BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

VILIO KUFUNGWA KWA MGODI MKUBWA WA MADINI TANZANIA


WATAALAMU wa uchumi wamebainisha maeneo manne yatakayoathirika kutokana na kufungwa kwa mgodi wa madini ya dhahabu wa Buzwagi uliopo Kahama mkoani Shinyanga.

Mgodi huo ambao ni mkubwa zaidi nchini, unatarajiwa kufungwa Desemba mwaka huu baada ya kubainika kuwa madini yameisha.



Kufungwa kwa mgodi huo ifikapo mwishoni mwa mwaka kulibainika juzi wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ilipowasili mgodini hapo na kuomba kupewa taarifa rasmi na wamiliki wake, Kampuni ya Acacia.

Meneja wa mgodi huo, Asa Mwaipopo, alisema wanatarajia kuufunga Desemba kutokana na kufikia hatua ya tatu ya uchimbaji ambayo imeonyesha 'mali' imekwisha lakini akabainisha kuwa wanaangalia uwezekano wa kuongeza eneo la uchimbaji ili waingie hatua ya nne ya uchimbaji (Cuts 4).

Alisema kufanikiwa kuingia hatua ya nne, kutaupa uhai mgodi huo kwa miaka mitatu hadi minne na kushindikana kuingia hatua hiyo kutamaanisha mwisho wa uchimbaji na watakachofanya ni kurudia kusaga mawe ya madini kwa miaka miwili iliyobaki katika mkataba wao na serikali kisha kuufunga rasmi.

700 KUKOSA AJIRA RASMI
Mwaipopo alisema mwaka 2012, mgodi huo ulikuwa na wafanyakazi 1,084 lakini mwaka jana wakapunguzwa 362, hivyo kwa sasa wana waajiriwa rasmi 722.

Kati ya waajiriwa hao 722, meneja huyo alisema 715 ni wazawa wakati wafanyakazi wa kigeni wako saba na kwamba idadi ya wafanyakazi imepunguzwa kutokana na kushuka kwa uzalishaji.

Hata hivyo, Mwaipopo aliiambia kamati hiyo kuwa hawajawaambia chochote wafanyakazi wao kuhusu kufungwa kwa mgodi huo wakihofia kushusha morali ya kazi na kuwakatisha tamaa, na pia kwa kuwa wanasuburi maombi ya mpango wao wa kuingia katika hatua ya nne ya kuongeza eneo la uchimbaji.

VILIO VINNE
Wakati kamati hiyo ikitaka kuelezwa jinsi Tanzania ilivyonufaika na mgodi huo na kuelezwa na meneja huyo kuwa kuna vituo vya afya, shule, maabara na barabara zimejengwa kupitia mapato ya Mgodi wa Buzwagi pamoja kufadhiliwa kwa timu za michezo mkoani Shinyanga, mtaalamu wa uchumi, Dk. Joel Silas, ameeleza athari zitakazotokana na kufungwa kwa mgodi huo.

Mhadhiri huyo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), katika mahojiano na Nipashe jana, alisema matokeo ya kufungwa kwa mgodi huo ni "kwa kiasi fulani kupungua kwa mchango wa sekta ya madini kwenye GDP (Pato la Taifa)".

Athari ya pili, Dk. Silas alisema ni maelfu ya Watanzania kupoteza ajira kwa kuwa wapo wengi walioajiriwa kwenye mgodi huo na wengine ambao wamejiajiri kwa kutoa huduma mbalimbali kwa wafanyakazi na vibarua wa mgodi huo.

"Kufungwa kwa mgodi huo pia kutaathiri kiasi kidogo cha mapato ya serikali. Shughuli nyingine za kiuchumi kuzunguka maeneo ya mgodi pia zitaathirika kama vile biashara,” alisema.

Dk. Silas aliitaja athari nyingine kuwa ni ya mazingira, akisema: "Kwa kawaida, kunakuwa na mkataba wenye kipengele cha kuyakarabati mazingira ya mgodi wanapomaliza shughuli za uchimbaji.

"Nafikiri kwa upande huo, watatekeleza hilo na mazingira kwa kiasi kikubwa yatalindwa. Wasipofanya hivyo, uharibifu wa mazingira utakuwa mkubwa."

MIKATABA MIBOVU
Mchumi huyo aliwashauri viongozi kuwa makini wanapoingia mikataba mipya ya madini kwa kutoa kipaumbele kwa masuala yanayohusu maslahi kwa nchi ili iweze kunufaika na rasilimali zake.

"(Kwa njia hiyo) hata wanapomaliza kuchimba, tunakuwa tumepata manufaa makubwa. Vile vile tujaribu kuangalia uwezekano wa serikali kuwa mbia kwenye uchimbaji, yaani serikali iwe inakuwa na hisa. Hii itasaidia kupata mapato makubwa," alifafanua zaidi Dk. Silas.

Mgodi wa Buzwagi ni miongoni mwa migodi mitatu ya dhahabu Kanda ya Ziwa inayomilikiwa na Kampuni ya Acacia. Mingine ni Bulyang'ulu uliopo Kahama pamoja na North Mara uliopo Nyamongo mkoani Mara.

Mgodi wa Buzwagi uligunduliwa mwaka 1950 lakini uchimbaji na upatikanaji wa dhahabu ulianza mwaka 2009 na ulitarajiwa kufungwa mwaka 2019.

Mwaka 2009 wakati mgodi huo unafunguliwa kwa uwekezaji wa Dola za Marekani milioni 400 (sawa na Sh. bilioni 888 kwa bei ya dola ya jana), ulitarajiwa kuajiri wafanyakazi zaidi ya 3,000. Hadi mwishoni mwa mwaka huo, kulikuwa na wafanyakazi takribani 1,500 mgodini hapo, hata hivyo. 


Mwaka uliofuata, yaani 2010, wafanyakazi 60 walifukuzwa baada ya Kampuni ya Acacia (kipindi hicho ikiitwa Barrick) kubaini kuwapo kwa wizi wa nishati mgodini hapo.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: