BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

PATROBAS KATAMBI JINSI ALIVYOWAPIGA CHENGA CHADEMA NA KUTUA CCM BILA KINYONGO


Aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (BAVICHA) Patrobas Katambi, akizungumza na kukaribishwa kurudi CCM mbele ya Mwenyekiti wa Chama hicho, Rais John Magufuli wakati wa kikao Cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kilichofanyika jijini, Dar es salaam jana. Picha na Ikulu

Aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), Patrobas Katambi ameacha vumbi baada ya kujiunga na CCM juzi, baada ya kutoweka katika mazingira ya kutatanisha.

Ofisa tawala na rasilimali wa Chadema, Aron Mashuve ambaye alikuwa naye mara ya mwisho, alisema Katambi alitoweka wakati wakipata mafunzo ya kitaifa ya chama na kwamba walishapangwa kimkakati kulingana na kanda.

Lakini, alipoulizwa kuhusu kutoweka kwake, Katambi alisema jana kuwa atazungumzia suala hilo.

“Nimesikia mengi. Nitafanya mkutano na waandishi wa habari,” alisema.

“Nilidhani wangejitathmini katika ukweli ili kusaidia vijana, chama na Taifa, lakini kama wanaamua kushambulia mtu kwa uongo bila ushahidi, nitasema ukweli waziwazi.”

Mashuve aliliambia gazeti hili katika mahojiano maalumu jana kuwa walikuwa kwenye timu ya mafunzo ya kitaifa kwa viongozi wapya, wakiwamo madiwani.

Alisema katika timu hiyo, Katambi alikuwa kiongozi na kulikuwa na wakufunzi 45 ambao waligawana kanda kulingana na jiografia ya nchi.

Ofisa huyo alieleza kuwa, walitoa mafunzo kwa madiwani maeneo ya Longido, Ngorongoro, Mwanga, Same Mashariki na Same Magharibi.

“Mimi na yeye tulikuwa majimbo ya Longido na Ngorongoro akiwa ni kiongozi wa mafunzo kwa viongozi wa halmashauri kwa sababu ni wageni wengi wao walipatikana 2015,” alisema.

“Baada ya kumaliza kutoa mafunzo Karatu, Patrobas akarudi Same ilikuwa siku ya Jumapili. Hapa nilianza kuona mabadiliko.”

Alisema siku iliyofuata saa 3:00 asubuhi, alimpigia simu na kumueleza kuwa kuna mabadiliko yametokea hivyo afike Same haraka amkabidhi baadhi ya vitu.

“Nilipofika nilimuona hayupo kama kawaida, anazungumza huku anatetemeka, anahema sana na hana amani. Nikamuuliza nini tatizo akajibu anauguliwa mama yake ni mgonjwa sana na ameanguka kabisa,” alisema.

Mashuve alisema kwa sababu alitakiwa afundishe mada iliyokuwa inafuata ambayo ni stadi za uongozi, alipoanza kufundisha Katambi alitoweka.

Alisema aliendelea na mafunzo hadi saa 12:30 jioni na alipompigia simu, hakupatikana na hata alipojaribu tena 1:25 jioni na saa 3:30 usiku.

Ofisa huyo alisema alikwenda alikofikia Katambi akaambiwa ameshaondoka.

“Nikalazimika kutoa taarifa kitengo cha ulinzi na usalama wa chama ili wanisaidie kubaini kilichotokea. Ilipofika saa 6:30 asubuhi nikamtumia ujumbe mfupi ‘chairman’. Ulivyopokelewa nikajua anapatikana, nilipompigia alipokea akiwa kwenye eneo lenye mwangwi na kusema samahani Mashuve nitakupigia,” alisema ofisa huyo.

“Hakufanya hivyo hadi ilipofika saa 7:00 usiku akatuma ujumbe kupitia WhatsApp akisema amefika salama na wanafanya utaratibu wa kutafuta ndege ya kumsafirisha mgonjwa kumpeleka Dar kwa ajili ya matibabu.”

Alisema baada ya kupewa pole na wajumbe mbalimbali, Katambi alijibu “ahsante” na kuwatakia mafanikio katika kazi ya ukombozi, lakini Mashuve akahisi kuna jambo, hasa mwenyekiti huyo alipokuwa akichagiza maandamano ya kupinga tukio la kupigwa risasi Tundu Lissu.

Alisema alikuwa akilalamika katika magrupu ya chama akitaka watu waingie barabarani kufanya maandamano na kuchukizwa na uamuzi wa chama wa kumuombea mgonjwa na kuchangia damu.

“Chama kimepooza, kimepoa, tungeingia barabarani kulipinga hili alikuwa akilalamika mara kadhaa,” alisema Mashuve akimnukuu Katambi.

Naye katibu mkuu wa Bavicha, Julius Mwita alisema Jumapili alipokea simu ya Katambi akimtaka amuongezee fedha kwa kuwa alikuwa na dharura. 


Alisema kwa kuwa ni moja ya majukumu yake, alielekeza apatiwe fedha na alipewa.Mwananchi
Share on Google Plus

About Juma Mtanda

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
Post a Comment