BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

HALI BADO TETE KWA WATU 14 WALIOFUKIWA NA KIFUSI MGODI WA DHAHABU GEITA

HALI bado ni tete katika kazi ya uokoaji wa watu 14 waliofukiwa na kifusi katika Mgodi wa Dhahabu wa Kampuni ya RZ Union Mining Ltd uliopo Kata ya Nyarugusu mkoani Geita, kutokana na hadi jana kutookolewa mtu yoyote.

Hata hivyo pamoja na sintofahamu hiyo juhudi za uokoaji zinaendelea kwa kasi, huku Mkuu wa Mkoa wa Geita, Ezekiel Kyunga akisema bado anayo imani kuwa watu hao wataokolewa wakiwa hai.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema moja ya kazi iliyoendelea jana ilikuwa ni kwa vikosi vya uokoaji kuendelea kuchimba kifusi ili kutafuta njia ya kuwafikia waathirika huku mipira zaidi ya Oxygen ikiingizwa chini ya mgodi waliko watu hao ili kuwaongezea hewa.

Watanzania 13 na raia mmoja wa China walifukiwa na kifusi juzi usiku baada ya udongo kukatika na kuziba mlango waliokuwa wakitumia kuingia na kutoka. Mkuu wa Mkoa aliliambia gazeti hili jana kuwa hadi jana walikuwa bado hawajafanikiwa kuwafikia watu hao lakini kazi ya kuwafuata waliko inaendelea kwa kasi.

Akizungumza akiwa eneo la tukio, Kyunga alisema vyombo mbalimbali vya uokoaji kwa kushirikiana na wananchi walikuwa wanaendelea kuchimba kifusi ili kuwasaka mahali walipo mgodini.

“Kutokana na uzoefu wa kazi na matukio kama haya yaliyowahi kutokea tuna matumaini makubwa ya kuwaokoa wakiwa hai kutoka na mlango ndiyo uliojiziba na udongo na watu hao wako katika mtaro wa mlalo hivyo kwa kutumia Oxygen tunayoingiza kwa mipira tutawakuta wakiwa hai,” alisema.

Kyunga alieleza kuwa watu wengi wapo katika eneo hilo wakiwemo ndugu wa waliofukiwa lakini kwa juhudi wanazoziona za uokoaji wametulia na kufuata maelekezo wanayopewa ikiwemo kukaa mita 500 kutoka eneo la tukio.

Alisema wametakiwa kukaa mbali na eneo hilo la uokoaji ili wasisongamane na watu wanaoendelea na uokoaji ili kuwapa fursa nzuri ya vikosi vyote kujadiliana namna ya kufanywa kwa ajili ya kufanikisha uokoaji huo.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Latson Mponjoli alisema juhudi za uokoaji zinaendelea kwa ushirikiano wa vikosi vya uokoaji vya Kampuni ya Geita Gold Mine (GCM), Jeshi la Zimamoto na Polisi pamoja na kikosi cha ukoaji cha Sekta ya Madini. Alisema hali ni shwari katika eneo hilo na wana matumaini ya kuwafikia watu hao wakiwa hai.

Kampuni inayoendesha mgodi huo imesema kutokana na kitabu cha orodha ya watu wanaojiandikisha kuingia mgodini, kuna majina ya Watanzania 12 na Mchina mmoja waliofukiwa kifusini. 


Ilielezwa kuwa watu pia waliomshuhudia Mtanzania mmoja akingia mgodini humo bila kujiandikisha na hivyo kufanya waliofukiwa kufikia 14.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: