BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

POLISI NA JWTZ WAINGIA KWENYE KUNDI LA WADAIWA SUGU KWA KAMPUNI YA SIMU YA TCCL


NI mtihani mzito! Hivyo ndivyo inavyoweza kuelezwa kuhusiana na mrundikano wa madeni yatokanayo na huduma ya mawasiliano unaozikabili taasisi kadhaa za Serikali zikiwamo Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Kwa sababu hiyo, uongozi wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) una kibarua kizito cha kuimarisha hali yake ya kifedha kwa kuhakikisha kuwa inakusanya madeni yake hayo yenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni tisa.

Mtihani huo wa aina yake kuhusiana na madeni ya mabilioni yatokanayo na huduma za mawasiliano umeibuliwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, huku ikitaja taasisi nyingine kadhaa za umma zinazodaiwa fedha nyingi kampuni hiyo.

Katika taarifa yake bungeni mjini Dodoma jana, kamati hiyo ilieleza kuwa TTCL inadai zaidi ya Sh. bilioni 9.804 kwa taasisi na mashirika ya Serikali ambayo yamelimbikiza madeni yao kwa muda mrefu.

Mbali na Polisi na JWTZ, kamati hiyo ilizitaja taasisi na mashirika mengine kuwa ni Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Idara ya Uhamiaji, Shirika la Reli Tanzania (TRL) na pia Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

Akisoma taarifa kuhusu utekelezaji wa bajeti ya wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa mwaka wa fedha 2016/17 pamoja na maoni ya kamati kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa mwaka wa fedha 2017/18, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk. Norman Sigalla, alisema namna bora ya kulinusuru shirika hilo ni wadaiwa hao kulipa kiasi hicho.

Alisema Kamati inaamini kuwa taasisi hizo zina bajeti kwa ajili ya kulipia huduma za mawasiliano na hivyo ni vyema kulipa ili kuleta tija katika utendaji wa TTCL.

“Kamati inasisitiza kuwa Serikali, mashirika na taasisi zake zilipe madeni ya TTCL kwani katika bajeti ya taasisi hizo kuna fedha ambazo huwa zinatengwa kwa ajili ya kulipia gharama za mawasiliano. Sasa iweje washindwe kulipia mpaka deni kuwa kubwa kiasi hiki?” Alhoji Dk. Sigalla.

Hivi karibuni, mtihani kama huo ulikuwapo pia kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linadai zaidi ya Sh. bilioni 270 kwa taasisi na mashirika mbalimbali ya umma.

Rais John Magufuli aliitaka Tanesco kukusanya madeni yake bila hofu yoyote na kukata umeme kwa taasisi au shirika litakaloshindwa kulipa madeni yake, ikiwamo ikulu ikibidi.

Baada ya hapo, mwitikio wa taasisi na mashirika mbalimbali ya Serikali kulipa madeni yao uliongezeka, ikiwamo JWTZ iliyolipa sehemu kubwa ya deni lake na pia Shirika la Umeme Zanzibar.

UWEKEZAJI TTCL
Katika hatua nyingine, Sigalla alisema Serikali inapaswa kuwekeza kwa kuipa fedha TTCL kwa ajili ya kuimarisha miundombinu yake kwa kuwa ushindani katika sekta ya mawasiliano ni mkubwa.

Sigalla alisema hivi sasa TTCL inahitaji kiasi cha dola za Marekani milioni 400 ili kuimarisha miundombinu yake na kufikia mikoa yote.

Alisema Kamati inaamini zipo njia nyingi ambazo Serikali inaweza kufanya pia ili kuinusuru TTCL,

Mojawapo ikiwa ni kununua hisa asilimia 60 zinazomilikiwa na Airtel Tanzania na kuwa na hisa zote asilimia 100. 


Alisema ni hatari kwa nchi kutokuwa na kampuni yake ya mawasiliano yenye mtandao mpana na kufika nchi nzima.NIPASHE
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: