BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WANAFUNZI SHULE YA MSINGI BADO WANAENDELEA KUKAA CHINI DARASANI MOROGORO


Mwalimu wa shule ya msingi Mngazi tarafa ya Bwakila halmashauri ya wilaya ya Morogoro, Laurencia Munishi akiwafundisha wanafunzi wa darasa la kwanza waliokaa chini sakafuni baada ya darasa hilo kukumbwa na changamoto ya madawati. Darasa hilo lina wanafunzi 170. Picha na Juma Mtanda
Na Juma Mtanda, Morogoro.
Tunapolalamika kama Taifa kuhusu kukithiri kwa utoro shuleni, tusisahau kutaja vishawishi vinavyochochea hali hiyo.

Miongoni mwa vichocheo vikubwa vya utoro kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, ni pamoja na mazingira yasiyokuwa rafiki kwa wanafunzi shuleni.

Pata taswira ya mtoto wa anayeandikishwa darasa la kwanza kisha anakutana na kibarua cha kukaa kwenye vumbi darasani. Fikra za kuanza kuchukia shule bila shaka zitaanzia hapo.

Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa wanafunzi wa awali na wale wa darasa la kwanza katika shule ya msingi iliyopo Mngazi iliyopo tarafa ya Bwakila mkoani Morogoro, waliokaribishwa shuleni kwa kukaa chini.

Mpango wa elimu bure umefanikiwa kuwaleta watoto wengi shuleni, lakini umesahau kuwa ili kuhimili ongezeko la wanafunzi, shule zinahitaji miundombinu ya kutosha ikiwamo vyumba vya madarasa na madawati.

Kinachoshangaza ni kuwa shule ya Mngazi, haina madawati ya kutosha katika kipindi ambacho fikra za wengi ni kuwa madawati sio changamoto tena shuleni, hasa kufuatia kumalizika kwa kampeni ya usambazaji wa madawati nchi nzima.

Kumbe pamoja na kampeni kabambe ya madawati na mikoa karibu yote kufikia lengo la usambazaji, bado kuna shule madawati yameendelea kuwa adimu.

Lakini kwa shule hii hata kama ina madawati ya kutosha, yangewekwa wapi ikiwa vyumba vya madarasa havitoshelezi?

Hiki ndicho kilichokumba shule hii, ikawa bora wanafunzi wa darasa la awali na la kwanza, wakae chini kwa hoja kuwa hakuna mahala pa kuyaweka madawati.

Athari kwa taaluma.

Kwa utaratibu uliopo, madarasa ya awali, ndiyo yanayojenga msingi wa taaluma wa baadaye kwa wanafunzi.

Ni madaraja ambayo wanafunzi wanafunzwa kuwa mahiri katika stadi za kusoma na kuumba herufi na hatimaye kuandika kwa usahihi.

Ili wanafunzi wapate stadi hizi, uwepo wa madawati ni muhimu.

Mwalimu wa darasa la kwanza katika shule hiyo, Laurencia Munishi, anasema wanafunzi hao wanapokaa chini kwa kipindi chote cha masomo, ni kikwazo cha kuwaandaa kuwa wanafunzi bora.

‘’Changamoto inayowapata wanafunzi hao ni kuandikia kwenye magoti, mapaja au daftari liwekwe chini ya sakafu, hali inayosababisha washindwe kuwa na mwandiko nzuri, anasema.

Sio wanafunzi hao 170, hawana madawati, lakini mwalimu huyo anasema changamoto nyingine ni kuwa wote hao wanalazimika kusoma ndani ya chumba kimoja tena chenye ufinyu wa eneo.

“Napata changamoto katika kufundisha wanafunzi wa darasa la kwanza, chumba cha darasa ni kidogo, wanafunzi wamekuwa wengi, mwaka huu pekee nina wanafunzi 170. Lakini kivumbi kilikuwa mwaka jana, nilikuwa na wanafunzi wa darasa la kwanza 235 ambao mwaka huu wapo darasa la pili,’’ anaeleza.

Hali mbaya shuleni
Shule ya Msingi Mngazi iliyojengwa mwaka 1948, haina changamoto ya ukosefu wa madawati pekee, uongozi wa shule unalia kwa kukosa madarasa ya kutosha kuhudumia wanafunzi 958 ambao baadhi ni matunda ya mpango wa elimu bure.

Mwalimu Mkuu, Wilbard Wenceslaus anasema vyumba vya madarasa vilivyopo ni 14 kati ya 22 vinavyotakiwa ili kwenda sambamba na uwiano wa wanafunzi.

Anaeleza kuwa kutokana na mwitikio wa elimu bure, wazazi wengi hasa wa kata ya Mngazi wamehamasika kuandikisha watoto shuleni, hali iliyoongeza changamoto ikiwamo ya wanafunzi wa darasa la awali na la kwanza kukaa chini kwa kukosa madawati

“Kutokana na idadi hiyo kubwa ya wanafunzi tuna uhitaji wa vyumba 22 vya madarasa ili kuendana sawa na idadi ya wanafunzi wa madarasa matatu ya awali, la kwanza na la pili ambao wanakaa chini ya sakafu na kurundikana chumba kimoja. Kwa sasa tuna vyumba 14 tu kwa idadi ya wanafunzi 958,”anasema.

Kuhusu athari ya wanafunzi wa madarasa ya chini kukaa chini, mwalimu Wenceslaus, anasema: “Zipo athari za moja kwa moja kwa wanafunzi kukaa chini. Kwanza mwanafunzi anashindwa kuumba herufi na anachafuka. Lakini kuna jitihada zinazofanywa na serikali ya kijiji kujenga chumba cha darasa na ofisi ya walimu.’’

Changamoto nyingine anataja ni uhaba wa walimu, kwani waliopo ni 10 huku mahitaji halisi ya shule ikiwa ni walimu 23.

‘’ Majengo ya shule hii iliyojengwa tangu mwaka 1948, yamechakaa na yanahitaji ukarabati mkubwa. Imefikia kipindi mvua ikinyesha maji yanajaa ndani ya vyumba vya darasa kwa kuwa mabati yametoboka,’’ anaeleza.

Kauli ya Serikali
Kaimu Ofisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Mbwana Mzandi, anasema halmashauri tayari imeshapokea zaidi ya Sh 500 milioni kutoka mpango wa EPFR. Fedha hizo zitatumika kukarabati baadhi ya shule.

EPFR ni mpango wa Serikali kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu shuleni.

Hata hivyo, wakati shule ya Mngazi inalia na wanafunzi kukaa chini, Mzandi anasema hali ya madawati katika shule yake ni shwari, kama anavyofafanua;

“Kwa sasa katika halmashauri yetu hakuna upungufu wa madawati, kwani tuna zaidi ya madawati 500, lakini baada ya kumaliza zoezi la uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza na kujua idadi ya wanafunzi hao, tutaangalia kama kuna upungufu wa madawati au la,”anasema.

Mwenyekiti wa bodi ya shule ya shule, Sinahamu Swala anasema kulikuwapo mpango wa kujenga chumba kimoja cha darasa pamoja na ofisi ya walimu, lakini baada ya Serikali kuwazuia walimu wa shule za msingi na sekondari wasijihusishe na michango shuleni, mchakato umekwama kwa anachosema kauli hiyo imepokelewa vibaya na wananchi. 


“Rais Magufuli amewazuia walimu wasijihusihe na michango ya aina yoyote shuleni na kutangaza elimu bure. Hii imetafsiriwa vibaya kwani hakuwazuia wananchi kuchangia elimu. Shida iliyojitokeza wananachi haohao wamefikia hatua ya kudai kile walichochanga kwa ajili ya watoto wao,’’ anafafanua.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: