BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

NCHI ZA CHINA, URUSI NA MAREKANI ZINAVYOTISHIA AMANI YA DUNIA KWA NGUVU YA KIUCHUMI

Image may contain: 3 people, suit

Na Luqman Maloto.

Hegemony ni nadharia ya dola moja kuongoza nyingine kisiasa, kiuchumi na kijeshi. Taifa moja linakuwa kiranja wa mataifa mengine duniani.

China, Urusi na Marekani ndiyo wanaopambana sasa hivi kujisimika ukuu wa Hegemony. Kila mmoja anataka awe kiranja wa dunia kiuchumi, kisiasa na kijeshi.

Mipango ya dola moja kuwa kiranja wa dunia haijaanza leo. Karne 4 Kabla ya Ujio wa Kalenda, Ugiriki ya Kale ilitawaliwa na Alexander III of Macedon, kwa umaarufu zaidi alifahamika kama Alexander the Great.

Alexander aliunda jeshi lake na kutangaza azma yake ya kutawala dunia akitokea Ugiriki, kwamba dunia nzima ingefuata amri zake. Viongozi wa dola nyingine wawe kama magavana, wenye kufuata maagizo yake.

Nyakati hizo Alexander the Great alikuwa anajidanganya tu. Ulimwengu wa kijima wakati huo, angeweza vipi kuifikia dunia yote? Akiwa Ugiriki hakuwa akijua chochote kuhusu nguvu za China na maeneo mengine.

Hata hivyo, Alexander anabaki kuwa mfano hai wa ulimwengu na walimwengu. Ni kipimo cha akili kwa dunia na busara za watu wake. Kwamba nyakati zote tamaa za kutawala dunia zimeendelea kuwepo.

Taifa moja linakuwa na sera ya kutaka kutawala dunia. Wakuu wa mataifa mengine wawe wafuata maagizo. Taifa moja linakuwa na mipango endelevu ya kutawanya mabavu yake ya kijeshi duniani ili kumiliki uchumi wa dunia.

Unapokuwa na uchumi imara pamoja na uwezo mkubwa wa kijeshi, dunia utaielekeza upande wako. Na hapo ndipo kwenye vita kubwa ya China, Marekani na Urusi.

MAPAMBANO NI MAKUBWA
Marekani ilipofanya uchaguzi Novemba mwaka jana, China na Urusi hawakulala. Ilikuwa muhimu mno kwao kwa ushindi wa kiongozi mwenye sura zenye kupunguza mabavu ya Marekani duniani.

Hii ni sababu vyombo vya usalama vya Marekani vimekuwa vikali sana baada ya kubaini kuwa Urusi iliwafanyia udukuzi kwenye uchaguzi mwaka jana, hivyo kuchangia ushindi wa Rais wao wa 45, Donald Trump.

Uamuzi ambao Rais wa 44 wa Marekani, Barack Obama aliuchukua haraka, ulikuwa kuwafungashia virago maofisa wote wa Urusi na kuwarejesha kwao, kisha akafunga ofisi zote za Urusi, hivyo kuvunja uhusiano wa kidiplomasia.

Kwa Marekani, kudukuliwa uchaguzi na Urusi ni kebehi, dharau, vilevile ni hatua ya juu ya kushindwa kama taifa. Historia ya mapambano kati ya Urusi na Marekani ndiyo sababu ya chuki kubwa iliyopo.

Urusi inarejea upya kupitia Shirikisho la Urusi baada ya anguko la dola ya Umoja wa Nchi za Kisovieti (USSR) mwanzoni mwa miaka ya 1990. Nayo ina maumivu yake kwa sababu Marekani ndiyo iliyoiandama Sovieti na kuchochea nchi za USSR kujitenga na umoja huo.

Marekani na Urusi ni nchi zenye kisasi. Urusi inaamini kuwa kama USSR isingeanguka, maana yake ubabe wa Marekani leo usingekuwepo. Marekani haitaki Urusi irejee nguvu zake za Sovieti.

Wakati huohuo ukubwa wa China, watu wengi ilionao, ustawi wake wa kiuchumi kupitia sera zake za Ukomunisti na jinsi inavyojitandaza duniani, ni sababu ya Marekani kukosa usingizi. Ni mapambano.

SIASA NA UCHUMI

Katika eneo la uchumi, Urusi inaachwa nyuma na sasa ushindani unaonekana kati ya China na Marekani. Kijeshi mataifa yote hayo yapo imara na kwenye siasa tayari Urusi imeshaonekana tishio kwamba kumbe inaweza mpaka kuiingilia Marekani.

Mataifa yote hayo yana uchokozi wa ajabu kwa dunia. Yametengeneza mashushushu ambao wamesambaa ulimwenguni kote. Sababu za uwepo wa mashushushu hao ni maslahi ya nchi hizo.

Tabia ya China kuwa rafiki wa mataifa madogo kisha kutengeneza urafiki uliokomaa, imeifanya nchi hiyo kuwa na mtandao mpana wa kiuchumi duniani. Hali hiyo iliishtua Marekani, nayo ikaamua kujishusha ili kutengeneza ushirikiano mpana na mataifa madogo.

Ndiyo maana China na Urusi wamekuwa na furaha kwa ushindi wa Trump kwa sababu wanaamini kiongozi huyo hatataka kujishusha kama walivyokuwa marais wa tatu waliomtangulia, ambao ni Obama, George Bush na Bill Clinton.

Ingekuwa pigo kubwa kwa China na Urusi kama Hillary Clinton angeshinda kwa sababu tayari alishakuwa na uelekeo wa kutengeneza ushirika mpana wa kiuchimi kwa nchi ndogo.

Imani yao ni kuwa miaka minne, zaidi ikiwa nane ya urais wa Trump ni mingi na inatosha kuvuruga nguvu ya Marekani kisha wao kujisimika na kujitanua. Ndiyo maana vigogo wa Marekani, wenye kujua hili hawakumtaka na wanaendelea kutomtaka Trump.

Wanafahamu kuwa ulimwengu wa sasa huwezi kuitawala dunia kwa mtindo wa Adolf Hitler. Dunia ya sasa inataka taifa imara lishuke na kujigeuza msaada kwa mataifa madogo. Jinsi taifa kubwa linavyosaidia nchi ndogo ndivyo linavyoingia ndani na kujisimika.

Afrika ya leo ni mtumiaji mkubwa wa bidhaa kutoka China, hilo halikutokea mara moja. Kuna maandalizi makubwa yanafanyika. China ni mzalishaji, kwa hiyo uimara wake unategemea zaidi soko katika nchi ambazo huzisaidia.

JESHI NA UJASUSI

Ufahari wa mataifa hayo upo kwenye eneo hili. Mataifa hayo yamewekeza nguvu kubwa ya ujasusi. Urusi na Marekani zina mashirika ya upelelezi mengi ambayo kwa asilimia 90 hufanya kazi ya ushushushu duniani.

Marekani ina mashirika ya upelelezi (intelligence agencies) zaidi ya 17 na kila moja inafanya kazi kwa mipaka bila kuingiliwa. Urusi ina mashirika ya upelelezi 15. China yapo mashirika zaidi ya 11.

Nchi zote hizo hufanya Espionage. Yaani huingia kwenye nchi mbalimbali na kupeleleza kisha kuchukua taarifa za siri za nchi husika bila kibali kisha kuzifanyia kazi.

Upelelezi huo huzisaidia nchi hizo kujipanga. Mathalan, Urusi inakuwa inajua mipango ya siri kati ya Marekani na Uganda kabla mipango yenyewe haijatangazwa.

Kupitia upelelezi huo nchi hizo huweza kuchunguza nguvu za kijeshi za mataifa mengine kisha kujua uimara na udhaifu wake. Vilevile kutambua mipango ya kijeshi ya nchi na ukubwa wa silaha zake.

Mashirika hayo yanapofanya upelelezi wake na kugundua nchi inayopishana na taifa hasimu au kikundi cha watu wanaoishi mbali wasiokubaliana na Serikali ya taifa hasimu, huunga mkono jitihada zote.

Mathalan, Marekani wanaunga mkono juhudi za Tibet kujitenga na China, kwa hiyo hufadhili makundi ya Watibet duniani kote ili kufanikisha mpango huo. Marekani pia inaunga mkono uhuru watu wa imani ya Falun Gong ambayo wanapigwa vita na Chama cha Kikomunisti cha China pamoja na Serikali.

Hivyo basi, popote utakapomwona adui wa Marekani basi huyo atakuwa rafiki wa China na Urusi. Adui wa Urusi ni rafiki wa Marekani. Mgogoro wa Ukraine na Urusi, Marekani ipo na Ukraine.

Marekani ilimsaidia Osama bin Laden na Mullah Omar mwishoni mwa miaka ya 1980, wakati Taliban walipokuwa wanapambana na Urusi nchini Afghanistan. Kimsingi mataifa hayo huchokonoana na hapo ndipo kwenye hatari.

JEURI YA JESHI

Jeshi la China lina askari takriban 2.3 milioni, Marekani wana zaidi ya 1.4 milioni, wakati Urusi ina wanajeshi 771,000. Vilevile nchi hizo zina utaratibu wa kujiwekea akiba ya askari, China akiba yao ni 2.3 milioni, Marekani 1.3 milioni na Urusi 1.9 milioni.

Bajeti zao; mwaka jana, Jeshi la Urusi bajeti yake ilikuwa dola 93.9 bilioni, sawa na Sh210 trilioni. Marekani walitumia dola 590 bilioni, Sh1,322 trilioni. China walitumia dola 150 bilioni, Sh336 trilioni. Bajeti ya Marekani ni kubwa sana kwa sababu wanatumia fedha nyingi kujilinda.

Nchi zote hizo zinamiliki silaha za nyuklia, kwa hiyo hakuna ambayo ina unyonge kwa mwenzake. Kwa ubabe kabisa, Marekani, Rais wao kila anapokuwa pembeni yake kuna askari aliyebeba mkoba mweusi. Mkoba huo ndani yake huwa na kitu mfano wa laptop, unaitwa Nuclear Football.

Hiyo Nuclear Football ni mashine isiyo na waya (wireless machine) ambayo Rais wa Marekani popote anapokuwa anaweza kuilipua nchi yoyote aitakayo kwa kutumia alama yake ya kidole. Kwa mantiki hiyo, Marekani wametega nyuklia kuelekea nchi yoyote dunia. Ni suala la Rais wao kubonyeza kidole kwenye Nuclear Football.

Mkoba wa nyuklia wa Urusi unaitwa Cheget ambao Rais wa Urusi muda wote yupo nao pembeni. Kama akitaka kulipua nchi yoyote ni suala la kufungua mkoba na kuchagua sehemu ya kuelekeza shambulio. Watu wengine wenye dhima ya kutunza Cheget ni waziri wa ulinzi na mnadhimu wa jeshi.

Upande wa China imekuwa na siri kubwa kuhusu mamlaka ya ulipuaji wa mitambo yao ya nyuklia, ingawa ipo dhana kuwa Rais na Mwenyekiti wa Chama cha Kikomunisti, wanayo mikoba yenye mashine za ulipuaji ila wanafanya siri.

Kuhusu silaha, mataifa hayo yanaendelea na ushari wao. Marekani wanamiliki ndege za Stealth Fighters ambazo zimetengenezwa kwa teknolojia ya hali ya juu kiasi kwamba zinaweza kuvuka anga yoyote pasipo kuonekana na rada za nchi husika. Ndege hizo zipo za aina mbili, 187 F-22s na F-35.

China na Urusi nazo zipo kamili. China ina aina nne ya Stealth Fighters, ambazo ni J-31, J-20, F-35 na F-22. Urusi wao wana aina moja tu ya Stealth Fighters ambayo ni F-22. Aina nyingine ambayo itakuwa ya pili kwa Urusi ni T-50 ambayo bado hazijazinduliwa.

Mataifa hayo yanamiliki vifaru vizito zaidi vya kivita, manowari pamoja na meli. Zipo pia ndege zisizo na marubani.

JEURI YA UPELELEZI

Nchi hizo zinatumia nguvu kubwa kufanya ujasusi duniani, wakiamini kuwa ndiyo njia yao ya kutanua mabavu yao. Hapa utaona vyombo vya mataifa hayo katika ujasusi na kazi zao.

URUSI; Jumuiya ya Ujasusi ya Urusi inaundwa na vyombo 15. 1. Huduma ya Ujasusi wa Kimataifa (SVR), wao huripoti kwa Rais. 2. Kurugenzi ya Ujasusi ya Jeshi la Urusi (GRU). 3. Kurugenzi Kuu ya 12 (12th Chief Directorate) hii inafanya kazi chini ya Wizara ya Ulinzi na inashughulika na usalama wa nyuklia.

Namba 4. Shirikisho la Usalama (FSB), inahusika na usalama wa nchi pamoja na mapambano dhidi ya ugaidi. 5. Shirikisho la Udhibiti wa Teknolojia (FSTEK) ambayo jukumu lake ni kuchunga mawasiliano na kudhibiti wizi wa kiteknolojia. 6. Shirikisho la Ulinzi (FSO), jukumu lao ni kutoa walinzi binafsi kwa viongozi.

Namba 7. Shirikisho la Ulinzi wa Rais (SBP), wao kumlinda Rais tu. 8. Kurugenzi Maalum ya Mawasiliano (SSSR), kulinda mawasiliano ya Serikali. 9. Kurugenzi Kuu Maalum (GUSP), jukumu lake kulinda hazina za Serikali. 10. Shirikisho la Forodha (FTS), kupambana uharamia wote wa forodha.

Namba 11. Shirikisho la Mihadarati (FSKN), jukumu lake ni kupambana na dawa za kulevya. 12. Shirikisho la Kudhibiti Pombe (FSKA), kupamabana na pombe bandia. 13. Shirikisho la Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi (MVD), kushughulikia utekelezwaji wa sheria.

14. Shirikisho la Polisi (Politsiya) yenyewe ni upelelezi wa mambo yote ya kipolisi. 15. Shirikisho la Udhibiti wa Fedha (Rosfinmonitoring) ambalo hupambana na utakatishwaji wa fedha haramu pamoja na ugaidi.

MAREKANI; 1. Central Intelligence Agency (CIA), hawa ni wambea wa dunia. Marekani kuna ofisi tu lakini wenyewe wametawanyika duniani wakipeleleza Serikali zote na kupeleka ripoti. Hawafanyi kazi ndani ya Marekani na hawakamati mtu, wao ni ushushushu tu.

2. Federal Bureau of Investigation (FBI), wajibu wao ni kufanya upelelezi na kukamata. Awali eneo la kazi lilikuwa ndani ya Marekani tu lakini baada ya ugaidi kutikisa dunia, kwa sasa hufanya kazi nchi mbalimbali.

3. National Reconnaissance Office (NRO), yenyewe inahusika na ushushushu wa satelaiti za Marekani na nchi nyingine duniani. 4. National Security Agency (NSA), hii ni taasisi ya kunasa signo za mitandaoni na kukusanya taarifa mbalimbali. Hawa hutumia teknolojia ya kuingilia na kunasa mawasiliano ambayo initwa SIGINT.

Kwa Marekani, NSA ilikuwa siri mpaka mwaka 2013, pale mtundu wa kompyuta, Edward Snowden ambaye aliwahi kufanya kazi NSA alipovujisha siri ya uwepo wa taasisi hiyo. Kwa kosa hilo, Marekani wamepanga ‘kumla nyama’ Snowden siku wakimkamata. Snowden kwa sasa amepewa hifadhi Urusi.

5. Defense Intelligence Agency (DIA), hawa ujasusi wao ni kuingia kwenye majeshi ya Serikali mbalimbali duniani kisha kuchukua taarifa zote za kijeshi. 6. National Geospatial-Intelligence Agency (NGA), jukumu lake ni kupeleleza kila shughuli inayofanywa na binadamu duniani kote.

Kwa Marekani, CIA, NSA, NRO, DIA na NGA ndiyo huitwa Big 5, kwa maana hiyo hayo matano hata FBI ni cha mtoto.

7. Office of Terrorism and Financial Intelligence (TFI), wao ni kupambana na ugaidi pamoja na kudhibiti fedha zote chafu. 8. Bureau of Intelligence and Research (INR), jukumu lao ni kuwapa mabalozi wa Marekani duniani kote huduma ya ujasusi. 9. Twenty-Fifth Air Force (25 AF), ushushushu wa anga kuhusu masuala ya kijeshi na teknolojia.

10. Office of Intelligence and Analysis (I&A), hii haitoki nje, yenyewe jukumu lake ni kuilinda ardhi ya Marekani. 11. Marine Corps Intelligence (MCI), ushushushu wa majini. 12. Drug Enforcement Administration (DEA), kupambana na dawa haramu. 13. United States Army Intelligence and Security Command (INSCOM), kunasa na kuripoti moja kwa moja taarifa za Jeshi la Marekani.

14. Coast Guard Intelligence (CGI), majasusi wa Jeshi la Marekani ambao hufanya kazi zao pwani kuona kinachotoka na kuingia baharini. 15. Office of Intelligence and Counterintelligence (OICI), kufanya ujasusi kuhusu masuala yote yenye kuhusu nishati. 16. Office of Naval Intelligence (ONI), hii pia hushughulika na ushushushu wa majini.

17. United States Secret Service (USSS), hawa majukumu yao ni mawili, kulinda viongozi wa Marekani ndani na nje, pili kulinda uhalifu wa kifedha kwenye hazina ya Marekani.

CHINA; Masuala yote ya ujasusi wa kimataifa, China limeyakasimisha kwa Wizara ya Usalama wa Nchi (Guojia Anquan Bu). Wizara hiyo ndiyo idara kuu ya ujasusi na majasusi wake wengi wamesambazwa ulimwenguni kote.

Hata hivyo, zipo idara nyingine 10 ambazo hufanya kazi za ujasusi ndani ya China. Hivyo kuzidi kuonesha kuwa mataifa hayo matatu, Marekani, China na Urusi yanatumia bajeti kubwa kwa ajili ya ushushushu.

HATARI YA ULIMWENGU

Kwa nini mataifa hayo hayatosheki na himaya zao mpaka kutaka kujitanua kwenye dola nyingine? Ipo nadharia pia ya matumizi ya sarafu moja, kwamba atakayefanikiwa kuitawala dunia kiuchumi, kisiasa na kijeshi, ataweza kulazimisha mataifa yote yatumie sarafu yake.

Hivi karibuni, CIA walitoa ripoti jinsi walivyoifanyia ujasusi Serikali ya Awamu ya Kwanza Tanzania, iliyoongozwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kwamba walitamani kumshawishi Mwalimu Nyerere aache urafiki na China ili awe upande wa Marekani lakini haikuwezekana.

Mbinu hizo hatari yake ni kuwa utafika wakati mataifa hayo yatagombea uungwaji mkono. Yanapokuwa yanaingilia siri za nchi nyingi ni tabia mbaya na ni uonevu, maana nchi ndogo hazina uwezo kuziingilia zile kubwa.

Tabia ya taifa moja likitaka kulipiga lingine, moja kati ya mataifa hayo matatu yanaingilia kati upande wa pili, itakuja kutokea zinapigwa Urusi na Marekani au Marekani na China. Ugomvi wa wababe hao utaitikisa dunia hata kama havitatokea Vita Kuu ya Tatu ya Dunia.

Wababe hao wote wanamiliki nyuklia. Wanavyochokozana, itakuwaje wakikasirishana? Halafu walivyo wababe, huwa hawataki mataifa madogo yamiliki nyuklia ila wao tu.
Share on Google Plus

About Juma Mtanda

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
Post a Comment