BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

SERIKALI YARUHUSU KUSAMBAZWA KWA CHAKULA



Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba (kulia), akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kuhusu hali ya chakula nchini. PICHA: JOHN BADI
 

SERIKALI imeruhusu nafaka iliyohifadhiwa kwenye maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) iuzwe ili kukabiliana na mfumuko wa bei nchini.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alitoa tamko hilo wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, baada ya kuzindua safari za Shirika la Ndege la ATCL kati ya mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma.

Majaliwa alisema taarifa ambazo zimekuwa zinatolewa kuhusu hali ya chakula nchini si sahihi kwa kuwa serikali ndiyo yenye jukumu la kutoa taarifa ya hali halisi na si vinginevyo.

Hata hivyo, Waziri Mkuu alikiri kupanda kwa bei ya baadhi ya mazao akieleza kuwa kumetokana na mahitaji ya chakula yaliyopo katika nchi za jirani ambazo zinategemea kupata chakula kutoka nchini.

“Nataka kuwaondoa hofu Watanzania kwamba kelele zinazopigwa na watu mbalimbali kuhusu hali ya chakula nchini siyo sahihi, Serikali ndiyo inajukumu ya kutangaza hali ya chakula, iwe ni mbaya au nzuri,” alisema Majaliwa.

“Tunataka kuhakikishia Watanzania msimu uliopita wa kilimo tulivuna chakula kingi na tulikuwa na ziada ya tani milioni tatu na ilipofikia mwezi wa 10 (Oktoba) mwaka jana, Watanzania wakiwamo wabunge ni mashahidi, waliomba wafanyabiashara waruhusiwe kuuza mazao yao nje ya nchi kutokana na kuwa na mazao mengi na yalikuwa hayapati soko.

“Kupanda kwa bei (sasa) kunatokana na mahitaji yaliyopo nchi jirani za Kongo, Rwanda, Kenya, Somalia, Sudan. Hizi nchi zinategemea kupata chakula kutoka Tanzania."

Alisema nchi jirani zina uhitaji mkubwa wa chakula kutokana na serikali kuzuia wafanyabiashara kupeleka mazao nje ya nchi ili Tanzania iendelee kuwa na chakula cha kutosha hadi msimu ujao.

Alibainisha kuwa serikali ilitoa kibali cha kuuzwa kwa tani milioni 1.5 nje ya nchi na tani milioni 1.5 zilizosalia zilihifadhiwa na sasa imeruhusu ziuzwe nchini ili kupunguza gharama ya bei sokoni.

Waziri Mkuu alisema serikali inatamani kuona mkulima anauza mazao yake kwa bei nzuri na pia chakula kinapozalishwa kwa wingi na kinauzwa kwa bei ya chini.

Akizungumzia hali ya mvua, Majaliwa alisema kwa sasa imeanza kunyesha kwenye mikoa yote na kuwataka wananchi kutumia fursa hiyo kulima mazao ya muda mfupi na yanayostahimili ukame ili msimu ujao wavune mazao mengi.

“Hakikisheni mnalima mazao ya muda mfupi ili ifikapo Machi na Aprili muanze kuvuna na kupata chakula,” alisema Majaliwa na kueleza kuwa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi itatoa taarifa zaidi za hali ya chakula na mazingira ya mvua kwa msimu huu wa kilimo.

WATU WAMEFICHA
Katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tzeba, alisema hakuna uhaba wa nafaka nchini isipokuwa "watu wameficha chakula kusubiri bei ipande zaidi".

Alisema serikali kupitia vyombo vyake, imezunguka nchi nzima kufanya utafiti juu ya hali ya chakula na kubaini kuwapo kwa chakula kingi na cha kutosha majumbani, sokoni na kwenye maghala.

“Naendelea kusisitiza kwamba hakuna uhaba wa chakula nchini, kama Mkuu wa Nchi (Rais John Magufuli) alivyotangulia kusema.

Hali ya chakula na upatikanaji wa chakula inaonyesha bado ni ya kuridhisha na hasa upatikanaji wa mchele na maharage ikilinganishwa na mahindi,” alisema Dk. Tzeba.

“Kinachotokea hivi sasa ni kwamba bei za baadhi ya vyakula ndio zimepanda hususani mahindi, na bado kuna watu wameficha chakula ndani wanasubiri bei ipande zaidi. Wanatumia mwanya wa mwenendo wa mvua za vuli usioridhisha kupandisha bei hizo.

"Tunaomba watoe chakula hicho kabla serikali haijachukua hatua zozote kwa sababu vyombo vyetu vimefanya kazi na tunawafahamu.

“Tunao mfumo madhubuti wa kutathmini hali ya chakula nchini, eneo kwa eneo, mkoa kwa mkoa, wilaya kwa wilaya, hali ya hewa ya nchi hii haifanani nchi nzima na kwa hiyo uvunaji ama upatikanaji wa chakula miaka yote umekuwa na utofauti kutoka eneo moja kwenda eneo jingine.

"Na siyo kwamba mavuno kila mwaka yamekuwa yakifanana katika mikoa bila kujali mvua zimenyesha sana ama hazikunyesha."

Alisema mwaka jana walitangaza halmashauri 43 ambazo hazikuvuna chakula cha kutosha, lakini maeneo mengine hakukuwa na uhaba na kwamba nchi ilikuwa na akiba ya chakula kwa zaidi ya tani milioni tatu na utoshelevu wake ulikuwa asilimia 124.

Dk. Tzeba alisema hali hiyo iliyoonyesha utoshelevu wa chakula ilileta wasiwasi kwa wakulima kwamba huenda wasipate faida na hivyo kuiomba serikali kuwafungulia soko nje huku wakiungwa mkono na wabunge.

Sawa na maelezo yaliyotolewa awali na Waziri Mkuu mjini Dodoma, Dk. Tzeba alisema hadi Oktoba mwaka jana, tani milioni 1.5 za nafaka ziliruhusiwa kwenda nje na kwamba kuanzia mwezi huo hadi sasa Tanzania imeendelea kuwa na chakula cha kutosha.

“Mwaka jana msimu kama huu bei ya mahindi kwa gunia ilikuwa wastani wa Sh. 65,000, lakini wastani wa gunia hilo kwa sasa ni Sh. 85,000. Kwa hiyo, hili ndilo linalojitokeza la kupanda kwa bei, lakini bado chakula kipo na tumezunguka nchi nzima, tunazo taarifa za kuwapo kwa chakula cha kutosha,” alisema Dk. Tzeba.

Alisema wakati bei ya mahindi ikipanda, bei ya mchele imeendelea kushuka kutokana na akiba iliyopo sokoni kuwa kubwa.

“Sababu nyingine ya kupanda kwa bei ya mahindi imetokana na wakulima kulalamika kutaka wauze mazao yao kwa tija, mpaka sasa hatuna kesi kwenye soko hata moja nchini ambalo halina mahindi, mchele, maharage isipokuwa jambo la ukweli lililopo ni kwamba mvua ya vuli mwaka huu haikunyesha kwa kiwango kilichotarajiwa, lakini kutokunyesha kwa mvua hizo siyo sababu ya kuleta upungufu wa chakula," alisema.

Aliomba wananchi kutumia vizuri akiba ya chakula iliyopo badala ya kushawishika na kupanda kwa bei.

“Kwa sababu hali hiyo hailetwi na mtu ikifikia wakati ikatokea hali kama hiyo serikali itatangaza, lakini siyo kusukumwa na watu, tuna maelfu ya tani ya chakula watu wamefungia kwenye magodauni (maghala) wanasubiri bei ipande zaidi, tunaomba biashara ifanywe kwa mbinu halali na siyo kwa mbinu chafu.

Hali ya chakula Tanzania siyo hivyo kama watu wanavyolazimisha iwe," alisema.

Dk. Tzeba aliongeza kuwa utamaduni nao umekuwa tatizo katika baadhi ya maeneo; kwamba baadhi ya tamaduni zinashindwa kutumia aina fulani ya chakula kutokana na mazoea.

“Utamaduni nao usiwe tatizo, nasemea mfano niliouona Karagwe. Nilifika kwa mwananchi mmoja, tena mke wa diwani, ananililia anasema njaa kwamba hawakuvuna, lakini nilivyogeuka nikaona kihenge kina kama magunia 10. 


Nilipomuuliza akasema watoto wake wanashindwa kula (nafaka) kwa sababu wamezoea ndizi, sasa huyu ana njaa kweli?" Alihoji. 

Alisema serikali inapofanya utafiti wake, hufanya kwa ujumla kwa kuangalia upatikanaji wa nafaka kwa ujumla na si vinginevyo.
Alisema wananchi wanaoshindwa kununua mahindi, wanunue mchele ambao una bei nafuu.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: