BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

PPF, NSSF KUFUFUA KIWANDA CHA SUKARI CHA MAGEREZA MOROGORO.


Kaimu kamishna jenerali wa magereza, Dk Juma Malewa akielezwa jambo na Msimamizi wa kiwanda cha sukari cha Magereza Mbigiri (kilichokufa) wakati wa ziara ya wakurugenzi wakuu wa mifuko ya hifadhi ya jamii wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara na mfuko wa pensheni wa PPF, William Erio walipokuwa wanakagua kiwanda hicho kwa lengo la kufufua baada ya kuingia ubia wa kuzalisha sukari.PICHA/JUMA MTANDA.

Juma Mtanda, Morogoro.
Kampuni ya Mkulazi Holding Co imetenga mamilioni ya fedha ili kufufua kiwanda cha kusindika sukari cha Mbigili na kilimo cha zao la miwa ambapo mara baada ya kuanza uzalishaji wake wanatarajia kuzalisha tani 30,000 za sukari kwa kipindi cha mwaka.

Mpango huo umejili baada ya kampuni ya Mkulazi Holding Co kuingia ubia na jeshi la Magereza ili kukabiliana na changamoto ya upungufu za sukari nchini.

Kampuni hiyo imeanzishwa na wakurugenzi wakuu wa mifuko ya hifadhi ya jamii ya NSSF na mfuko wa pensheni wa PPF kwa lengo la kuwekeza katika sekta ya sukari.

Wakizungumza na waandishi katika Magereza ya Mbigili wilayani Mvomero, mkoani hapa jana, Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza, Dk Juma Malewa alisema kuwa jeshi la Magereza na wakuu wa mifuko ya hifadhi ya jamii wa NSSF na PPF wameingia ubia wa kufufua kiwanda cha kusindika sukari cha Mbigili na kuzalisha zao la miwa.

Dk Malewa alisema kuwa magereza tayari umeridhia kutoa hekali 17,5000 za ardhi kwa ajili ya kulima kilimo cha zao la miwa na kufufua kiwanda cha kusindika sukari cha Mbigili na kuwa kwa sasa wapo katika mchakato wa kuangalia miundombinu yote.

“Kiwanda cha kusindika sukari cha Magereza Mbigili kilikufa tangu mwaka 1996 kutokana na changamoto mbalimbali lakini kwa sasa Magereza tumeingia ubia na wakurugenzi wakuu wa mifuko ya hifadhi ya jamii ya NSSF na PPF kupitia kampuni yao ya Mkulazi Holding Co.”alisema Dk Malewa.

Dk Malewa alisema kuwa Rais Magufuli alisisitiza kuwa taasisi za serikali ziingie kwenye uchumi wa viwanda kwa kuingia ubia na taasisi zake na wao (Magareza) wameitikia wito huo kwa kujiingiza katika uzalishaji wa zao la miwa ili kuzalisha sukari na kampuni hiyo.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa mfuko wa hifadhi ya jamii wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara alieleza kuwa mpango huo utakapokamilia wanatarajia kuvuna tani 500,000 za miwa na kuzalisha tani 30,000 za sukari kwa mwaka.

Profesa Kahyarara alieleza kuwa wamevutiwa kuingiwa ubia na Magereza katika kilimo cha zao la miwa baada ya kuona mazingira mazuri ya uwekezaji wa kilimo hicho lakini miundombinu ya kiwanda na shamba yapo vizuri kiujumla wake.

“Tumevutiwa na mambo mengi katika kukubali kwetu kuwekeza katika mradi huu, shamba lipo kwenye bonde zuri linaloweza kufikiwa na maji kutoka mtoni kirahisi hata umwagilia pia unafaa.”alisema Profesa Kahyarara.

Profesa Kahyarara alisema kuwa uwepo wa mradi huo ni fursa kwa wakulima wanaozunguka bonde la Mbigili kuingia kwenye kilimo cha zao la miwa na baadaye miwa hiyo kuuza kiwandani kwani kiwanda kitahitaji malighafi nyingi.

Naye Mkurugenzi wa mfuko wa hifadhi ya jamii wa pensheni (PPF), William Erio alisema kuwa utekelezaji wa sera ya viwanda unafanyika kama serikali ya awamu ya tano inavyosisitiza kwa taasisi zake kuingia kwenye uchumi wa viwanda.

Erio alisema kuwa mifuko ya hifadhi ya jamii ina kazi nne ikiwemo kuandikisha wanachamaa, kukusanya michango ya wanachama, kulipa mafao ya wastaafu na kuwekeza na hiyo inatokana na sera ya uanzishwaji wa mifuko ya jamii.

“Baada ya kuingia ubia na magereza mifuko ya hifadhi ya jamii NSSF na mfuko wa pensheni wa PPF itanufaika kwa kupata wanachama wapya lakini mradi huo utatoa ajira za kudumu na zile za muda mfupi kwa hiyo uwekezaji huu utakuwa na faida kwa taifa.”alisema Erio.

Aliongeza kwa kusema kuwa uwekezaji huo utakuwa na manufaa makubwa kwa taifa kwani, taifa litakuwa linaokoa kutumia fedha za kigeni kuagiza sukari nje ya nchi kutokana na kuwepo kwa kiwango kidogo cha sukari kinachozalishwa Tanzania kutokidhi mahitaji.

Erio alisema kuwa kwa sasa wapo katika hatua ya tathimini ya awali na tathimini akinifu na mipango inaendelea na kukamilika kwake kutafuatia ununuzi wa mashine mpya na kufungwa kiwandani ambapo kazi za kuandaa shamba itakuwa ikiendelea na kupata mbegu.

Share on Google Plus

About Juma Mtanda

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
Post a Comment