BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

HUU NDIO MUUJUZI WA MTI WA MLONGE KATIKA KUOKOA MAISHA YA BINADAMU KWA KUTIBU MAGONJWA SUGU


Mti wa mlonge

MIMEA mbalimbali imekuwa ikitumika kama dawa na kuwezesha watu wenye matatizo mbalimbali yakiwamo maradhi sugu kupata ahueni.

Moja ya mimea hiyo ni mti wa mlonge ambao umeelezwa kuwa na faida mbalimbali katika mwili wa binadamu ikiwamo shinikizo la damu na kwa kinamama wanaonyonyesha.

Mlonge kama wengine ambavyo wamekuwa wakiuita moringa, umeelezwa na wataalamu wa masuala ya afya kuwa na faida mbalimbali kwa afya kutokana na kuwa na virutubisho vingi.

Daktari wa Hospitali ya Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa, Seleman Hassan, aliiambia Nipashe jana kuwa mti huo umejaaliwa kuwa na virutubisho mbalimbali kuanzia kwenye majani, mbegu, mizizi na magamba yake.

“Matumizi ya mlonge huwaongezea kiwango cha maziwa wanawake wanaonyonyesha na wale wanaosumbuliwa na maumivu wakati wa hedhi kuisha,” alisema.

Dk. Hassan alisema utafiti mbalimbali uliofanyika umethibitisha kuwa mlonge husaidia kutibu matatizo ya shinikizo la damu (BP),
ambayo yamekuwa yakiwasumbua watu wengi kwenye jamii, hususan wenye umri mkubwa.

Pia alisema virutubisho vinavyopatikana kwenye mlonge hurudisha heshima ya ndoa huku watu wenye upungufu wa kinga mwilini wakiimarika kiafya.

“Kiini cha mbegu ya mlonge kina vitamini ya kujitosheleza ambayo husaidia wanaume kudumu kwa muda mrefu katika tendo la ndoa na huwaongezea hamu ya tendo hilo wanawake na wanaume pia.

“Madini ya zinki yanayopatikana kwenye mlonge huwawezesha wanaume kutengeneza shahawa za kujitosheleza na kwa wanawake, vitamini A, B na C zinazopatikana ndani yake huwawezesha kupata ujauzito kwa urahisi badala ya kutumia dawa za kizungu za kupevusha mayai,” alisema.

Pia alisema mlonge una virutubusho vya nyuzinyuzi ambavyo humwezesha mtu kupata choo na kwa wale wenye matatizo ya usingizi pindi achukuapo majani ya mti huo na kuyaweka kwenye maji kisha kunywa, tatizo hilo huisha.

“Mlonge huondoa aina zote za saratani katika mwili. Na matumizi ya mara kwa mara humwezesha mtu kupata madini ya chuma ambayo humwepusha na matatizo ya upungufu wa damu na ugonjwa wa kisukari,” alisema na kuongeza kuwa: “Pia huondoa mafuta katika moyo na kumwacha mtu salama na kuishi maisha marefu.”

Dk. Hassan alitaja faida zingine zinazopatikana kwenye mlonge kuwa ni kuweka sawa homoni, kuondoa lehemu na hupunguza mafuta tumboni.

“Husaidia kutibu kisukari, shinikizo la juu la damu, hutuliza mapigo ya juu ya moyo na hutibu matatizo au maumivu ya mishipa ya damu.

“Mlonge una kalsiamu nyingi, una vitamini C, potasiamu, vitamini za aina mbalimbali, protini nyingi, klorofili (kemikali ya rangi ya kijani ipatikanayo katika mimea), madini chuma, Omega 3, 6, na 9, asidi amino zile muhimu zaidi zinazohitajika mwilini.

“Una kiasi cha kutosha cha madini ya zinki ambayo ni muhimu katika kuongeza homoni za kiume na nguvu za kiume,” alisema.

Dk. Hassan alisema kutokana na virutubisho hivyo, mtumaji wa mlonge anaweza kujiepusha na kikohozi, maumivu ya kichwa na husafisha ini.

“Mlonge husaidia kusafisha kibofu cha mkojo na kibofu, huondoa uchafu mwilini, hutibu vidonda vya tumbo, kifua kikuu, mzio, maambukizi kwenye ngozi, husafisha damu, hutibu kipindupindu, matatizo ya macho na kwenye masikio, homa na kuondoa chunusi,” alisema. 


Kadhalika, alisema hutibu matatizo ya mfumo wa upumuaji, gauti, matatizo ya kuhara damu, minyoo, kisonono na kwa wale wenye matatizo ya ukosefu wa usingizi pamoja na kuimarisha misuli ya mwili na kutibu magonjwa ya mifupa pamoja na kuongeza kwa kasi kinga ya mwili.Nipashe
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: