BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

SERIKALI YA TANZANIA YAUTAKA UMOJA WA MATAIFA KUFANYA UCGUNGUZI SHAMBULIO JUU YA VIFO VYA ASKARI WA 14 TANZANIA, DRC CONGO


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitoa heshima za mwisho kwa askari 14 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliouawa wakiwa katika operesheni ya ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa nchini Congo (DRC), kwenye viwanja vya Makao Makuu ya JWTZ, Dar es Salaam akimwakilisha Rais Magufuli.

Dar es Salaam.SERIKALI imeutaka Umoja wa Mataifa (UN) kufanya uchunguzi wa kina, wa wazi na wa kweli, wa shambulio lililosababisha vifo vya askari 14 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Askari hao walikuwa katika mpango wa kulinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Shambulio hilo lilitokea Desemba 7, mwaka huu majira ya jioni, ambapo sehemu ya kikosi cha askari hao wa JWTZ kilichopo DRC kilivamiwa na waasi wa kundi la Allied Democratic Forces (ADF).

Askari hao wa Tanzania walikuwa katika kambi ndogo iliyopo eneo la daraja la Mto Simulike, barabara kutoka Oicha kwenda Kamango mpakani mwa Uganda, kaskazini mashariki mwa wilaya ya Beni, Jimbo la Kivu Kaskazini.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitoa agizo hilo wakati wa kuaga miili ya askari hao iliyofanyika Makao Makuu ya jeshi hilo Upanga Dar es Salaam jana. Alisema sera ya nchi ya Tanzania tangu wakati wa Uhuru ni kutetea wanyonge dhidi ya ukoloni, ubaguzi, uonevu na dhuluma na walio katika mazingira hatarishi; na ndio maana nchi imeshiriki kulinda amani katika nchi mbalimbali zilizopo kusini mwa Afrika.

Aliongeza kuwa operesheni zote hizo, askari wa Tanzania wamekuwa wakisifiwa kwa utendaji kazi wao, uvumilivu wao na uhodari wao katika kurejesha hali ya amani katika maeneo husika.

Alisema uwezekano wa askari kujeruhiwa au kuuawa ni mambo yanayofikiriwa kuweza kutokea katika operesheni hizo, ingawa alisema haijawahi kutokea kama ilivyotokea sasa kwa kupoteza idadi kubwa ya askari, kwa kuwa tahadhari zote husika zinachukuliwa kuepusha hatari hizo; na ndiyo maana wanapewa silaha, mafunzo na ushirikiano wa majeshi jirani. “Tunataka UN wafanye uchunguzi kuhusu damu hizi za Watanzania zilizomwagika ili tujue na haki iweze kutendeka, ni matumaini yetu kuwa Umoja wa Mataifa watafanya hivyo kwa haraka,”alisema Majaliwa.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi alisema askari hao wametolewa uhai wakiwa na dhamira thabiti ya kuwawezesha wananchi wa DRC kuishi kwa amani katika nchi yao.

Alisema askari hao watakumbukwa kwa uzalendo wao na kujitoa kwao katika kulitumikia jeshi na nchi na wameacha pengo, ambalo litachukua muda kuzibika. Aidha, Dk Hussein aliwataka maofisa na askari kutokatishwa tamaa na tukio hilo na mengine yaliyowahi kutokea, bali yawe chanzo cha hamasa ya utekelezaji majukumu yao kwa nguvu zaidi na weledi wa hali ya juu ili kukamilisha jukumu ambalo askari hao wameliacha.

“Vifo hivi viwe chachu kwetu kuwa wamoja zaidi, kuelewana zaidi, kupendana zaidi na kushirikiana zaidi katika kutekeleza majukumu yetu na katika maisha yetu kwa ujumla kwa kufanya hivyo tutakuwa tunazienzi roho za askari wetu waliotangulia mbele za haki,” alisema Dk Hussein.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo alisema kikosi cha JWTZ kipo DRC katika operesheni ya kulinda amani tangu mwaka 2013. Kwamba kilichopo hivi sasa ni cha tano, kilichoingia Agosti mwaka huu na kuanza kutekeleza majukumu yake tangu wakati huo.

Alisema siku ya tukio hilo, kikosi hicho kikiwa kambini kilishambuliwa kwa kushtukizwa na waasi wa ADF, ambao walikuwa wanakadiriwa kuwa zaidi ya 200 na kuzusha mapigano yaliyodumu kwa saa 13 na kusababisha askari 14 kuuawa na wengine 44 kujeruhiwa; huku mmoja akiwa hajulikani alipo na jeshi linaendelea na jitihada za kumtafuta.

“Shambulizi hilo lilikuwa ni baya na kubwa ambalo halijawahi kutokea tangu vikosi vyetu vianze kushiriki ulinzi wa amani DRC, limetuletea maafa na madhara makubwa hata hivyo pamoja na madhara na maafa, kikosi chetu bado kina uwezo wa kutekeleza majukumu yake kwa weledi na umahiri mkubwa baada ya kuimarishwa zaidi,” alisema.

Pia alisema jeshi hilo linafanya uchunguzi wa kina ili kubaini mazingira halisi yaliyosababisha mashambulizi hayo ili kuimarisha zaidi kikosi, na kuwa tukio hilo halitawavunja moyo bali linawaongezea nguvu, ari, ushupavu na uhodari katika kukabiliana na matishio mbalimbali yatakayojitokeza.

Kwa upande wake Mkuu wa Ulinzi wa Amani wa UN, Jean Lacroix, alisema umoja huo umesikitishwa na tukio hilo la kinyama lililofanywa na kikundi hicho cha waasi na kwamba UN iko bega kwa bega na Tanzania na familia za askari waliopoteza maisha.

Aidha, alisema umoja huo utaendelea na uchunguzi, kujua nini kilitokea na kuangalia hatua za kuchukua katika kuwalinda wanajeshi wanaolinda amani DRC kutokana kutokea kwa tukio hilo.

Majina ya askari waliouawa Askari waliopoteza maisha ni Sajenti Hassani Abdallah Makame, Koplo Issa Mussa Juma, Praiveti Deogratius Rashid, Praiveti Mwichumu Vuai Mohamed, Praiveti Ali Haji Ussi, Praiveti Hamad Mzee Kamna, Praiveti Juma Mossi Ali , Praiveti Paschal Misingo na Praiveti Idd Abdala Ali. 


Wengine ni Praiveti Shazil Khatibu, Praiveti Hamad Haji Bakar, Praiveti Nassor Daud Iddi, Praiveti Salehe Mahembano na Praiveti Samwel Chenga. Askari tisa kati yao ni kutoka Zanzibar. Waliosalia ni kutoka Tanzania Bara.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: