BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WATOTO WALIVYOGEUZWA KITEGA UCHUMI FAMILIA ZA WILAYA YA MVOMBERO MOROGORO

WASWAHILI wana usemi 'Ukistaajabu ya Musa, utaona ya firauni'. Hilo ndilo linadhihirika ndani ya vijiji vilivyoko katika wilaya ya Mvomero kama Mela, Mlandizi, Kololo na Majengo katika kata mbili za Mangai na Melela.

Nini kikubwa? Ni simulizi ya kutia huzuni, kutokana na wazazi kutumikisha watoto wao wadogo kwa lengo la kuipatia familia kipato.

Kwa kutumikishwa huko, dhana ya shule na safari yake hutoweka, kana kwamba hawasikii shinikizo, wito na mbiu kutoka serikalini katika ngazi mbalimbali, pia mamlaka za umma kama vile asasi za kidini.

Jitihada za serikali, wanaharakati, watetezi wa haki za binadamu na wadau mbalimbali wa kupinga vitendo vya utumikishwaji wa watoto kwa lengo la kujipatia kipato, zinakwamishwa kwa namna ya wazi kabisa.

Sehemu kubwa ya watoto na hasa wa kiume wilayani Mvomero hawasomi, bali wamegeuzwa wazalishaji mali hata kufikia kiwango cha kulea familia kiuchumi kutokana na ujira wanaopata kutoka walikoajiriwa.

Wakazi wa Mvomero wamegawanyika katika sehemu mbili - wakulima na wafugaji - kundi la pili likiwa kwa sehemu kubwa ni wahamiaji mahali hapo, kutoka sehemu nyinginezo ambao walifuata malisho bora ya mifugo yao.

Watoto wengi katika sehemu hizo tajwa, wanaajiriwa kwa mikataba ya ama miezi sita au 12 katika familia za jamii za wafugaji na shughuli kuu huwa ni kuchunga na kutunza mifugo.

Mikataba mingi iliyozoeleka ni kwamba mchungaji kwa mkataba wa miezi sita hupatiwa ndama dume baada ya kumaliza mkataba huo na anayechunga kwa miezi 12 hupatiwa ndama jike.

Uchunguzi uliofanywa na Nipashe katika kata hizo, umebaini asilimia kubwa ya watoto wanaoajiriwa kuchunga ng'ombe ni wa makabila ya nje ya Morogoro na kabila moja tu ndiyo wanaotoka katika mkoa huo.

Sababu ya kutochukua makabila ya Morogoro ni madai kwamba wenyeji wake ni wavivu wa kazi kulinganisha na wanaotoka mikoa tofauti na huo.

Miongoni mwa makabila yaliyopo ni pamoja ni Waluguru, Wandamba, Wakaguru, Wapogoro na Wakutu.

Wafanyakazi hao watoto hupatikana kupitia pamoja na njia nyingine, ndugu na marafiki wanaokuwa kama wakala wao, na wengi ni wa umri wa kati ya miaka sita hadi miaka 12.

Baadhi ya wafugaji waliliambia Nipashe kuwa sababu kubwa ya kupenda kuajiri watoto wadogo ni urahisi wao wa kuelekezwa kazi kuliko wenye umri mkubwa zaidi ya hapo.

Mmoja wa wafugaji hao aliyejitambulisha kwa jina la Jacqueline Kweko, anayeishi katika kijiji cha Mela, anasema yeye ameajiri watoto wanne ambao aliwapata kwa kuletewa na ndugu yake aliyeko mkoani Dodoma.

Jacqueline, mama kutoka jamii yenye asili ya Kimasai, anasema anamiliki ng'ombe zaidi ya 700 na mbuzi zaidi 200 wanaoangaliwa na watoto hao wanne.

Bila ya kumtaja jina, anasema mkongwe kati yao, alimpata akiwa na miaka sita mwaka 2011 na mpaka sasa yuko naye.

Anasema baada ya kuwachukua watoto hao, huanza kwa kuwafundisha kuzungumza Kimasai na mfumo wa maisha ya jamii hiyo ili waendane na uhalisia wa maisha hayo mapya, kisha huchukuliwa kuwa sehemu ya familia.

"Watoto wadogo ndio wazuri kuchunga, kama unao wadogo walete tu, nafasi ipo (maana) wakubwa hawawezi kuchunga na hatupendi kuwachukua kwa sababu wana mambo mengi," alisema Jacqueline, "wanawaza mengi. Wakikaa mwezi mmoja au miwili wanatoroka."

Mfugaji huyo anaeleza zaidi: "Watoto wadogo ukiwachukua unawalea kama watoto wako na hawana mawazo mengine, anawaza kuchunga, kula... basi, lakini mtu mzima atakusumbua vibaya mno!

"Tunapoletewa (watoto), tunakubaliana na wazazi wao, ila ujira wao huwa tunawapelekea wazazi wao. Watoto wenyewe kwa sababu ni wadogo tunawanunulia nguo za kuvaa tu, kuwalisha na labda akiugua ndiyo tunamtibu."Anasema wale wanaowachukua wakiwa wadogo sana, kwa mara ya kwanza baadhi huanza kwa kuchunga mbuzi kwa kipindi kifupi, kabla ya kuanza kuchunga ng'ombe.

Mama huyo tajiri wa mifugo anasimulia kwamba kuna wakati mwingine huwapa waongozane na wenzao wazoefu wanaowafundisha kwa miezi miwili au zaidi kulingana na wepesi wa mtoto husika na kisha huachwa wachunge wenyewe.

"Tunaleta wadogo sana, kwa hiyo ni lazima mwanzoni waanze kuchunga mbuzi au waongozane na wenzao, halafu baada ya hapo wanachunga wenyewe," anasema.

"Mpaka sasa baadhi ya watoto wanaongea lugha yetu na watoto wetu wanaongea lugha ya kwao huko walikotoka kwa sababu wanafundishana. Kwa hiyo kwenye familia zetu unakuta kuna lugha hata zaidi ya tatu ambazo zinazungumzwa."

Anasema kabla ya kupewa mkataba mtoto huonyeshwa kabisa ndama wa ujira wake, ambaye huchanganywa katika wale anaowachunga ili aweze kushuhudia maendeleo ya ukuaji wake.

Jacqueline anasema iwapo ng'ombe wa mkataba ni jike na akibahatika kuzaa, basi anakuwa faida ya mtoto."Hiyo ndio faida ya kutumikia ng'ombe jike na ndio maana huyu anatumikiwa kwa kipindi kirefu tofauti na ilivyo ng'ombe dume," anasema Jacqeline.

"Ili apatiwe ng'ombe jike, mtoto anaweza akachunga kwa miezi 12 au zaidi kulingana na makubaliano, na dume mara nyingi ni miezi sita tu." Mbali na ujira wa ng'ombe hata

hivyo, pia kuna malipo ya fedha taslimu.

Hata hivyo, malipo hayo yanatofautiana kati ya mtoto mmoja na mwingine kulingana na makubaliano ya waajiri na wazazi wa mtoto husika.

Imebainika kiwango cha mshahara ni kati ya Sh. 30,000 na Sh. 50,000 kwa mwezi, malipo ambayo hutumwa moja kwa moja kwa mzazi au mlezi anayesimamia mkataba husika. Njia kuu ya utumaji malipo hayo mitandao ya simu za mkononi.

Mfugaji mwingine, Benjamini Mujalisho wa kijiji cha Mlandizi, kata ya Melela, anaeleza kuwa ujira huo wa fedha hutofautiana kwa sababu ni makubaliano yanayofanywa kulingana na ukubwa wa kundi la ng'ombe wanaohitaji kuhudumiwa.

"Unakuta mwingine ana ng'ombe 200, 600 au 700, kwahiyo malipo nayo hayawezi kufanana," anasema Mujalisho. "Ukiwa na ng'ombe wachache na malipo nayo yanabidi yashuke kidogo, lakini ukiwa nao wengi, malipo nayo yanaongezeka kidogo."

Kama ilivyo kwa Jacquelinea, Mujalisho naye anakiri kwamba asilimia kubwa ya wanaodumu katika ajira ni watoto wadogo, akitaja umri wao kuwa ni kati ya miaka saba hadi 11.

"Pia kuna baadhi ya makabila hatuchukui watoto (wake) kwa sababu siyo makabila yote yanaweza kuchunga," anasema Mujalisho.

"Wengine hawawezi na wazazi wengine kwa sababu huwa na shida ya hela, kwa hiyo huwa hawaoni shida kuwatoa watoto wao kuwaleta huku.

"Watoto wadogo kama hawa hawana shida, hawajui matumizi ya hela kwa hiyo wazazi ndio huwa wenye shida, isipokuwa kikubwa huwa tunakubaliana hela ya mwezi tunakuwa tunawatumia wao.

"Kwa sababu hiyo, unakuta mzazi anaridhika kwa sababu inamsaidia na pengine anaweza kukuachia mtoto mpaka anakulia mikononi mwako na kwa kuwa wanakuwa wamejifunza tabia za kwetu tangu wakiwa wadogo huwa ni rahisi kuishi nao."

Takwimu zilizotolewa na asasi ya International Resque Committee (IRC) mwaka 2012 inaonyesha asilimia 27.5 ya watoto wenye umri chini ya miaka 17 hushirikishwa katika ajira hatarishi, ikiwamo kazi za majumbani, sehemu za starehe, uvuvi, migodi na shambani, hivyo kuthibitisha uwapo wa tatizo la ajira za watoto nchini.

Aidha, pamoja na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004 kukataza mtoto mdogo kuajiriwa isipokuwa kazi nyepesi na ambazo siyo hatarishi kwa afya na zisizoleta athari kwa mahudhurio yake shuleni, bado inaonekana kutoheshimiwa ipasavyo.

Sheria hiyo hiyo inatamka kuajiri mtoto mdogo kuwa ni kosa la jinai na kwamba ambaye atabainika kutenda kosa hilo adhabu yake ni kifungo cha mwaka mmoja, au faini isiyozidi Sh. milioni tano, au vyote kwa pamoja.

HAJUI KUSOMAAmoni Zabloni (11) ni muajiriwa anayesema alianza kuchunga ng'ombe akiwa na umri mdogo (akionyesha kwa kidole mtoto aliyeambatana naye).

Zablon ambaye ana miaka mitano tangu aanze kuchunga mifugo anasema awali alikuwa akiishi na mama yake mkoani Dodoma na hakuwahi kupelekwa shule.

Zabloni anasema hajui kusoma wala kuandika licha ya kwamba anamudu vyema kuhesabu fedha, kiasi cha kuwa hawezi kudhulumiwa.

"Mimi nililetwa huku kuanza kuchunga ng'ombe nikiwa mdogo kabisa. Nilikuwa ni mdogo kuzidi hata huyu unayemuona, lakini nilianza kuchunga na wenzangu niliowakuta," anasema Zabloni na kueleza zaidi:

"Nilichunga kwa pamoja na wenzangu kwa muda mfupi (kisha) nikaanza kwenda mwenyewe, na walinionyesha ng'ombe wangu ambaye walisema nitapewa nikishamaliza miezi sita."

Anasema katika familia hiyo alikoajiriwa kuchunga ng'ombe, kuna watoto wengine wawili walioajiriwa kama yeye, ambapo wawili wanalipwa ujira wa mkataba wa miezi sita kwa ng'ombe dume na mmoja anamtumikia ng'ombe jike kwa mkataba wa miezi 12.

Zabloni anasema yeye peke yake anachunga ng'ombe 400 na kwamba huwafungulia kila siku saa tatu asubuhi kwenda malishoni na kuwarejesha kati ya saa 11.00 na saa 12.00 jioni.

Anasema tangu aajiriwe kuchunga ng'ombe, kwa kipindi cha miaka hiyo mitano hajawahi kurudi Dodoma na kwamba tayari ameshazoea maisha ya familia za kifugaji.

"Mwanzoni kabisa wakati nimekuja huku, nilipata shida sana kuzoea maisha ya huku kwa sababu ni porini na hata lugha yao na vyakula vyao wanavyokula vilikuwa vinanishinda. Sasa hivi nimezoea kabisa na nimekuwa kama wao," anasema Zabloni, katika vazi la kimasai.

Anasema katika kipindi hicho chote tangu aanze kuchunga, amepata ng'ombe 10 na wameshasafirishwa kupelekwa kwa mama yake.

"Ninachoshukuru ni kwamba wafugaji wakishakuonyesha kwamba huyu ndiye ngombe wako, huwa hawawezi kukunyang'anya tena, hata kama akizaa," anasema. "Hiyo (kuzaa) inakuwa faida yako".

"Kwa kweli nafurahi kufanya nao kazi na nitaendelea mpaka niwe na ng'ombe wengi ili wanisaidie mimi na mama yangu nyumbani."

Akielezea ratiba ya maisha kwa siku, Zabloni anasema kabla ya kwenda machungoni asubuhi huwa wanakula, pia jioni baada ya kurejesha ng'ombe saa 11.00 au 12.00 hukuta wameshapikiwa.

Kwa upande wa mavazi, anasema amekuwa akipewa na mwajiri wake nguo wanazotumia kujifunga 'lubega'.

"Tajiri yangu mimi ni Mmasai. Kama unavyoniona, nimejifunza hata kuvaa kama wao na huwa wananiletea wenyewe. Nimezoea kabisa na hata nikikutana na mtu atajua tu kwamba na mimi ni Mmasai, kwa sababu huwezi kututofautisha," anasema Zabloni.

Kuhusu endapo akipata nafasi ya kwenda shuleni, Zabloni anaonyesha shaka akisema haamini kufanya vizuri shuleni kama wenzake kwa sababu ameshazoea kuchunga ng'ombe.

"Sijui kama nitakuwa na akili kama wenzangu, naogopa nitakuwa wa mwisho, ila natamani na mimi nijue kusoma na kuandika," anasema Zabloni.

Rutu Afidhi (9), ambaye naye ameajiriwa katika familia ya wafugaji katika kijiji cha Majengo, kata ya Mangai, anasema mara yake ya kwanza kufanya kazi hiyo na alianza Julai, mwaka jana.

Yeye anasema ni mzaliwa wa mkoa wa Iringa na hajawahi kwenda shule na alipelekwa kufanya kazi hiyo na anayemtaja kuwa "baba mmoja" aliyemchukua nyumbani kwao.

"Alikuja nyumbani kunichukua, sijui aliongea nini na baba na ndio mimi nikaletwa huku kuchunga ng'ombe," anaeleza mtoto huyo na kwamba amekuwa akichunga na wenzake watatu kwa sababu mifugo ni mingi.

"Niliambiwa kuwa hela ninayochunga wanapeleka kwa baba yangu. Mimi sijawahi kupewa hata mara moja," anasimulia Rutu.

Alipoulizwa endapo anafurahia kazi hiyo, Rutu anasema ni ngumu kwake kwa sababu mara nyingi anashinda porini, juani na kutembea umbali mrefu kutafuta malisho bora ya ng'ombe.

"Mimi natamani kwenda shuleni, baba yangu alisema hawezi kunipeleka kwa sababu hana uwezo wa kuninunulia sare za shule kwa hiyo akasema akipata hela ataninunulia niende, lakini hakunipeleka mpaka nimekuja huku," anasema Rutu.

Sheria ya Elimu ya Mwaka 1978 na rekebisho lake Sura ya 353, kifungu namba 35(3) ya mwaka 2002 inalenga kuwa kila mwanafunzi akijiandikisha shule, hanabudi kuhudhuria na kumaliza shule katika ngazi husika.

Aidha, mipango yote ya Elimu ikiwamo wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES), inasisitiza wanafunzi kuandikishwa, kuhudhuria na kumaliza masomo katika ngazi husika.

Amosi Kuvila (13), ambaye amekuwa akichunga ng'ombe na Rutu kwa mwajiri mmoja, anasema ameshazoea kazi hiyo kwa sababu ameifanya kwa miaka mitatu sasa.

AMEKUWA MZITOAnasema ingawa ameanza kuchunga na Rutu miezi sita iliyopita, maendeleo yake bado siyo mazuri na kwamba hawezi kuachiwa mwenyewe mpaka atakapoweza vizuri.

"Mimi nimeshakuwa mzoefu na kazi hii, lakini ninavyomuona Rutu, bado. Siwezi kumwachia ng'ombe akachunga peke yake, anaweza akasababisha matatizo, kwa sababu bado hajaweza vizuri," anasema Kuvila na kueleza zaidi:

"Wakati mwingine anaweza kuona wanaondoka, ukimwambia awarudishe, wengine wanamshinda. Kwa hiyo inabidi niende nikamsaidie.

"Sijui kwa nini amekuwa mzito hivyo wakati mimi nilichunga ndani ya mwezi mmoja nikawa nimeweza, nikawa naachiwa mwenyewe tena ng'ombe wengi tu."

Kuvila anasema Rutu na yeye wamekuwa wakilipwa ujira wa fedha kila mwezi ambazo hutumwa kwa wazazi wao.

"Mimi nalipwa Sh. 50,000 kila mwezi, wanatuma kwa wazazi wangu wananiwekea, lakini nilisikia Rutu yeye bado analipwa Sh.30,000, labda na yeye akizoea atalipwa kama mimi."

Mtoto huyo anasema yuko tofauti na wenzake, kwani aliwahi kuhudhuria shule hadi darasa la pili, lakini akaacha kwa sababu hakuwa anaipenda.

"Mimi mwenyewe ndiyo nilikuwa sipendi shule, wazazi wangu walikuwa wananichapa kila siku nisipoenda shuleni, lakini walichoka wenyewe wakaamua kuniacha mpaka waliponileta huku," Kuvila anasema zaidi.

"Lakini nimezoea na siku nikirudi nyumbani nitakuwa na hela nyingi na nataka nikimaliza mkataba wa sasa hivi nianze kuchunga wa kutumikia ng'ombe, nipate jike ambaye akizaa wanaongezeka."

Anasema kwa sasa anajitahidi kumfundisha Rutu kuchunga vizuri ili naye awe mzoefu mzuri apate mkataba wenye malipo makubwa.

"Unajua sasa hivi 'dogo' (Rutu) bado hajui umuhimu wa hela na ndiyo maana hakazani kufanya kazi, lakini akishaanza kujua atakazana tu."

Rutu na Kuvila licha ya kuwa si wazaliwa wa jamii ya kimasai, lakini walikuwa wamevalia nguo za asili za kabila hilo na walisema wanaweza kuzungumza lugha hiyo wakaelewana nao bila tatizo.

WASICHANA WENGI Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mela, Juvenus Ng'atigwa, anasema katika shule yake asilimia kubwa ya wanafunzi ni kutoka jamii ya kifugaji na kwamba idadi kubwa ni wasichana.

Anasema katika kipindi cha kuandikisha wanafunzi kwa ajili ya darasa la kwanza, wazazi wengi huandikisha wasichana na kubakiza nyumbani wavulana wakichunga ng'ombe.

Alisema wanapowauliza wazazi hao sababu za kubakiza wavulana nyumbani hujibiwa kwamba si watoto wa wazazi hao.

"Baadae huwa tunakuja kugundua kwamba wakati mwingine ni waongo," anasema Ng'atigwa. "Watoto wengine ni wao lakini hao wa kiume wanabakishwa nyumbani kwa shughuli za uchungaji".

"Baadhi yao huwa wamewatoa mikoa mingine na kuwaajiri ambao nao ukiwaona ni wadogo wanaostahili kwenda shule."

Anasema hata baadhi ya wanafunzi wavulana wanaoandikishwa shuleni, mahudhurio yao katika masomo ni ya kusuasua.

Mwalimu Ng'atigwa anataja tatizo jingine la watoto wengi kushindwa kuandikishwa masomoni kuwa ni wazazi kukosa uelewa stahiki kuhusu umuhimu wa elimu.

Anasema huwa wanawashauri wafugaji kutafuta mbadala wa wasaidizi wa kufuga ambao wana umri mkubwa ambao watakuwa wameshamaliza masomo, kuliko watoto wadogo wanaotakiwa kuwa shuleni.

Mwalimu huyo anaeleza masikitiko yake kwamba ushauri huo huwa hauzingatiwi, hata hivyo.

"Unaweza kukuta familia moja ina watoto wanne au watano wanaostahili kwenda shule, lakini anaweza kuandikishwa mmoja tu au wawili, wengine wote wanabakishwa na kuachwa wachunge ng`ombe, kwa kweli huku hili ndio tatizo linalotukabili," anasimulia Mwalimu Ng'atigwa.

MASAFA YA MBALIMwalimu Ng'atigwa anasema kipindi cha kiangazi kati ya Julai-Novemba, wavulana wengi waliaoandikishwa shuleni hutoroka masomo na kujiunga na msafara wa mifugo masafa ya mbali kutafuta malisho ya ng'ombe wa familia.

Anasema katika kipindi hicho malisho huwa ni shida kwa sababu majani huwa yamekauka, hivyo wafugaji wengi kulazimika kusafiri mbali kutafuta malisho.

"Kwa hiyo unakuta katika kipindi hicho watoto nao wanaenda huko kuchunga na kibaya zaidi wazazi hawatoi taarifa shuleni," anasema na kufafanua:

"Kwa hiyo kipindi hicho chote (wanafunzi) wanakuwa nje ya masomo na wanaporudi, wanakuwa wameachwa nyuma sana.

"Mara nyingi katika kipindi hicho ndicho watoto wengi huamua kuacha shule kabisa na tunabakia na wanafunzi wengi wa kike.

"Hata wale wanaobaki na kuendelea inapofika kipindi cha mitihani huwa wanafanya vibaya sana katika mitihani yao ya kupanda darasa na baadhi yao huwa inabidi warudishwe tena darasa, hasa madarasa ya pili na nne.

"Wazazi wengi wao huwa wanapenda kuwaleta watoto wao inapofika kipindi cha mitihani, hata kama walikuwa hawahudhurii masomo na tunapowauliza kwa nini wanawaleta kipindi hicho na ilihali wameondoka muda mrefu hawajahudhuria masomo, huwa wanatujibu kwamba wanataka wafanye tu mtihani ili wapande darasa.

"Lakini sasa wengi wao hupata alama za chini sana, kwa hiyo tuna changamoto kubwa sana katika hilo."

Mwalimu Ng'atigwa anasema kwa mwaka jana, wanafunzi wa darasa la saba katika shule hiyo walikuwa 20, lakini waliofanya Mtihani wa Taifa walikuwa 10, kati yao wasichana wakiwa wanane.

Anasema uwiano huo wa wanafaunzi wa kike na kiume wanaohitimu darasa la saba kila mwaka hufanana mara nyingi.

Ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ya mwaka 2016 inaonyesha kuwa watoto milioni mbili wenye umri kati ya miaka saba hadi 13 hawapo shuleni.

Mwalimu Ng'atigwa sasa anaoimba serikali iingilie kati kudhibiti suala hilo, ili watoto wapate haki yao ya msingi ya elimu.

"Wito wangu kwa serikali ni kuiomba itusaidie katika hili. Lengo letu ni kuona watoto wote wanapata elimu na siyo kukatishwa au kunyimwa haki hiyo muhimu," anasema. "Waangalie namna ya kuwadhibiti hawa wanaowaajiri."

Kiongozi mmoja kutoka jamii ya wafugaji wa Kimasai aliyepo katika kijiji cha Wami-Sokoine wilayani humo, Meti ole Saitoti, anasema mila na desturi za Wamasai zinatoa masharti watoto wanaochukuliwa kutoka kabila jingine, ni lazima wapitie taratibu zote za jadi za kabila hilo kama vile kutoga masikio, kupitia jando la rika na kuwekwa alama nyingine zinazoashiria mila na desturi zake.

Kiongozi huyo anakiri kwamba ni kawaida kwa watoto kujikita katika kuchunga mifugo kwa kuwa ndiyo kazi yao kwa taratibu za mila na desturi za kabila hilo; ukizingatia mifugo ndio utajiri, utambulisho, fahari na heshima kwa kabila hilo.

MIGOGORO WAKULIMA Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Frolent Kyombo, anasema suala la jamii ya wafugaji kutumia watoto katika kazi za kuchunga wilayani humo ni kubwa na linachangia kiasi kikubwa katika migogoro ya wakulima na wafugaji.

"Ninachosema suala la jamii ya wafugaji na hasa wenzetu ambao wako hapa ni kubwa kwa wilaya ya Mvomero, kutumia watoto katika kazi za uchungaji," alisema Kayombo.

Alisema zaidi: "Wakati tunakuja hapa lilikuwa ni kubwa sana na lilikuwa ni sehemu inayosababisha migogoro kati ya wakulima na wafugaji kwa sababu watoto ni wadogo na unakuta mtoto mmoja anachunga ng'ombe 200, kwa hiyo unakuta ng'ombe wanamzidi uwezo.

"Kutokana na udogo wao ilikuwa kama wanachunga karibu na mazao, walikuwa wanashindwa kuwazuia ng'ombe wasiingie shambani kwa sababu wanazidiwa nguvu.

"Kwa hiyo, kupitia Mkuu wa Wilaya, tulipoingia tu Julai mwaka 2016 katika wilaya hii, alitoa katazo kwamba kila mfugaji ahakikishe watoto wenye umri wa kwenda shule waende shule na wasichunge ng'ombe.

"Ndio maana kwa sasa migogoro baina ya wafugaji na wakulima imepungua, isipokuwa tulikuwa hatujui kama wanachukua watoto kutoka sehemu nyingine. Kama hilo lipo inabidi tulifanyie tena kazi kuhakikisha tunalikomesha."

Kuhusu maendeleo yao kielimu, Kyombo anasema kwa watoto wa kifugaji, maendeleo yao si mazuri sana kwa sababu wengi wao mahudhurio yao ni duni.

"Maendeleo ya watoto wa kifugaji walioko shuleni kwa kweli siyo mazuri sana," anaeleza zaidi Kayombo.

"Naweza kusema hivyo, kwa sababu unakuta mtoto anasoma halafu anachomolewa kwa hiyo 'consistence' (mwendelezo) wa mtoto kusoma shule inakuwa siyo nzuri sana, lakini wale wanaobahatika wazazi wao ambao wamekwisha kujitambua wanajitahidi."

Anatoa wito kwa jamii ya kifugaji kuhakikisha inapeleka watoto shule na siyo kuwaajiri katika kazi za uchungaji.

Ofisa Elimu ya Msingi katika Halmashauri hiyo ya Mvomero, Maajabu Mkanyemka, anasema wasichana ndiyo wenye wastani mzuri kuliko wavulana katika kiwango cha ufaulu kwenye shule za msingi wilayani humo.

Anasema wanafunzi wa kike waliofaulu mwaka 2016 kwenda sekondari walikuwa 1,967 ukilinganisha na wavulana 1,584.

Kwa mwaka jana, anasema Mkanyemka, wasichana waliofaulu kwenda sekondari walikuwa 2,361 na wavulana 1,820. 


Ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ya mwaka 2016 inaonyesha kuwa asilimia 30 tu ya wanafunzi nchini ndiyo hufaulu kwenda sekondari huku asilimia 70 ya waliotakiwa kuwepo sekondari wakiwa hawajulikani walipo.Nipashe
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: