BannerFans.com

SUZAN KIWANGA, LIJUALIKALI WAONJA JOTO YA JIWE MAHAKAMANI MOROGORO

Millionaire  Ads

MBUNGE WA KILOMBERO ATIKISA IFAKARA NA VIJIJI VYA KANDO YA BARABARA KUU MIKUMI-IFAKARA BAADA YA KUTOKA MAGEREZA UKONGA.

Mbunge wa jimbo la Kilombero, Peter Ambrose Lijualikali akihutubia maelfu ya wananchi wa mji wa Ifakara wakati wa mkutano wake wa kwanza wa hadhara uwanja wa shule ya msingi Jongo baada ya mahakamau kuu kanda ya Dar es Salaam kumwachia huru kufuatia mahakama ya hakimu mkazi wilaya ya Kilombero kumfunga kifungo cha miezi sita jela./JUMA MTANDA.

Juma Mtanda, Morogoro.
January 11 mwaka huu, mbunge wa jimbo la Kilombero, Peter Lijualikali alihukumiwa kwenda jela miezi sita baada ya mahakama ya hakimu mkazi wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro kumtia hatiani kwa kosa la kufanya vurugu wakati wa uchaguzi wa Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo mjini Ifakara ukiendelea.


Kutokana na kosa hilo, Lijualikali alijikuta akishitakiwa kwa kosa la kuwashambulia polisi waliokuwa wanalinda amani eneo hilo kufuatia kitendo cha kumzuia mbunge huyo kuingia kwenye ukumbini kwa madai ya kutokuwa mjumbe halali wa vikao vya baraza la madiwani.

Hali hiyo imemfanya mwakilishi huyu wa jimbo la Kilombero katika vikao vya bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania kukaa ndani ya gereza siku 79 kabla ya kuachiwa huru Marchi 30 mwaka huu na mahakama kuu kanda ya Dar es salaam iliyotengua hukumu yake na kuwa huru.

April 8 mwaka huu, majira ya mchana msafara uliomsindikiza mbunge Peter Lijualikali ukiongoza na Katibu wa kanda ya kati, Iddi Kizota ulianza safari mjini Morogoro kuelekea mji wa Ifakara ambako ni makao mkuu ya jimbo la Kilombero kufanya mikutano miwili mikubwa na kuonekana baada ya siku 88 kupita kufuatia mkasa huo.
 
Hapa wananchi wakisukuma gari la mbunge huyo kijiji cha Kiberege/JUMA MTANDA.

 
WANANCHI WASHIKWA NA BUTWAA.
Sehemu kubwa ya wananchi walishikwa na butwaa baada ya kuona sura ya mbunge huyo akiwapungia mkono wakati msafara wake ukipita kuelekea Ifaraka kwa wananchi waliojitokeza kando ya barabara na wengine waliozuia msafara kwa kutanda barabarani wakitaka ashuke ndani ya gari ili awasalimu.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara katika uwanja wa shule ya msingi Jongo kata ya Viwanja sitini, mbunge wa jimbo la Kilombero, Peter Ambrose Lijualikali aliwaeleza umati wa wananchi waliojitokeza kumpokea baada ya kupotezana nao kwa siku 88 kutokana na mkasa uliompata sasa amerejea uraiani.

Lijualikali alieleza kuwa sababu ya yeye kuhukumiwa kifungo cha jela miezi sita gerezani hakikutokana na kufanya fujo kama ilivyotafsiriwa na vyombo vya dola kupitia mahakama isipokuwa ni uonevu uliotokana na hila zisizo na msingi za kumzuia kuingia kwenye kikao cha baraza la madiwani halmashauri ya Kilombero na kumnyima haki ya kumchagua mwenyekiti wa halmashauri hiyo.
Wananchi wakifurahia jambo wakati mbunge huyo akihutubia katika mkutano wa hadhara/JUMA MTANDA.

“Mimi ni mbunge wa jimbo la Kilombero na napaswa kuingia kwenye vikao vya baraza la madiwani halmashauri yetu lakini pia mimi ni diwani wa kata ya Ifakara na kutokana na sifa hizo sipaswi kuzuiliwa na chombo chochote kushiriki vikao vyote.”alisema Lijualikali.

Akisimulia maisha ya jela, Lijualikali aliwaeleza wananchi hao kuwa maisha ya jela ni magumu na ugumu wake unatokana na amri zinazosimamiwa na askari magereza yakiambatana na mateso pindi wanapoona inafaa kutolewa adhabu.

“Magereza sio mahapa salama lakini mtu mwenye hadhi kama mbunge anawekwa selo na wahalifu wengine kama wahalifu wa ujambazi hii ni hatari kwa usalama wa watu wenye hadhi kama mbunge labda nimefanyiwa mimi kwa sababu natoka upinzani hilo sijui.”alisema Lijualikali.

Mbunge huyo ambaye amekumbana na visa vya kila aina na shuruti kutoka ndani ya vyombo vya dola amedai kuwa, askari magereza wamekuwa watu wasiopenda kusikiliza shida ama matatizo ya mfungwa pindi anapojisikia kuwa na afya dhoofu lakini hata wakipata udhibitisho wa daktari bado wataupinga na utapewa kazi.

Aliongeza kwa kueleza kuwa mtu yoyote anayefungwa gerezani kwa kufanya kosa ama kubambikiwa, jamii isiwatenge maana watu hao wanahitaji faraja kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki maana kukaa siku moja jela sio jambo rahisi.

VITA YA DAWA ZA KULEVYA GEREZANI.
Lijualikali alieleza kuwa ameshsngazwa kuona vita ya kupambana na madawa ya kulevya kuwa sasa rais, Dk John Pombe Magufuli amulike na kwenye magereza kwani huko madawa ya kulevya yanauzwa kama njugu ndani ya gereza licha ya kuwa na ulinzi mkali.

“Unaweza kujiuliza watu waliofungwa ndani ya magereza wanawezaje kupata madawa ya kulevya na kuyatumia wakiwa wapo chini ya ulinzi mkali?....mimi nipo tayari kutoa ushirikiano mkubwa kwa chombo chochote kwenda gereza la Ukonga kuwafichua wote wanaojihusisha na madawa ya kulevya.”alisema Lijualikali.

Mtu yoyote anayefikiria kukupeleka jela kwa njia ya namna yoyote huyo sio mtu mzuri kwako, huyo ni adui yako mkubwa kwa maisha yako kwani jela sio kuzuri, kuna mateso na ukisikia filimbi inalia chanza kwanza unatakiwa mfungwa ulale haijalishi iwe asubuhi, mchana.

“Ukiwa jela mtu unajiona kama mnyama, siku moja nilikuwa naumwa na kumweleza (Mzee) askari leo naumwa nina malaria na nilienda kwa daktari na kupewa wiki moja ili nipumzike lakini askari hakunielewa na badala yake alinipa kazi ya kubeba matofari bila kujali cheti cha daktari.”alisema Lijualikali.

Askari magereza wana marungu yaliyoandika majina ya viongozi wengi wa dunia likimo la Putin, Trump, Magufuli mengine lakini kule Ukonga kipo chumba kilichopewa jina la “staki shari” na mfungwa akipelekwa huko basi atarejea selo akiwa anatambaa kutokana na mateso kwa wale waliokosa.

Lijualikali anaeleza kuwa mfungwa wa Tanzania hapewi haki zinazostahiki kama mfungwa mbaya zaidi mbunge anapaswa kukaa jela tena chumba maalumu cha daraja la kwanza na sio kukaa pamoja na mfungwa wengine wakiwemo wenye makosa ya uhalifu wa ujambazi.

MIRADI YA ILIYOKWAMA KUIFANYIA KAZI.
Akizungumzia juu ya kukwama kwa miradi iliyokuwa chini ya ofisi ya mbunge alisema kuwa miradi iliyokwama itamaliziwa ili kupunguza changamoto katika maeneo husika.alisema Lijualikali.

Lijualikali alisema kuwa katika vijiji vya Chicago, Mwaya, Siginali na Berege miradi yote iliyokwama kutokana na yeye kufungwa gerezani sasa ipo mbioni kupatiwa ufumbuzi.

“Nakumbuka vizuri miradi yote ya maendeleo iliyokwama jimboni kwetu wakati nipo gerezani likiwemo daraja la kijiji cha Chicago, daraja la mto Mwaya kijiji cha Mwaya itakamilika lakini nitafuatilia na miradi mingine ya baadhi ya wakazi wa vijiji kukosa huduma ya majisafi na salama.”alisema Lijualikali.

Aliongeza kwa kusema kuwa mambo mengi ya kimaendeleo yamelala lakini hilo haliwezi kukatisha tamaa wana Kilombero ambapo baada ya kumalizika kwa kazi ya madaraja kutakuwa na kazi ya ukarabati wa barabara za mitaa kutumia fedha zetu za mfuko wa jimbo.

Kwa upande wa viongozi wa vijiji vy Sululu na Siginali, mbunge huyo ameagiza uongozi huo wakishirikiana na Diwani wa kata ya Siginali, Shemajiji Ndama kwenda kwa Mkurugenzi wa halmashauri ya Kilombero kupata maelezo ya kina ya juu ya kukwama kwa mradi wa mji ya koki.

Akizungumzia mradi wa maji ya koki kushindwa kupokelewa, Mwenyekiti wa kijiji cha Siginali, Ramadhan Chuma alieleza kuwa kushindwa kupokelewa mradi huo kumetokana na kujitokeza kwa kasoro nyingi zilizojitokeza wakati wa matamio.

Chuma alieleza kuwa pampu ya maji ya mradi huo ipo kwenye chanzo cha maji kijiji cha Sululu na tanki la kusambazia maji kwa wakazi wa vijiji hivyo limejengwa kijiji cha Siginali.

“Mradi wa maji ya koki umegharimu kiasi cha sh400 mil na ulianza mwaka 2013 lakini mradi huo umeshindwa kupokelewa kutokana na kujengwa chini ya kiwango kwani baadhi ya maeneo mipira ipo nje ya ardhi lakini vituo vya maji maji mita hazizomi.”alisema Chuma.

Chuma aliongeza kwa kueleza kuwa sehemu ya mto limepitishwa bomba la plastiki badala ya bomba la chumba na mradi huo ulikuwa kwenye matazamio na Februari mwaka huu ulitarajiwa ukabidhiwa.

Mwenyekiti wa kijiji cha Chicago kata ya Kidatu, Prosper Komba alimweleza mbunge huyo kuwa kitendo cha kufungwa kwake gerezani kumechangia daraja la mto Chicago kushindwa kukamilika kwa wakati.

“Tumefuraha kukuona upo huru mbunge wetu na jambo lililopo mbele tu ni kukwama kwa daraja la mto Chicago ambapo mpaka sasa limetumia kiasi cha sh10 Mil na tunakuomba uongeze kiasi cha sh9 Mil ili kumalizia ujenzi wa daraja hili na liweze kutumika ambapo kwa sasa limebakia hatua ya kufunika juu.alisema Komba.
Sehemu ya wananchi wa Ifakara wakifurahia jambo wakati mbunge wa jimbo la Kilombero, Peter Lijualikali (Hayupo Pichani) wakati akihutubia maelfu ya wananchi wa mji huo mkutano wa hadhara katika uwanja wa shule ya msingi Jongo Ifakara.

 KATIBU WA KANDA YA KATI CHADEMA AKERWA NA CCM KUFANYA SHEREHE KUFUNGWA KWA MBUNGE.
Katibu wa kanda ya kati chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema) Iddi Kizoto amekerwa na vitendo vya baadhi ya viongozi wa kisiasa kutoka CCM kufanya sherehe kwa kitendo cha makahama ya wilaya ya Kilombero kumhukumu kifungo cha miezi sita jela januari 11 mwaka huu.

Kizota alieleza hayo kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wananchi waliojitokeza kwenye mikutano ya hadhara ya mbungu Peter Lijualikali baada ya kutoka gerezani na kuwasalimia.

“Ni kitendo cha aibu na kisicho cha kiungwana pengine ni ufinyu wa kuona mbele, leo hii kiongozi mwenye akili timamu anafurahia mbunge wako kufungwa jela ?....kama tumefikia hatua hii ni hatari sana na viongozi wa namna hii hawapaswi kupewa tena uongozi.”alieleza Kizota.

Aliongeza kwa kueleza kuwa inapofanyika sherehe sehemu hiyo kuna furaha ya kutosha…..sasa inakuwaje mbunge wa jimbo anafungwa jela na suala hilo linageuka kuwa furaha ?.

Mtu anayefungwa jela anaweza kutazamwa kwa sura nyingi kama ni kweli alistahuhili adhabu kutokana na mahakama inavyoweza kutafsiri sheria maana wapo wanaofungwa kwa kusingiziwa lakini sidhani kama jambo hilo linaweza kumfanya viongozi aandaye sherehe.

Kizota alieleza kuwa kuna mambo mtu ama wananchi wanaweza kufurahia ndani ya vyama vya siasa kama mgombea kushindwa uchaguzi kuanzia ngazi ya urais, ubunge, udiwani na uchaguzi mwingine lakini kusherehekea kufungwa kwa kiongozi ambaye hana tuhuma kama za ufisadi, rushwa na nyingine hapo unafurahia nini ?alihoji Kizota.

KATIBU WA MBUNGE JIMBO LA KILOMBERO.
Msaidizi wa mbunge wa jimbo la Kilombero, Anthony Mwampunga ameeleza kuwa katika mikutano ya hadhara ya mbunge huyo ya kuongea na wananchi tangu atoke gerezani katika shule ya msingi Jongo Ifakara na shule ya msingi Mgudeni kijiji cha Mwaya, wananchi wameweza kumpa pole kwa kumchangia fedha kiasi cha sh620,000 na jogoo.

“Mbunge ameweza kuchangiwa fedha na wananchi kiasi cha sh620,000 kama sehemu ya kumpa pole katika mikutano ya Jongo na Mgudeni pamoja na zawadi ya jogoo na hii inaonyesha ni namna gani wananchi wanavyoonyesha upendo kwa Lijualikali.”alisema Mwapunga.

Mwampunga alisema kuwa upendo wa wananchi haukuweza kujificha kwa, Peter Ambrose Lijualikali baada ya kuonyesha mapokezi makubwa katika vijiji vilivyopo kando ya barabara kuu ya Mikumi-Ifakara na kwenye mikutano yake.

“Wapigakura wa jimbo la Ifakara hawajaweza kuonana na mbunge wao kwa siku 88 tangu afungwe gerezani hivyo kutengeneza shauku kubwa ya kila mtu atake kumuona na kumsikiliza anasema nini baada ya kutoka kwenye kifungo.”alisema Mwampunga.

BIBI ALIYETOA ZAWADI YA KUKU KWA MBUNGE ANENA.
Mkazi wa mtaa wa Kiyonjo katika mji wa Ifakara, Mwanaisha Lyandu (85) anaeleza kuwa, Peter Lijualikali kwake ni zaidi ya mbunge wa jimbo hilo la Kilombero.

Mwanaisha amefurahishwa na kitendo cha mahakama kuu kanda ya Dar es Salaam na kupongeza jopo la mawakili waliokuwa wanamsimamia mbunge Lijualikali na kutengua kifungo chake kuwa kwake ni ukombozi mkubwa na kuwatakia afya nje mbele za mwenyezi mungu wanasheria hao.

“Huyu Lijua (Lijualikali) huyu ni mjukuu wangu na kamwe siwezi kumsahau katika maisha yangu kwani ameweza kunijengea nyumba akiwa huko ndani ya gereza namshukuru sana na leo nampa zawadi ya jogoo.”alisema Mwanaisha ambaye alijawa na furaha.

“Nimejengewa nyumba ya vyumba viwili na huyu mbunge na kilichobaki sasa ni hatua ya kuezeka bati tu ili nihamia nyumba mpya lakini nimshukuru kijana wake (Msaidizi wa Mbunge) kusimamia kazi ya ujenzi wakati Lijualikali akiwa gerezani.”alisema Mwanaisha.

Peter Lijualikali amekuwa mbunge aliyekumbana na misukosuko ya kila aina inayompelekea kuswekwa rumande polisi na gereza la Idete kunatokana na madai ya misimamo yake ya kusimamia haki katika jamii.

Mwaka 2013 wananchi wa kata ya Ifakara walimchagua kuwa diwani wa katika uchaguzi mdogo baada ya kifo cha aliyekuwa diwani wa kata hiyo na Mwenyekiti wa baraza la halmashauri ya wilaya ya Kilombero marehemu, Ramadhan Kiombile.

Mbunge huyo machachali alizaliwa Juni 25 mwaka 1985 mkoani Kigoma na kusoma shule ya msingi Kulasini Dar es Salaam na kuhitimu elimu ya chuo kikuu cha Tumaini tawi la Dar es Salaam kozi ya Library and Information Studies kuanzia mwaka 2011.
Share on Google Plus

About Juma Mtanda

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
Post a Comment
Millionaire  Ads