BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

RAIS MAGUFULI AFICHUA SIRI WAKATI AKIWA KATIKA ZIARA KENYA



TANGU aiingie madarakani Novemba 5, mwaka jana, kiongozi wa upinzani na Waziri Mkuu mstaafu wa Kenya, Raila Odinga, aliwahi kumtembelea Rais John Magufuli mara mbili, ikiwemo kukaa naye mapumzikoni katika Kijiji cha Kilimani, Wilaya ya Chato mkoani Geita. 


Kitendo hicho, na ingawa Rais Uhuru Kenyatta alihudhuria pia sherehe za kuapishwa kwa Rais wa tano Magufuli, kilileta minong'ono kwenye mitandao ya kijamii na picha kuwa Tanzania inaunga mkono wapinzani wa Kenyatta.

Lakini jana Rais Magufuli aliweka wazi kwamba ana uhusiano mzuri na Rais huyo wa Kenya na kufichua siri kuwa wamekuwa na mawasiliano ya simu ya mara kwa mara.

Magufuli alifichua siri hiyo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika Ikulu ya Nairobi, ambako alianza ziara ya kiserikali ya siku mbili kwa mwaliko wa Kenyatta.

Katika mkutano wa marais hao wawili na waandishi wa habari, Magufuli alisema amekuwa akiwasiliana mara kwa mara na Kenyatta, kujadiliana mambo mbalimbali ya kimaendeleo yanayohusiana na nchi zao.

Ingawa Magufuli hakuweka wazi sababu za kueleza hayo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanadhani ni kuondoa dhana kuwa huenda hakuna uhusiano mzuri kati ya viongozi hao wawili, hasa tangu Tanzania na Uganda kutiliana saini kuanza ujenzi wa mradi wa bomba la kusafirisha mafuta huku Kenya ikionekana kutengwa.

”Huwa tunapigiana simu na Uhuru Kenyatta kwa mambo mengi lakini kwa sababu simu huwa hazionekani hadharani, watu wengine hawajui, sasa basi mjue kuwa huwa tunawasiliana,” alisema.

Magufuli aliongeza: "Watanzania na Wakenya watambue sisi ni wamoja, lengo letu ni moja, nia yetu ni moja na Mungu wetu ni mmoja, tunataka kufanya kazi (na Kenyatta) kwa ajili ya maslahi ya nchi zetu."

Alisema katika kudhihirisha uhusiano wa nchi hizo, Tanzania kuna wafugaji ambao hata wanapolisha mifugo yao, hakuna uhakika kama huwa wanaangalia mipaka mradi tu kuna majani.

“Watanzania na Wakenya ni ndugu, nimetoa mfano wa Nyumbu wakati fulani wanakuja Tanzania na wakati mwingine Kenya. Watalii wakitaka kuwaona nyumbu, wanaweza kuwaona wakiwa upande wa Tanzania au wa Kenya,”alisema.

Magufuli ambaye kabla ya mkutano huo na waandishi wa habari, alipokelewa rasmi kwa kupigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa kwa heshima yake na baadaye kufanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, alisema Kenya ndiyo nchi inayoongoza kwa kuwekeza nchini kulinganishwa na nchi zingine barani Afrika.

Alisema takwimu za kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC) zinaonyesha Kenya ina jumla ya kampuni 529 zinazoendesha shughuli zake Tanzania na zimewekeza Dola za Marekani bilioni 1.7 na zimeajiri watu 56,260.

Magufuli alibainisha kuwa biashara kati ya Tanzania na Kenya imeongezeka kutoka Sh. bilioni 652.9 hadi Sh. trilioni 2.044.

"Naomba niwahakikishie kuwa uhusiano na ushirikiano wetu ni mzuri na utaendelea kuwa mzuri zaidi, na kwetu sisi Tanzania, Kenya ndiyo nchi ya kwanza kwa uwekezaji kuliko nchi zote za Afrika.

"Tunashirikiana vizuri katika uchumi, watu wetu wanafanya kazi pamoja, yapo makabila yetu ambayo yanaingiliana kwa shughuli zao za kila siku na hata wanyamapori wetu wanazunguka katika nchi zote mbili bila kujali mipaka."

Magufuli alisisitiza serikali yake itaendeleza kuimarisha zaidi uhusiano na Kenya ulioasisiwa na Rais wa Kwanza wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa Kwanza wa Kenya, Hayati Jomo Kenyatta na amewakaribisha wafanyabiashara wengi zaidi wa Kenya kuwekeza Tanzania.

"Kabla ya kuja hapa, nimekwenda kutoa heshima katika kaburi la Mzee Jomo Kenyatta, kwa kweli nimeguswa sana na kazi kubwa iliyofanywa na wazee wetu, naomba niwahakikishie kuwa tunawathamini sana ndugu zetu Wakenya na tutaendelea kufanya hivyo," alisisitiza Magufuli.

Rais Kenyatta alimshukuru Magufuli kwa kukubali mwaliko wake na amemhakikishia kuwa Kenya itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano na Tanzania.

"Kwetu sisi Tanzania ni ndugu zetu, ni kaka na dada zetu tunao ushirikiano wa siku nyingi na wa kidugu na tutahakikisha tunauendeleza ushirikiano na uhusiano huu mzuri ulioasisiwa na wazee wetu," alisema Kenyatta.

Kiongozi huyo wa Kenya alisema Tanzania na Kenya ni nchi zinazofanana kwa mambo mengi muhimu ikiwamo kubadilishana uongozi wa serikali kwa njia ya amani.

Kenyatta aliongeza kuwa katika mazungumzo yao, wamekubaliana kuwa nchi hizi zitaendelea kuzisaidia nchi nyingine za Afrika Mashariki zinazokabiliwa na matatizo mbalimbali.

Aidha, Rais Kenyatta alisema Kenya itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi ya ushirikiano ikiwamo ujenzi wa miundombinu kama vile barabara ya Bagamoyo (Tanzania) hadi Malindi (Kenya) pamoja na mambo mengine ambayo Tume ya pamoja ya ushirikiano kati ya nchi hizi mbili (Joint Commission Cooperation) itayaainisha.

Kenyatta alisema miongoni mwa masuala muhimu ambayo tume hiyo itayasimamia ni kuimarisha ulinzi na usalama kati ya nchi hizo mbili.

Jumapili ya wiki iliyopita, Msemaji wa Rais Kenyatta, Manoah Esipisu, aligusia baadhi ya mambo ambayo Kenya inatarajia kutoka kwa ziara ya Rais Magufuli kuwa ni pamoja na kusaidia kukoleza uhusiano wa nchi hizo katika nyanja mbalimbali.

Esipisu alisema viongozi wa nchi hizo watashauriana kuhusu masuala mbalimbali ya pamoja katika ngazi ya taifa kwa taifa na kanda yakiwamo ya ada ya vibali vya kufanyia kazi ambayo raia wa Kenya hutozwa pamoja na karo ya juu ambayo Wakenya hutozwa kwenye vyuo vikuu vya Tanzania.

Mengine ni suala la kuondoa vikwazo vya kibiashara baina ya nchi hizo mbili, suala la magari ya kusafirisha watalii yanayovuka mipaka.

“Muhimu katika mashauriano haya itakuwa pia kufufuliwa kwa Tume ya Ushirikiano wa Pamoja na Tanzania (JCC) ambayo ni jukwaa ambalo linaweza kutumiwa kutangaza biashara na uwekezaji baina ya nchi zote mbili.

Rais Magufuli leo anatarajiwa kutembelea kiwanda cha maziwa cha Eldoville kilichopo Karen, Jijini Nairobi na kuzindua barabara ya mchepuko ya Southern By-pass iliyopo jijini Nairobi. 


Ziara hiyo ya ughaibuni, ni ya pili ya kiserikali ya nje ya nchi kwa Rais Magufuli tangu aingie madarakani mwishoni mwa mwaka jana, baada ya Rwanda.Nipashe
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: