BannerFans.com

SUZAN KIWANGA, LIJUALIKALI WAONJA JOTO YA JIWE MAHAKAMANI MOROGORO

Millionaire  Ads

SAKATA LA VYETI FEKI VYAZUA TAHARUKI HOSPITALI YA TAIFA YA MUHIMBILI, WATUMISHI 134 WASOMBWA

SAKATA la vyeti ‘feki’ vya kielimu na taaluma kwa watumishi wa umma, limezua taharuki ya aina yake katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), baada ya kubainika kuwapo kwa watumishi 134 wasio na sifa huku wengi wao wakinaswa katika Idara ya Dharura na wodi zikiwamo za Wazazi na Mwaisela.

Kutokana na hali hiyo, tayari athari za kishindo cha vyeti feki kimetua hospitalini hapo baada ya uongozi wa MNH kuwaonyesha mlango wa kutokea wafanyakazi wake hao 134, waliojumuishwa katika orodha itokanayo na uhakiki kabambe ambao ripoti yake ilikabidhiwa hivi karibuni kwa Rais John Magufuli, tukio lililofanyika mjini Dodoma na kurushwa ‘live’ kupitia matangazo ya runinga.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Lawrance Museru, wafanyakazi hao waliokutwa na vyeti feki wametakiwa kuondoka sehemu zao za kazi mara moja kuanzia jana.

Aidha, taarifa hiyo imeonyesha kuwa eneo lililoathirika zaidi kwa watumishi wake wengi kubainika kuwa na vyeti ‘feki’ ni wa Idara ya Dharura ya Utoaji Dawa ambayo watumishi 20 wamenaswa na kutakiwa kuondoka.

Idara nyingine ni uzazi ambayo watumishi 19 wamebainika wakiwa na vyeti feki, wengine wakiwa ni wa wodi za Mwaisela watumishi 14, maabara ya uchunguzi (14) na jengo la watoto watumishi 11.

Taarifa hiyo ya Mkurugenzi Mkuu MNH ilisema kuwa wafanyakazi hao (134) wamebainika kughushi vyeti vyao vya elimu ya sekondari na hivyo wamekosa sifa za kuendelea kuwa watumishi wa umma.

“Wakuu wa Idara na Majengo wanatakiwa kuhakikisha kwamba wafanyakazi wanaohusika hawaendelei kutoa huduma kuanzia sasa,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo, ikimkariri Prof. Museru.

Ilielezwa kuwa endapo kutakuwa na mfanyakazi ambaye hataridhika na uamuzi huo, utaratibu ni kwa mhusika kukata rufani kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa umma na Utawala Bora kabla ya Mei 15, mwaka huu.

Taarifa hiyo iliorodhesha majina ya watumishi hao waliobainika kuwa na vyeti vya kughushi pamoja na idara zao walizokuwa wakifanyia kazi.

Idara zingine ambazo zitaathirika ni pamoja na Rekodi ya Dawa (tisa), wodi ya Kibasila (watano), Idara ya Upasuaji (wanne), wodi ya Sewahaji (watatu) na Idara ya Utafiti na Ushauri watumishi watatu.

Zingine ni Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) watumishi watatu, Ushonaji na Upigaji pasi (wawili), Idara ya Mapokezi kwa wagonjwa wa nje watumishi wanne, Taasisi ya Sayansi Shirikishi za Afya (mmoja), Idara ya Fedha (watatu), kurugenzi ya ufundi (watatu), kurugenzi ya rasilimali watu (wawili) na kurugenzi ya upasuaji watumishi wanne

Operesheni ya uhakiki wa vyeti vya elimu na taaluma kwa watumishi wote wa umma ilianza kushika kasi baada ya kuingia madarakani kwa serikali ya awamu ya tano, chini ya Rais John Magufuli. 


Lengo la ukaguzi huo ni kuongeza ufanisi katika kazi ya kuwatumikia Watanzania na pia kutoa fursa za ajira kwa wataalamu wa fani husika katika kila nafasi baada ya kuondoshwa kwa ‘wataalamu bandia’.

Katika ripoti ya operesheni hiyo, zaidi ya watumishi 9,932 kutoka tasisi mbalimbali za serikali walibainika wakitumia vyeti feki, hali iliyomlazimu Rais Magufuli kutangaza kuwa waondoke wenyewe kabla ya Mei 15, mwaka huu na kwamba, vinginevyo wahusika watachukuliwa hatua kali za kisheria. 


Baada ya kutoa agizo hilo, Rais Magufuli alimwagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala bora, Angela Kairuki kutangaza nafasi za kazi ili kuziba nafasi ya watumishi hao waliobainika kuwa na vyeti feki.Nipashe
Share on Google Plus

About Juma Mtanda

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
Post a Comment
Millionaire  Ads