikiriwe athari zake na siyo kukurupuka tu.

Mikutano ya hadhara
Marufuku ya mikutano ya siasa mpaka wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2020 kama ilivyotangazwa na Rais Magufuli ilikuwa ni mfano bora wa mchezaji kukamata filimbi kuchezesha mechi, akiwa bado anacheza uwanjani.


Sababu iliyotolewa na Rais Magufuli ni kuwa huu ni muda wa kufanya kazi na siyo siasa. Katika kufafanua kauli yake, Rais alisema ni wabunge na madiwani tu ndiyo wanaoruhusiwa kufanya mikutano katika maeneo yao na hawaruhusiwi kuleta wageni kutoka nje.


Pia, Rais alisema ni yeye pekee anayeruhusiwa kufanya mikutano nchi nzima kwa sababu ni eneo lake, vinginevyo vyama vya siasa visubiri mpaka mwaka 2020 wakati wa kampeni.


Msukosuko mwingine ulioikumba Serikali ambao unahusiana na haki za kiraia ni pale Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilipotangaza kufanya maandamano na mikutano nchi nzima Septemba Mosi kwa lengo la kupinga udikteta (Ukuta).


Serikali iliipa Chadema kalipia zito kuwa wangeona chamtema kuni iwapo wangeandamana na zaidi ya hapo mazoezi mazito ya kijeshi yakaendelea mitaani kuthibitisha kuwa Serikali inakusudia ilichosema.


Serikali ilidai mazoezi hayo wala siyo ya Ukuta bali ni utaratibu wa kawaida, lakini ‘utaratibu ule wa kawaida’ uliisha baada ya tishio la Ukuta kupotea.


Maandamano yale yaliahirishwa mpaka Oktoba Mosi na sasa wazo hilo limepotea kabisa, ingawa jambo la ajabu Serikali inamvumilia Profesa Ibrahim Lipumba ambaye amefanya mikutano na maandamano akaandamana na wafuasi wake mara kadhaa. Kuna nini hapo?


Kuhamia Dodoma
Kishindo kingine cha Serikali ya Awamu ya Tano kilikuja kufuatia tangazo la Rais Magufuli katika Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM, alilolirudia tena katika Siku ya Kumbukumbu Mashujaa kwamba Serikali yake itahamia Dodoma Julai 25 mwaka huu.


Katika hali iliyonyesha kutokufanyika kwa maandalizi mapema, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliagiza mawaziri wahamie Dodoma mara moja na mwenyewe akaahidi kufanya hivyo ifikapo Septemba, jambo ambalo halikutekelezeka kwa wakati.
Tangazo la kuhamia Dodoma lilipokelewa kwa namna tofauti. 


Wapo waliopongeza, walioponda na hata kuhoji uamuzi wa kuhamia Dodoma, kama vile ni jambo jipya walilolisikia kwa mara ya kwanza; lakini wenye busara zao walionyesha wasiwasi juu ya utekelezaji wa suala hilo kwa uharaka uliozungumzwa wakihoji bajeti, miundombinu na matayarisho ya wahamaji.

Hatimaye inaonekana baada ya joto la jazba kutulia, busara ikapata nafasi na sasa nasikia ratiba nzuri zaidi ya uhamaji imepangwa huku mkuu wa nchi mwenyewe akitegemewa kuhamia Dodoma ifikapo mwaka 2020.MWANANCHI

Share on Google Plus

About Juma Mtanda

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
Post a Comment