BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

Millionaire  Ads

ULINZI MKALI UCHAGUZI WA MBUNGE

 
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewataka wananchi wanaoishi katika kata 19, zitakazofanya uchaguzi mdogo wa madiwani kwa upande Tanzania Bara na ubunge katika Jimbo la Dimani Zanzibar leo, wajitokeze kwa wingi kupiga kura kuwachagua viongozi watakaowaongoza kwa kipindi cha miaka mitatu.

Akizungumza na vyombo vya habari mjini Zanzibar jana, Mwenyekiti wa NEC Jaji Semistocles Kaijage alisema kuwa maandalizi ya uchaguzi huo, yamekamilika.

Kwamba wananchi wenye sifa za kupiga kura katika uchaguzi huo, wajitokeze kutimiza wajibu wao wa kikatiba.

Kaijage aliwapongeza wananchi wanaoishi katika Jimbo la Dimani, na wale wa Kata 19 za Tanzania Bara, zitakazofanya uchaguzi mdogo leo kwa utulivu, waliouonesha wakati wa kipindi cha kampeni za uchaguzi huo.

Alieleza kuwa licha ya kuwepo kwa dosari za hapa na pale zilizojitokeza, zikiwemo za ukiukwaji wa maadili ya uchaguzi kwa baadhi ya vyama na wagombea wao, NEC ilichukua hatua za kukemea vitendo hivyo ili kuwezesha kampeni za uchaguzi kufanyika kwa usalama na amani.

“Licha ya kwamba kutakuwa na ulinzi wa kutosha katika vituo vya kupigia kura, ni matumaini ya Tume kuwa hali ya amani na utulivu ambayo imekuwepo hadi sasa na kama ilivyokuwa katika chaguzi zilizopita itaendelea kudumishwa ili kuhakikisha uchaguzi huu unafanyika kwa utulivu, amani na ustawi wa Taifa letu,” alisema Jaji Kaijage.

Alieleza kuwa katika uchaguzi huo, jumla ya wapiga kura 9,280 wa Jimbo la Dimani Zanzibar wanatarajiwa kupiga kura ili kumchagua mbunge, atakayewaongoza kwa kipindi cha miaka mitatu kupitia vituo 29 vya kupigia kura katika Jimbo hilo.

Kwa upande wa uchaguzi mdogo wa madiwani katika Kata 20 za Tanzania Bara, wapiga Kura 134,705 walioandikishw,a wanatarajia kupiga kura katika vituo 359 ambavyo vilitumika katika Uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

“Naomba nitumie fursa hii kutoa rai kwa wananchi waliojiandikisha wajitokeze kwenye vituo vilivyotumika wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ili waweze kupiga kura kuwachagua viongozi mnaowataka bila hofu, woga, wasiwasi au ushawishi,” alisisitiza.

Kuhusu mchakato mzima upigaji wa kura ikiwemo taratibu za kuzingatiwa na wananchi kwenye vituo vya kupigia kura, uhesabuji wa kura, ujumlishaji wa kura na utangazaji wa matokeo, alisema kuwa hatua zote zitafanywa na wasimamizi wa uchaguzi kwa kuzingatia sheria.

Alisema vituo vyote vitafunguliwa saa moja asubuhi na kufungwa saa 10 jioni na kufafanua kuwa iwapo wakati wa kufunga kituo, watakuwepo wapiga kura katika mstari ambao wamefika kabla ya saa 10 jioni na hawajapiga, wataruhusiwa kupiga kura. Jaji Kaijage alisisitiza kwamba mtu yeyote, hataruhusiwa kujiunga katika mstari wa wapiga kura baada ya saa 10 jioni, muda ulioainishwa kisheria.

Alieleza kuwa kwa kila mpiga kura katika jimbo hilo, akumbuke kubeba kadi yake ya mpiga kura kwa kuwa Sheria ya Uchaguzi, inaelekeza kuwa ili mpiga kura aruhusiwe ni lazima awe na kadi ya mpiga kura.

Alisema kuwa ni marufuku na ni kosa la jinai, kumkataza mtu kwenda kupiga kura akisisitiza kwamba siku hiyo ya kupiga kura, kipaumbele kitatolewa kwa wagonjwa, watu wenye ulemavu, wanawake wajawazito au wenye watoto wachanga na wazee ambao hawatatakiwa kupanga mstari.

Jaji Kaijage alifafanua kuwa wakati wote wa kupiga kura na kuhesabu kura, mawakala wa vyama vya siasa watakuwepo kwenye vituo kwa kuwa wajibu wao ni kulinda maslahi ya vyama vyao vya siasa na wagombea wao.

Hata hivyo ,alisema hawatakiwi kuingilia masuala ya utendaji ambayo yamekabidhiwa kwa msimamizi wa kituo.

Alisema mawakala hao wataruhusiwa kuwepo vituoni kwa mujibu wa sheria na kanuni na kusisitiza kwamba wakala asiyekuwa na barua ya utambulisho kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi na ambaye hatakula kiapo cha kutunza siri, hataruhusiwa kuingia katika kituo cha kupigia, kuhesabia na kujumlishia kura.

Uhesabuji wa kura Katika hatua nyingine, Jaji Kaijage amebainisha kuwa kura zilizopigwa zitahesabiwa katika Kituo cha Kupigia Kura, mara tu upigaji kura utakapokamilika.

Wakati huo huo, Is-haka Omar, Zanzibar anaripoti kutoka Zanzibar kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk.Ali Mohamed Shein amesema anakishangaa chama cha CUF, kususia Uchaguzi wa Marudio mwaka juzi na kuingia kwa mbwembwe katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Dimani.

Alisema kitendo hicho kinadhihirisha wazi kufilisika kisiasa kwa chama hicho. Alitoa kauli hiyo alipohutubia mamia ya wafuasi wa CCM na wananchi wa Jimbo la Dimani wakati akifunga kampeni za chama hicho katika skuli ya Fuoni Unguha, jana.

Alisema kitendo cha CUF kuingia katika uchaguzi wa jimbo la Dimani, huku awali walisusia uchaguzi wa kitaifa, ni sawa na kuwadharau wafuasi wao, kuwa hawana maamuzi wala thamani ndani ya chama hicho.

“ Viongozi wa CUF ni vigeugeu, walisusia kuingia katika uchaguzi wa marudio kwa vitimbwi na mbwembwe za kila aina, leo wanaingia katika uchaguzi wa jimbo, sasa tuwaeleweje, ni sawa na mtu kusema hali nyama ya ng’ombe lakini mchuzi anakunywa, ndivyo ilivyo CUF.”alisema Dk.Shein .

Aidha aliwataka wakazi wa jimbo la Dimani, kumchagua mgombea wa CCM, Juma Ali Juma ili awe mbunge wa chama hicho kwa kuwaletea maendeleo endelevu wananchi hao.

Kuhusu mikakati ya Serikali katika kupunguza changamoto zinazowakabili wananchi wa wilaya ya Magharibi hasa jimbo la Dimani, Dk Shein alisema kuna mradi mkubwa wa maji, utakaoanza utakaosambaza maji katika wilaya hiyo. Kwa upande wa sekta ya elimu.

Akimnadi mgombea huo wa CCM, Dk Shein alisema Juma Ali Juma ni mgombea aliyechaguliwa kwa kufuata demokrasia ndani ya chama hicho na kujiridhisha kuwa anafaa kuwa kiongozi wa kuwatumikia wananchi.

Alisema mgombea huyo ni mchapakazi wa hali ya juu, hivyo anafaa kupewa ridhaa ya kubeba matumaini ya jimbo hilo hadi 2020.
Share on Google Plus

About Juma Mtanda

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
Post a Comment
Millionaire  Ads