BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MTUMISHI WA SERIKALI IDARA YA ELIMU ASHINDA UCHAGUZI NDANI YA CCM WILAYA YA MVOMERO MOROGORO


Uchaguzi wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wilayani Mvomero umeibua sintofahamu baada ya mtumishi wa Idara ya Elimu, Salvatory Richard kushinda uenyekiti.

Richard ameshinda nafasi hiyo kwa kupata kura 226 katika uchaguzi uliofanyika jana Jumamosi baada ya kumbwaga Dominick Elisha aliyepata kura 138.

Baada ya uchaguzi, Elisha amehoji uhalali wa Richard kugombea nafasi hiyo wakati akijua ana jukumu lingine la kuitumikia Serikali kupitia nafasi yake ya utumishi wa umma.

“Kwa nini watumishi wa umma wanajiingiza kwenye siasa, huku wakijua wazi kuwa wao wanapaswa kuitumikia Serikali kupitia ofisi zao na kama watumishi wanahitaji hizi nafasi za kisiasa basi waachie nafasi zao za utumishi,” alilalamika Elisha.

Richard alipotafutwa kuzungumzia suala hilo leo Jumapili, amesema atatoa ufafanuzi kesho kwa kuwa amechoka na pilika za uchaguzi na asingeweza kuzungumza lolote.

“Mwandishi naomba uniache nipumzike maana hivi (saa nne asubuhi) ndio narudi kutoka kwenye pilika za uchaguzi naomba tuonane kesho Jumatatu ofisini ili tuweze kuzungumza kwa kirefu,” amesema Richard.

Akizungumzia suala hilo, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilayani Mvomero, Ally Castro amesema kila mwanachama wa CCM ana haki ya kugombea nafasi yoyote ndani ya chama hicho.

“Hata mimi nimesikia kuwa ni mtumishi wa Serikali ila sina uhakika lakini ninachofahamu mwanachama yeyote anayo haki ya ama kuchagua au kuchaguliwa katika kuongoza chama,” amesema.

Alipotakiwa kuzungumzia suala hilo, Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro, Kulwa Milonge amesema ofisi yake haina taarifa kama kuna mtumishi aliyeshinda nafasi hiyo lakini kama ni mwanachama anaruhusiwa kugombea.

Milonge amesema hakuna kanuni ya chama hicho inayomzuia mtumishi kugombea kwa kuwa kila mwanachama anaruhusiwa kugombea lakini suala la utumishi ataamua mwenyewe na mwajiri wake.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mvomero, Florent Kyomo amethibitisha kuwa Richard ni mtumishi wa Idara ya Elimu katika halmashauri hiyo ambaye kwa sasa yupo masomoni. 


"Ni kweli huyu ni mtumishi wa halmashauri yangu na kwa sasa yupo masomoni lakini bado sina uhakika kama ameshinda uchaguzi wa CCM, hebu niache nifuatilie kwanza," amesema Kyomo.Mwananchi
Share on Google Plus

About Juma Mtanda

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
Post a Comment