BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

CHUNGA VIDOLE VYAKO SHERIA YA MTANDAO IPO



Mwaka 2004 wakati mtandao wa kijamii wa Facebook unaanzishwa wengi walifurahi. Walitarajia mengi yatakayoletwa na mtandao huo. Hata hivyo, kwa zaidi ya miaka 10 walikata kiu yao.

Baada ya Facebook, mitandao mingi mingine imevumbuliwa na kuiunganisha dunia. Sasa hivi mtandao huo mkongwe umenunua mitandao mingine na kuiweka kwenye orodha yake. PrivateCore, Oculus VR, WhatsApp na Instagram ni miongoni mwa kampuni tanzu za mtandao huo.

Watumiaji wa mitandao ya kijamii wanaongezeka kadri muda unavyoenda. Tanzania haipo nyuma. Tunayo mamia ya watu mashuhuri ambao akaunti zao zimethibitishwa, ishara ya kutambuliwa na kampuni husika.

Kampuni kubwa za simu za mkononi zinashindana kuunda simu za kisasa zinazotumia intaneti inayofanikisha mitandao hiyo. Smartphone siyo lugha ngeni masikioni mwa wengi. Wenye uwezo wanatumia tablets, notepads, ipads au laptops.

Wakati Samsung, Apple na kampuni nyingine kubwa duniani zikishindana kuunda vifaa hivyo vya mawasiliano, tena kwa teknolojia kubwa, wadau wengine pia wanatekeleza wajibu wao. Serikali ya Tanzania ina miradi kadhaa yenye dhamira ya kusambaza intaneti kwa wananchi.

Kwenye ilani yake ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, chama tawala kilieza kwamba kinataka kuongeza matumizi ya intaneti ili ifike asilimia 25 ya wananchi wote mwaka 2025. Siyo Tanzania peke yake, kwenye baadhi ya mataifa, mfano Estonia, intaneti ni haki ya binadamu.

Taifa zima lina mtandao wa intaneti ya uhakika. Kila shughuli inaendeshwa kimtandao. Wanajitahidi kuondokana na uchumi wa karatasi, ingawa hawajafanikiwa kwa asilimia 100. Huenda Tanzania na nchi nyingine zinazoendelea zikafika huko.

Hakuna haki isiyokuwa na utaratibu kwa mujibu wa wanasheria na wanasiasa. Baada ya zaidi ya miaka 10 ya kutumia intaneti na huduma za Facebook kwa jinsi kila mmoja anavyojisikia, Serikali imeona haja ya kutunga sheria itakayoongoza mijadala ya sekta hiyo.

Ndiyo, mambo yalikuwa hayaendi sawa. Wapo wengi waliochafuka kutokana na vidole vya mahasimu wao. Ambao kupitia mguso mmoja kwenye skrini za simu zao waliweza kutuma picha zisizo na maadili kwa jamii hii. 


Wapo walioandika ujumbe usiokuwa na ukweli, ukapotosha, kusononesha na kushusha heshima ya mlengwa mbele ya jamii.

Mwaka jana, Sheria ya Makosa ya Mtandao ilitungwa. Haijawagusa wengi ingawa kila mmoja ni mshukiwa. Unashukiwa kwa sababu unaweza ukaenda kinyume na matakwa yake. Ukibainika, muda wowote, utapaswa kutoa maelezo yanayojitosheleza.

Wapo baadhi ya ‘ma-admin’ wa magrupu ya mitandao ya kijamii ambao wameamua kuyafunga kutokana na wanakikundi wenzao kuenenda kinyume na sheria hiyo. Ni bora ukafanya hivyo kabla halijakukuta kuliko kuongoza watu wasiotaka kuheshimu dola.

Kumbuka, Jeshi la Polisi lipo macho wakati wote kuhakikisha linalinda raia na mali zao. Hii ni pamoja na heshima yao mtandaoni. Chochote kinachofanywa na vidole vyako, chunga, kisije kikakuletea balaa ukatupwa korokoroni.

Ni wajibu wa kila mmoja wetu kujua sheria za nchi na kuziheshimu. Kupuuza chochote ni kukaribisha matatizo ambayo mwisho wa siku hakuna rafiki, ndugu wala jamaa atakayeweza kukusaidia. 


Ili kuepusha shari inayoweza kujitokeza ni busara kuvikanya vidole vyako sasa ili tuendelee kufurahia uwepo wa dunia na vilivyomo. 

Kufanya kinyume na hapo ni kutoa mwaliko wa jamaa zako kuja kukuwekea dhamana mahakamani yoyote utakayofikishwa na kusomewa mashtaka yako kabla hawajalifahamu gereza utakalokuwa ukifundishwa utii wa mamlaka zilizopo.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: