BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

HAYA NDIO MAISHA YA GODBLESS LEMA NDANI YA GEREZA LA KISONGO MCHANA NA USIKU MKOANI ARUSHA

 
MBUNGE wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, amechanganywa na mahabusu wengine katika Gereza Kuu la Arusha, Kisongo, lakini hali hiyo haimpi shida, imeelezwa.

Akizungumza na Nipashe jijini hapa jana, mke wa Lema, Neema, alisema mumewe haishi katika selo ya peke yake kama ambavyo watu wengi wanadhani.

"Amechanganywa na mahabusu wengine, lakini anasema hiyo haimpi shida," alisema Neema.

Neema alisema amekuwa akimpelekea mumewe huyo milo mitatu ya chakula kila siku.

Naye Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, ambaye kwa pamoja na Mwenyekiti Freeman Mbowe walimtembelea Lema jana gerezani hapo, alisema asilimia 75 ya mahabusu walioko katika gereza hilo wana haki ya dhamana.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Lissu alisema chama kinakusudia kuandika barua kwa vyama vya mawakili vya Afrika Mashariki na Tanganyika Law Society, ili waungane kupinga vikali ukiukwaji wa haki ya dhamana anayonyimwa lema.

Akizungumza jana Jijini Arusha pia katika ofisi za chama hicho, Lisu akiwa ameambatana na Mbowe, Mbunge wa Bunda Mjini, Esta Bulaya na Mbunge wa Arumeru Magharibi, Gibson Meseyeki, alisema:

“Kesi inayomkabili Lema ni ya uchochezi ambayo kimsingi mimi kama wakili sijawahi kuona kosa la kuota (likawa) ni kosa la uchochezi.

"Ikibidi chumba cha mahakama kujaa mawakili tujae sababu hata wananchi wake pia wanazuiwa kuingia mahakamani.
"Sasa acha tujae wenye majoho ya sheria tupambane na tuionyesha dunia mahakama yetu inayumba."

Alisema kimsingi Mahakama Kuu ilipopokea rufaa ya serikali na kuamua kuisikiliza ilitakiwa kuendelea na msimamo wake wa kutoa maamuzi, lakini sio kusitisha kutoa uamuzi kwa madai imefungwa mikono yake kutokana na upande wa Jamhuri kusema umekata rufani Mahakama ya Rufani.

“Hawa serikali ndio walikata rufani sasa imesikilizwa na kabla ya kutoa uamuzi inachezewa kwa kudai wanakusudia kukata rufani Mahakama ya Rufani," alisema.

"Huu ni mchezo ambao anafanyiwa Lema ili kuikomoa familia yake na wananchi wa Jimbo la Arusha, kitu ambacho wahusika wakuu wa kusimamia haki ya mhimili wa sheria hawapaswi kulifumbia macho.”

Naye Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Mbowe, alisema kuwa wamemtembelea Lema Gereza Kuu la Kisongo ambako yuko mahabusu tangu Novemba 2 mwaka jana, na wanashukuru hana hofu na anaendelea vizuri.

Alisema yeye kama kiongozi amejitahidi kuzungumza na viongozi wakuu wa nchi kuhusu suala hilo, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.

Mbowe alisema wanalaani kitendo anachofanyiwa Lema. “Hatuogopi kusema ukweli hata kama tutafungwa, hivi sasa kumekuwa na visa kwa wafuasi wa upinzani,”alisema.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: