BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KWANI VIP UHAI WA BEN SAANANE UMEKUWA NA UTATA BAADA YA KUTEKWA ?.


UTATA umeibuka juu ya uhai wa kada wa Chadema, Ben Saanane, baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kusema ‘familia ya mtajwa (Ben Saanane) aliyetangulia mbele za haki au vinginevyo’, uchunguzi wa suala lake utakapokamilika, taarifa rasmi itatolewa.

Wakati Majaliwa akisema hayo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, alisema watu waliokuwa wanafanya kazi na Saanane, na familia yake, inabidi waangaliwe ni lini walitoa taarifa polisi baada ya tukio kutokea na kama wametoa picha yake kwenye vyombo vya habari ili jamii isaidie kumtafuta.

Suala la Saanane, liliibuka wakati wa maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu, baada ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, kuhoji kwanini Serikali isishirikiane na vyombo vya nje ambavyo vina uwezo mkubwa wa kiteknolojia katika kutafuta mtu aliyepotea.

Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema, alisema Serikali imekuwa kimya kiasi ambacho inatia shaka na hivyo iko haja ikaomba msaada kutoka mataifa mengine kama ilivyofanyika nchini Kenya baada ya kifo cha mwanasiasa, Robert Ouki.

“Taifa limekumbwa na mambo kadhaa, ikiwamo hofu ya kikatiba, hofu ya kuishi na hofu ya kupata habari na kutoa habari. Hii inachagizwa kwa kiasi kikubwa na wabunge kukosa uhuru hata wa kuchangia ikiwemo kuzuia Bunge ‘live’. Jambo hilo limetawala katika mijadala na vyombo mbalimbali vya habari.

“Kupotea kwa msaidizi wangu Ben Saanane, jambo hili linazua hofu kwa familia na jamii na kwa kuwa ni utamaduni kwa nchi kushirikiana na mataifa mbalimbali na mataifa tofauti katika kufanya utafiti na uchunguzi.

“Uingereza wametumika maeneo mbalimbali pale inapohitajika kufanya uchunguzi kama ilivyofanyika Kenya kwa Robert Ouki, Serikali kama imeshindwa kuchunguza.

“Kutokana na mazingira hayo, kwanini Serikali isitoe kauli kwa sababu miezi sita ni mingi, kwanini isishirikiane na wenzetu ambao wana teknolojia ya ziada?” alihoji Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai.

WAZIRI MKUU
Akijibu swali hilo, Majaliwa alisema Serikali iko kazini wakati wote, ikiwamo kumtafuta Saanane ili kupata ukweli na kwamba majibu yakipatikana watawaambia Watanzania.

“Baada ya familia kutoa taarifa na haya yote, Serikali lazima mtuamini kwamba tunayo jinsi ya kuweza kuchunguza na kubaini, labda niseme haina kikomo cha uchunguzi kutegemea na ‘nature’ (asili) ya tatizo lenyewe.

“Familia ya mtajwa aliyetangulia mbele za haki au vinginevyo, sina hakika, uchunguzi utakapokamilika tutaeleza,” alisema.

Kuhusu muda wa uchunguzi huo, alisema: “Muda inategemea vyombo vyetu vinapata msaada na jamii na teknolojia tunayoitumia, bado kauli ya kuwaomba wawe watulivu na jambo hili ni letu na Watanzania watupe ushirikiano.”

Alisema Serikali haiwezi kutangaza mipango yake yote hadharani jinsi inavyoshughulika na masuala hayo na kuhusu vyombo vyake vinavyofanya kazi na mahali au hatua wanazofikia, kwani kwa kufanya hivyo wataharibu utendaji kazi wake.

Majaliwa aliwataka Watanzania kuwa watulivu kwa kuwa vikosi vya Serikali vinaendelea kufanya kazi yake na akaomba kila anayejua jambo lolote kuhusu mambo mbalimbali yaliyolalamikiwa na wabunge watoe ushirikiano.

“Hata Waziri wa Mambo ya Ndani (Mwigulu Nchemba), alizungumza kuwa Watanzania watupe muda vyombo vyetu vinafanya kazi ili tuweze kuchunguza kwanini vinatokea, kwanini Watanzania wanakuwa na hofu na haya, hatuwezi kutoa hadharani na kueleza vyombo vinavyofanya kazi,” alisema.

Alikiri Tanzania ina mahusiano na mataifa mengine katika kufuatilia vitendo vya aina hiyo, lakini akasema kwa sasa ni mapema kuomba msaada kuhusu Ben Saanane, kwani bado wana imani kuwa watapata ukweli kupitia vikosi vya ndani ya nchi.

MWANASHERIA MKUU
Akizungumza wakati mawaziri wakianza kujibu hoja za wabunge walizotoa, wakati wa kuchangia hotuba ya Wizara ya Tamisemi na ya Utawala Bora, AG Masaju, alisema: “Mimi naomba kushauri polisi waendelee kushirikiana na watu walio karibu sana na huyu mtu anayedaiwa kupotea (Saanane), waisaidie polisi ili tupate ukweli.

“Kwanza familia yake, watu ambao amekuwa akifanya nao kazi kwa karibu tutoe ushirikiano kama ambavyo wabunge wameshauri kwenye suala hili, hatuwezi kuwa na ‘double standard’.

“Kwa mujibu wa Katiba ibara ya 26, kila mmoja anawajibika kutii Katiba na sheria za nchi, mheshimiwa Mbowe ametusaidia katika hotuba yake, hakuna mtu aliye juu ya sheria.

“Moja watatueleza tangu huyu mtu anayedaiwa kupotea au kufariki, ilichukua muda gani kutoa taarifa, halafu familia na watu waliokuwa karibu na huyu mtu na hii familia wameshapeleka katika vyombo vya habari kwamba huyu mtu amepotea ili watu wote au mtu yeyote aliyeko kwenye ‘public’ (jamii) atusaidie halafu ‘will take action accordingly’.

“Mimi ndiyo nilivyojua polisi walikuwa wanafanya kazi, siku hizi wanafanyaje kazi?

“Sasa hivi tungekuwa na watu wanaisaidia polisi kwa karibu mno sasa, ‘how we can handily this matter so much successfully’, watu waliokuwa wanafanya naye kazi na watu wa karibu na familia yake watoe taarifa vyombo vyetu vifanyie kazi kwa karibu mno,” alisema Masaju.

Awali Waziri Mkuu, akizungumzia Bunge ‘Live’, ambalo pia aliulizwa na Mbowe, alisema hawezi kurudi kuzungumzia jambo hilo kwa kuwa walishalizungumza na kufikia mwafaka na ipo namna bora ya kuwafikishia wananchi matangazo ya Bunge na kwamba hawajaona malalamiko au upungufu.

FAMILIA
Katika hatua nyingine, familia ya Saanane imesema Jeshi la Polisi limekuwa na kigugumizi kutoa taarifa rasmi za mawasiliano ya mwisho ya simu aliyoyafanya Saanane kabla ya kupotea.

Pia familia hiyo, imedai licha ya Serikali kuwataka kuwasilisha maombi mapya ya kumtafuta mtoto wao, tayari yalishatolewa na familia na kuchapishwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari.

Akizungumza na MTANZANIA jana, baba mzazi wa Saanane, Focus Saanane, alisema amepata taarifa za kuwa Serikali imewataka kuwasilisha maombi mapya ya kutafutwa upya mtoto wake, jambo ambalo limekuwa likiwachanganya.

“Tunachanganyikiwa kabisa, huku Jeshi la Polisi linasema linaendelea na uchunguzi juu ya kutepotea kwa Ben, leo tunaambiwa tuwasilishe maombi ya kuanza mchakato mpya wa kumtafuta, sasa hapa lipi ni lipi?” alihoji mzee huyo.

Alisema familia hiyo, haina ombi jipya kwa Serikali zaidi ya maombi ya awali ambayo tayari familia ilikwishayatoa kupitia vyombo vya habari mbalimbali na kuiomba pamoja na mwajiri wake (Chadema) kuongeza nguvu za kumtafuta mtoto wake.

“Familia hatuna uwezo mwingine, eti tuwaandikie barua tena, hatuwezi kufanya hivyo, tulishaomba mara nyingi serikalini pamoja na mwajiri wake watusaidie kumtafuta, sijui wanataka tuongee kwa lugha gani zaidi ya hii,” alisema.

Alisema familia imekuwa ikijitahidi kufuatilia kwa karibu mchakato unaofanywa na Jeshi la Polisi, lakini jambo la kusikitisha wamekuwa wakiambiwa uchunguzi unaendelea.

“Tumekuwa tukifuatilia suala hili polisi mara kwa mara, wanatwambia uchunguzi unaendelea, hata tulipotaka watupatie taarifa za mawasiliano yake aliyoyafanya mara ya mwisho kabla ya kupotea, walitupiga chenga, tumebaki hewani hatujui tufanyaje,” alisema.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: