BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

TFDA YAPOKEA MAOMBI YA USAJILI WA VIWANDA VIPYA 767

KATI ya Julai mosi mwaka jana hadi Machi mwaka huu, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imepokea maombi mapya ya usajili wa viwanda 767 vinavyojishughulisha na uzalishaji wa bidhaa vinavyodhibitiwa na mamlaka hiyo.

Baada ya tathimini na ukaguzi wa maombi hayo, viwanda vipya 635 vilisajiliwa vikiwemo vikubwa vya kati na vidogo (chakula 613, dawa kimoja na vipodozi 21). Zaidi ya asilimia 75 ni vidogo.

Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Hiiti Sillo alisema jana mjini hapa kuwa idadi hiyo ya viwanda vipya vilivyosajiliwa ni sawa na asilimia 82.8 ya maombi yote na hivyo kuashiria viwanda vingi vimezingatia sheria.

Sillo alieleza kuwa hayo ni miongoni mwa mafanikio ya utekelezaji kwa vitendo dhana ya Tanzania ni viwanda ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kuimarisha udhibiti wa ubora, usalama na ufanisi wa chakula, dawa, vipodozi na vifaa vya tiba.

Alikuwa akizungumza kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri kufungua kikao kazi cha wahariri wa vyombo vya habari nchini juu ya usimamizi wa sheria, majukumu ya TFDA kwenye Ukumbi wa Isike Mwanakiyungi mjini hapa.

Sillo aliongeza kuwa katika kipindi hicho cha Julai 2016 hadi Machi, 2017, mamlaka ilifanya tathimini ya maombi 4,762 (82.1%) ya usajili wa bidhaa za dawa, chakula, vifaa vya tiba na vipodozi, kati ya maombi 5,802 yaliyowasilishwa.

Alisema kati ya maombi hayo, 4,322 yaliidhinishwa ambayo ni asilimia 75 na 440 yalikataliwa kwa kutokidhi vigezo. Akizungumzia uchunguzi wa bidhaa za chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba, Sillo alisema katika Serikali ya Awamu ya Tano jumla ya sampuli 8,066 kati ya sampuli 6,697 sawa na asilimia 83 zilifaulu na sampuli 347 hazikukidhi vigezo na hivyo bidhaa husika kutosajiliwa na au kuondolewa katika soko.

Alisema kati ya tani hizo 631.7, tani 497.3 zenye thamani ya Sh 601,301,867.9 zilitolewa taarifa kwa hiari na wahusika na tani 134.4 zenye thamani ya Sh 196,010,235.25 zilikamatwa katika ukaguzi mbalimbali uliofanywa na TFDA.

Alitoa mfano wa mfumo mpya wa kielektroniki wa utoaji wa taarifa za madhara ya dawa (ADR) umekuwa na mfano ambapo kwa kipindi cha miezi mitano tangu kuzinduliwa kwake Oktoba 12, 2016 jumla ya taarifa mpya 71 Sawa na asilimia 44 ya taarifa zote za ADR zimepokelewa na kufanyiwa tathimini.

Akifungua kikao kazi hicho, Mkuu wa Mkoa Mwanri aliwataka wanahabari kote nchini kuisaidia TFDA na Taifa kwa ujumla katika kuwaelimisha wananchi kuhusu usalama na ubora wa bidhaa zinazodhibitiwa na TFDA.

TFDA iliyoanzishwa Julai mosi 2003 ni taasisi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto yenye jukumu la kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa chakula, dawa, vipodozi na vifaa vya tiba.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: