BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

NYAMBIZI YA MAREKANI YAWASILI KOREA KUSINI

Nyambizi ya jeshi la Marekani imewasili katika pwani ya Korea Kusini huku wasiwasi ukiongezeka kuhusu uwezekano wa Korea Kaskazini kufanya jaribio jingine la kombora au silaha za nyuklia.

Meli hiyo kwa jina USS Michigan, ambayo ina uwezo wa kushambulia kwa makombora, inatarajiwa kujiunga na kundi jingine la meli za kivita zinazoelekea eneo hilo, zikiongozwa na meli kubwa ya kubeba ndege ya Carl Vinson.

Korea Kaskazini inaadhimisha miaka 85 tangu kuanzishwa kwa jeshi lake Jumanne.

Miaka ya nyuma, imekuwa ikiadhimisha siku hiyo kwa kuzindua makombora na silaha nyingine.

Wasiwasi umeongezeka wiki za karibuni kutokana na Marekani na Korea Kaskazini kujibizana vikali na kutoleana vitisho.

Hayo yakijiri, katika tukio ambalo si la kawaida, bunge lote la Seneti nchini Marekani limealikwa kwa kikao cha kupashwa habari kuhusu Korea Kaskazini siku ya Jumatano katika ikulu ya White House.

Nyambizi ya USS Michigan hutumia nguvu za nyuklia na hubeba makombora aina ya 154 Tomahawk na wanajeshi 60 pamoja na meli nyambizi nyingine ndogo, gazeti la Korea Kusini la Chosun Ilbo limeripoti.

Meli hiyo inatarajiwa kushiriki kwenye mazoezi ya kijeshi pamoja na kundi la meli zinazoongozwa na Carl Vinson, kundi ambalo lilitumwa eneo la Korea kuonyesha ubabe wa kijeshi wa Marekani. USS Carl Vinson ilishiriki mazoezi na majeshi ya Australia

Meli hizo za kivita wakati mmoja zilizua utata baada ya suitafahamu kuhusu iwapo zilikuwa hasa zinaenelekea eneo la Korea.

Lakini maafisa wa jeshi la wanamaji la Marekani kwa sasa wamesema zinaelekea eneo hilo kama ilivyoamrishwa.

USS Carl Vinson mwanzoni ilikamilisha mazoezi na jeshi la Australia na kisha kuondoka ikidhaniwa kwamba ilikuwa inaelekea pwani ya Korea.

Lakini meli hiyo na meli nyingine zilipita na kuelekea upande wa Bahari ya Hindi. Korea Kaskazini inaadhimisha miaka 85 tangu kuundwa kwa jeshi lake

Pyongyang ilikerwa sana na kutumwa kwa meli hiyo na imetishia kuizamisha kwa "shambulio moja kubwa" dhidi ya ilichosema ni uchokozi wa Marekani.

Rais wa Marekani Donald Trump alisema mapema mwezi huu kwenye mahojiano ya runinga kwamba angetuma "kundi kubwa la meli zenye nguvu" na kwamba Marekani ina nyambizi ambazo "zina nguvu zaidi, nguvu zaidi kabisa kushinda meli hiyo (Carl Vinson) ya kubeba ndege".

China imeendelea kuhimiza kuwepo kwa utulivu.

Rais Xi Jinping, akizungumza kwa simu na Bw Trump mnamo Jumanne, alizihimiza pande zote "kuvumiliana na kujiepusha na vitendo ambavyo vinaweza vikaongeza wasiwasi zaidi".
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: