BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

HIVI NDIVYO AJALI YA GARI ILIVYOKATISHA UHAI WA MPIGAPICHA MPOKI BUKUKU

MPIGAPICHA Mwandamizi wa The Guardian Limited, Mpoki Bukuku (44), amefariki dunia,Bukuku alifariki dunia jana alipokuwa akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), alikokuwa amepelekwa baada ya kupata ajali ya gari katika eneo la Mwenge juzi, alipokuwa akitoka kazini.

Ajali hiyo ilisababisha Bukuku kuvunjika miguu yote miwili na mkono mmoja.

“Leo (jana), kama ilivyo kwa wengine wengi, nimepokea kwa mshtuko mkubwa na kutoamini, kuhusiana na kifo cha ghafla cha mmoja wa wapigapicha waandamizi wa The Guardian Limited, Mpoki Bukuku (44), aliyefariki asubuhi kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili.

“Kwa familia yake, wamempoteza baba, mume na zaidi ya yote rafiki wa kweli, lakini kwetu sisi The Guardian Limited, tumempoteza pia rafiki wa kweli na nguzo katika tasnia ya uandishi wa habari,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa The Guardian Limited, Richard Mgamba, katika taarifa yake.

Kwa mujibu wa ndugu wa marehemu, msiba na mipango yote kwa ajili ya mazishi ya Bukuku inafanyika nyumbani kwake, Tabata Kimanga, jijini Dar es Salaam.

Bukuku alizaliwa Machi 15, 1972 na kusoma elimu ya msingi na sekondari kabla ya kusoma diploma ya uandishi wa habari katika kilichokuwa Chuo cha Uandishi wa Habari Tanzania (sasa Shule Kuu ya Uandishi wa habari na Mawasiliano Kwa Umma- SJMC).

Alifanya kazi akiwa mpigapicha mkuu katika kampuni ya Business Times Limited (inayochapisha magazeti ya Majira na Business Times) mwaka 1999 hadi 2004; Mhariri wa Picha, Mpigapicha Mkuu na Ofisa Uhusiano wa Mwananchi Communications (2000-2014) na The Guardian Limited hadi alipofariki dunia.

TUMEPOTEZA NGUZO KATIKA TASNIA YA HABARI

Leo (jana), kama ilivyo kwa wengine wengi, nimepokea kwa mshtuko mkubwa na kutoamini, kuhusiana na kifo cha ghafla cha mmoja wa wapigapicha waandamizi wa The Guardian Limited, Mpoki Bukuku (44), aliyefariki dunia asubuhi kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Kwa familia yake, wamempoteza baba, mume na zaidi ya yote rafiki wa kweli, lakini kwetu sisi The Guardian Limited, tumempoteza pia rafiki wa kweli na nguzo katika tasnia ya uandishi wa habari.

Bukuku alikuwa mwanadamu tu kama ilivyo kwa yeyote kati yetu, lakini katika uandishi wa habari, alikuwa mtu aliyeipenda fani yake na hakuogopa kupambana alimradi apate habari nzuri. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana kuna wakati kiu yake ya kupata habari nzuri kuliko wengine wote ilimuweka matatani.

Wale wanaoelewa uandishi wa habari wa picha watabaini kwamba ujasiri na kuipenda kazi ni sifa kuu mbili za kila mpigapicha ili kupata habari nzuri na yenye nguvu. Bukuku alikuwa na sifa zote hizo mbili. Alikuwa shujaa na mwenye mapenzi na kazi yake hasa wakati akifuatilia habari kubwa kokote kule katika nchi hii.

Alipigwa na hata kuteswa na maadui wa uhuru wa vyombo vya habari, lakini bado mahaba yake katika kufanikisha habari bora hayakuzimwa.

Alikuwa mwandishi wa habari si kwa bahati mbaya, bali ni kwa kuchagua na ndiyo maana alikuwa na mapenzi wakati akitimiza wajibu wake wa kutekeleza kazi mbalimbali za kihabari alizopangiwa na wahariri wake.

Bukuku amemaliza safari yake duniani, kimwili hayuko nasi, lakini kiroho na kiuweledi, mara zote atakuwa nasi daima.

Sisi katika Kampuni ya The Guardian Limited tunaungana na famila, ndugu na marafiki katika kipindi hiki kigumu, kuombeleza msiba wa mtu ambaye tumekuwa tukifanya naye kazi kwa miaka mingi. Kampuni itaiunga mkono kwa ukamilifu familia ya marehemu Bukuku.

Kwa niaba ya wafanyakazi wote wa The Guardian Limited, kwa heshima kubwa natoa salamu zangu za rambirambi kwa mjane wa Bukuku, Lucy, watoto na wadau wote wa tasnia ya habari nchini Tanzania, kwa kifo cha ghafla na kushtua cha mmoja wetu.

Richard Mgamba
Mkurugenzi Mtendaji,
The Guardian Limited
Desemba 23, 2016

KIFO CHA MPOKI CHAWASHUTUA WENGI

“Mpigapicha maarufu Mpoki Bukuku amefariki dunia leo katika Taasisi ya Mifupa (MOI), alikokuwa amelazwa akipatiwa matibabu.

“Taarifa za kifo chake zimethibitishwa na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano kwa Umma (MOI), Almas Jumaa”, taarifa ya mwandishi wa Radio One na ITV kituo cha Morogoro ilitolewa kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook.

"Ni kweli Mpoki amefariki dunia mchana huu, alipokelewa jana usiku baada ya kupata ajali ya gari maeneo la Mwenge ITV, taarifa zaidi tutazitoa baadaye," Mushi alimnukuu Almas kupitia taarifa hiyo na kubainisha kuwa:

“Mpoki Bukuku amewahi kufanya kazi kama Mpigapicha Mkuu katika gazeti la Mwananchi, linalochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Pia amewahi kufanya kazi magazeti kadhaa yakiwamo Majira na Nipashe.”

Hivyo ndivyo ilivyokuwa katika mitandao juu ya taarifa za kifo cha Bukuku ambaye alijulikana kwa majina mengi kutokana na kuwa mtu wa watu, mpenda utani na asiyejua kuchukia.

Pamoja na kuuarifu umma juuu ya kifo hicho, Mushi kama ilivyo kwa mwanadamu mwingine alionyesha kushtushwa na taarifa hizo.

“Ni vigumu kuamini, lakini ndio ukweli. Mpigapicha za habari mahiri, mpendwa wetu, ndugu, jamaa yetu, Mpoki Bukuku, hatunaye!

Tulimpenda, lakini Mwenyezi Mungu amempenda zaidi. Madereva tusipokuwa makini barabarani, hizi ajali zitatumaliza… Mpoki, wewe mbele siye nyuma yako tutafuata. Tangulia Mpoki Bukuku.”

Lakini katika chumba cha habari cha The Guardian, taarifa zilianza kusikika chini chini, lakini baadaye zikathibitishwa kwamba Mpoki Bukuku amefariki dunia.

“Bwana kuna habari kuwa Mpoki amefariki, lakini bado haijathibitishwa,” alisema Mhariri Mtendaji wa Nipashe (Habari na Uzalishaji), Ramadhan Mbwaduke, akimweleza Mhariri Msanifu, Epson Luhwago.

Baada ya dakika chache simu yake iliita tena na kumwambia: “Bwana ni kweli…kazi ya Mungu haina makosa. Ni jambo zito tujikaze tufanye kazi.”

Baada ya kuthibitishwa, chumba kizima kilikuwa tuli kama hakuna mtu na dakika chache baadhi wakaanza kutokwa machozi na wengine kukaa kimya na kuduwaa wasijue kilichotokea.

Kuna maelezo mengi ambayo yanaweza kuelezwa kwa namna yoyote pindi mtu anapofariki dunia, lakini ukweli ni kwamba kila mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke ataishi kitambo kidogo duniani kisha ataondoka.

Mhubiri mmoja aliwahi kusema: “Kifo ni tukio ambalo limekuwapo duniani kwa miaka mingi tangu mwanadamu wa kwanza, Habili (Abel) kuuawa na ndugu yake, Kaini. Pamoja na kuwa tangu wakati huo wanadamu wamekuwa wakifa katika umri tofauti, hakuna aliyekizoea, kila kikitokea kinaonekana jambo geni.”

WENGI WASHTUKA
Maneno ya kasisi huyo yanasadifu na wengi walivyopokea kwa mshangao taarifa za kifo cha Mpoki Bukuku, ambaye hadi juzi alikuwa kazini akiendelea na majukumu yake hadi jioni.

“Mimi alinipa mkono tukiwa tunapishana kwenye mlango wa kuingilia kwenye ofisi za The Guardian. Kumbe ndiyo tulikuwa tunaagana!” alisema Beatrice Bandawe, mhariri mwandamizi wa Nipashe.

Mbali na Bandawe, wengi walimzungumzia na kutoa maoni yao kwa staili tofauti.

Mfanyakazi wa zamani wa The Guardian, Mashaka Mgeta, katika kundi la Nipashe kwenye mtandaon wa kijamii Whatsapp aliandika: “Leo (jana) unatuaga kama ulivyoshiriki kuwaaga waliotutangulia. Nasi tutakuaga kama tunavyokuaga leo.

“Kifo ni udhihirisho wa nguvu za Mwenyezi Mungu, mweza wa vyote. Kwa kifo chako Bukuku, tunaopumua tutambue ipo sekunde tutanyakuliwa kutoka duniani.

Tujinyenyekeze tukitafuta utakatifu tukufa, tufe kifo chema. Raha ya milele umpe ee Bwana, mwanga wa milele umwangazie. Mpendwa wetu Bukuku upumzike kwa Amani. Amina.”

Mwingine aliyeonyesha kushangazwa na taarifa hizo ni mwandishi wa Nipashe, Hellen Mwango aliyesema: “ Mpoki wangu, Mpoki wangu ni kweli? Why best wangu?”

Mhariri Msanifu Mkuu wa Lete Raha, Joseph Kapinga naye alisema: “Juzi alikuja ofisini na mtoto wake akamtambulisha kuwa anaitwa Junior, akanitania kusema hiyo ndiyo chata (alama) yangu ya ukweli urithi wangu wote uko kwake.

“Kumbe ni maneno ninayoyafananisha na kifo chake. Kuishi ni bahati kufa ni lazima. Tunaamka na kifo mkononi, tunashinda nacho na tunalala nacho. Pumzika kwa Amani Bukuku.”

Gwamaka Alipili, mwandishi mwandamizi wa Nipashe alisema: “Mara ya mwisho kuwa naye ni siku ya mazoezi ya Uhuru Desemba 9… tulipomaliza tukatembea kwa miguu kutoka Uwanja wa Uhuru hadi Chang’ombe huku akiniambia mdogo wangu siku moja moja fanya mazoezi, tasnia yetu ni ngumu, enzi zetu tunafanya roving (kuzunguka kupiga picha) kwa mugii bila gari.” Nitakukumbuka kaka yangu …RIP (Pumzika kwa Amani).”

“Mungu tu anajua njia zetu na miisho yake. Mpoki Bukuku tangulia mdogo wangu, ndiyo njia yetu sote. Pumzika kwa Amani. Poleni wanahabari wote, poleni familia ya kina Bukuku, poleni The Guardian Limited,” alisema Jesse Kwayu, Mhariri Mkuu wa The Guardian Limited.

Mwandishi wa Nipashe kituo cha Dodoma naye alionyesha kushtushwa na hata kusema: “Vigumu kuamini! Mpoki umeondoka kweli? Hatujui siku wala saa. Tunakuombea kwa Mungu akupumzishe kwa amani mpendwa wetu. Poleni sana familia ya The Guardian Limited.”

“Dah! Kweli umatutoka hata siamini, tumwombee Mungu ampunguzie adhabu ya kaburi,” alisema mwandishi wa zamani wa The Guardian, Judica Tarimo, huku mfanyakazi mwingine wa The Guardian Limited, Grace Nackso alisema “No Comment, inabidi kumshukuru Mungu kwa kila jambo.”

Bryceson Kayungila, mwanahabari mwingine mkongwe katika tasnia alieleze alivyomfahamu Bukuku tangu alipokuwa akifanya kazi katika gazeti la Majira.

“Ukija jeshini kufanya ‘coverage’ katika matukio ambayo tukiwaalika waandishi wa habari na wapigapicha, bila kumuona Mpoki miongoni mwa wapigapicha nilihisi kama vile safu ya picha imepunga.

“… tuliheshimiana sana, kwa kuniita, "Afande" namimi kwa unyenyekevu nilikuitikia Mpoki kwa heshima uliyonipa. Nakuombea upumzike kwa amani katika nyumba yako ya milele. Amina.”

Makonde Nyikomba Junior, mmoja wa wanatasnia ya habari, alisema: Leo (jana) mchana nasikia alipata ajali jana (juzi) maeneo ya

Mwenge na alikuwa akipata matibabu pale Moi (Taasisi ya Mifupa Muhimbili) tangu jana (leo) mpaka alipofariki dunia leo mchana. Tasnia ya habari na picha imepoteza mpigapicha mkongwe na wa muda mrefu.”

Mkuu wa Mawasiliano na Masoko wa Chuo cha Mipango Dodoma, Godrick Ngoli naye alionyesha kushtushwa na taarifa hizo huku akiomba Mwenyezi Mungu awatie nguvu ndugu, jamaa na marafiki.

Kwa hakika kila nafsi yenye uhai itaonja mauti. Kila mtu kwa wakati wake na kwa staili yake atarejea kwa Mola wake.

Kinachotakiwa ni kwa wanadamu kuamini kwamba maisha ya duniani ni ya kitambo tu na kila mmoja kuna siku asiyoijua, ataondoka katika dunia hii kama ilivyotokea kwa mpendwa wetu Mpoki Bukuku. 


Pamoja na hayo, kwa kuwa kila mmoja anajua hilo, ni vyema kuyatenda yaliyo mema huku kila mmoja akimpenda mwenzake kama nafsi yake.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: