BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

Millionaire  Ads

CHADEMA SASA WABAKIA NA SILAHA MOJA YA MDOMO WAKATI WANAIKABILI SERIKALI


MWANASHERIA Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amesema silaha yao ni mdomo na wataendelea kuitumia kuitaarifu jamii ya kimataifa juu ya vitendo alivyoviita vya kionevu wanavyofanyiwa na serikali katika kuendesha shughuli zao za kisiasa.

Lissu ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, aliyasema hayo katika mahojiano na Nipashe juu ya hatua wanazochukua baada ya Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, kudai kuwa serikali imekuwa ikilitumia Jeshi la Polisi kuwahujumu kisiasa.

Mtaalamu huyo wa sheria alisema wiki iliyopita kuwa chama hicho hakina mbinu nyingine ya kupambana na "hujuma" hizo zaidi ya kuchukua hatua za kisheria na kupaza sauti kuziarifu jumuiya za kimataifa juu ya kile kinachoendelea.

"Sisi (Chadema) hatuna majeshi ya kupambana na Jeshi la Polisi," Lissu alisema. "Silaha yetu ni mdomo, tutapiga kelele, dunia itatuelewa.

"Jamii ya kimataifa itatuelewa tu kama ambavyo Amerika (Marekani) walivyofuta misaada kwa Tanzania na sasa Umoja wa Ulaya nao wameanza kuchukua hatua.

"Serikali itatuelewa tu."
Serikali ya Marekani, kupitia taasisi inayohusika na misaada ya maendeleo ya MCC, ilitangaza kusitisha awamu ya pili ya misaada yake kwa Tanzania Machi 29, mwaka jana.

MCC ilisitisha misaada hiyo baada ya kutoridhishwa na kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa 2015 na kupitishwa kwa Sheria ya Makosa ya Mtandao mwaka huo pia, mambo ambayo yalipingwa pia na Chadema chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi(Ukawa).

Msaada wa awamu ya pili huo kutoka MCC ulikuwa wa dola milioni 472.8 (sawa na Sh. bilioni 946) ambazo ni chini kidogo ya makusanyo ya Mamlaka ya Mapato kwa mwezi.

Katika awamu ya kwanza ya misaada ya MCC kwa nchi, Tanzania ilipokea dola milioni 698 (sawa na Sh. Trilioni 1.4) ambazo zilitumika kugharimia miradi ya barabara na umeme vijijini.

Matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar yalifutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi visiwani (Zec), Jecha Salim Jecha kwa maelezo ya kutokuwa huru na haki, huku wagombea wa Chama cha Wananchi (Cuf) wakionekana kuongoza kura za Urais na Ubunge.

MIEZI MINANE
Kauli ya Lissu ilitoka muda mfupi baada ya Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Lindi, Selemani Matthew Luwongo, kuhukumiwa kifungo cha miezi minane gerezani kwa kosa la kufanya mkusanyiko bila kibali.

Mbali na Luwongo, kiongozi wake mwingine, Katibu wa Kata ya Nyangamala, Ismail Kapulila, alifungwa kifungo kama hicho na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Lindi wiki iliyopita.

Hukumu hiyo pia ilitolewa ikiwa ni saa chache baada ya Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Mbowe, kulalamikia jijini Mwanza kile alichokiita njama ya kukihujumu chama hicho kutokana na Jeshi la Polisi kuwakamata baadhi ya viongozi na kuwafungulia mashtaka.

Luwongo na Kapulila walihukumiwa kifungo cha miezi minane jela, baada ya kupatikana na hatia ya kufanya mkusanyiko bila kibali.
Luwongo na Kapulila walifungwa baada ya mahakama kujiridhisha pasipo shaka kwamba Aprili 3, mwaka jana, katika Kata ya Nyangamala, walifanya mkusanyiko usio halali.

Mbowe, akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza alidai kuwapo kwa hujuma hizo dhidi yao kutokana na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa, kukamatwa na kushikiliwa kwa saa kadhaa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita wakati akienda kwenye mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani, uliofanyika jana katika kata 20 za Bara.

Lowassa ambaye aligombea urais kupitia chama hicho na kuungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), alikamatwa na polisi mkoani humo alipokuwa safarini akitokea Kagera.

Mbowe pia alilalamikia hukumu ya kifungo cha miezi sita bila faini iliyotolewa kwa Mbunge wa Kilombero mkoani Morogoro kupitia chama hicho, Peter Lijualikali Januari 11.

Mbunge huyo aliye katika Gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam, alihukumiwa kifungo hicho baada ya kupatikana na hatia ya kufanya fujo kwenye mkutano wa halmashauri. 


Lissu pia aliiambia Nipashe wiki iliyopita kuwa chama chake kilishaanza mchakato wa kuomba dhamana ya Lijualikali katika Mahakama Kuu ili awe nje wakati akisubiri kukatwa na kusikilizwa kwa rufani yake dhidi ya kifungo hicho.
Share on Google Plus

About Juma Mtanda

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
Post a Comment
Millionaire  Ads