SPIKA SPIKA WA BUNGE ANNA MAKINDA.
DK SLAA.
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimewazuia wabunge wake kuhojiwa na Kamati ya Haki, Mamlaka na Madaraka ya Bunge, hadi hapo Spika wa Bunge, Anne Makinda, atakapokuwa ameweka hadharani majibu ya hoja kumi zilizotupwa pamoja na rufaa zilizofikishwa kwake.
Hatua hiyo inakuja wakati Bunge likiwa limepamba moto kwa wabunge wa kambi ya upinzani, kuonesha wazi kutoridhishwa na uamuzi wa kiti cha spika ambacho kinalalamikiwa kwa kutowatendea haki.
Kwa siku mbili mfululizo, Bunge limelazimika kuahirisha vikao kabla ya muda wake kutokana na kutokuelewana kwa wabunge wa upinzani, kiti cha spika na serikali kwa upande mwingine wakati wa kujadili na kupitisha hoja binafsi.
Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alitoa msimamo wa chama jijini Dar es Salaam jana, akisema kuwa wanalaani vikali uamuzi unaofanywa na kiti cha spika kwa kuwa umejaa upendeleo na ubaguzi hali inayokiondolea sifa chombo hicho.
“Tunalaani namna Spika Makinda anavyoendesha kiti chake, kwa wamaofuatilia Bunge watakubaliana na mimi kwamba ni kichaka cha uovu kwa maana limejaa uovu na ubaguzi sana,” alisema.
Dk. Slaa aliongeza kuwa, Makinda pamoja na wasaidizi wake, wamekuwa wakitumia ubabe kuzima na kuondoa hoja za wabunge wanaotoka katika vyama vya upinzani baada ya kupewa maagizo na Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vikao vingine.
“Kama mlifuatilia Bunge jana na leo.
Naibu Spika amefuta hoja ya Mnyika kibabe pasipo kuwa na madaraka ya kufanya hivyo, lakini sasa Watanzania wanapaswa watambue kuwa ule utukufu wa Bunge umeshatoweka, na bungeni sasa kumekuwa ni sehemu ya kupika majungu, chuki, uongo na kudhalilishana pasipo kuangalia mahitaji ya Watanzania,” alisema.
Alifafanua kuwa Bunge linapaswa kutambua kwamba hoja zinazopelekwa na wabunge wa upinzani ni kwa ajili ya kutetea maslahi ya Watanzania wote na si wapinzani pekee.
Huku akionesha kuchukizwa zaidi na matendo ya Naibu Spika Job Ndugai, alisema kuwa amefanya mazoea kuwakera wabunge wa upinzani ili watoke nje na wao waendelee na shughuli zao huku wakijifariji kwamba wameshinda.
“Baada ya kuona wanakerwa na kiti hicho, sasa wabunge wetu wameamua kuja na mbinu mpya ya kutoa hoja ili ijadiliwe kwa maslahi ya Watanzania, lakini nazo zinatupwa, hili si jambo nzuri hata kidogo,” alisisitiza.
Dk. Slaa aliongeza kuwa, ili kukomesha hali hiyo, CHADEMA itazipeleka hoja zake katika mahakama ya wananchi ili waweze kutoa hukumu ya kweli kutokana na vile walivyoona katika Bunge.
Kwamba Makinda kuwataka wabunge wake wakate rufaa wanapoona hawajatendewa haki, imekuwa ikitumika kama kiini macho kwani hakuna majibu ya rufaa zao kwa kipindi kirefu.
“Ni huyu Spika Makinda ambaye mpaka sasa ameshindwa kutoa majibu hadharani ambayo aliwataka wabunge wetu kuweka hadharani uthibitisho wa baadhi ya mawaziri na wabunge kuwa ni waongo.
“Mnakumbuka Godbless Lema alitoa ushahidi kuhusu Waziri Mkuu kusema uongo kwa yaliyotokea Arusha, Tundu Lissu dhidi ya tuhuma zake kwa baadhi ya majaji wa Mahakama Kuu na rufaa na hata Meshack Opulukwa aliyesema kuna mkuu wa wilaya alihongwa gari ili awahamishe wananchi kwa nguvu na vyote vilitolewa ushahidi, mbona hatukuyaona majibu?” alihoji Dk. Slaa.
“Mimi nasema afadhali ya Sitta (Samuel) mara kumi kuliko huyu Makinda. Sitta alikuwa na aibu ya kupindisha sheria na ilikuwa ukimbana kwenye hoja anakubaliana na hoja yako kwa manufaa ya Watanzania,” alisema.
Dk. Slaa aliongeza kuwa Bunge la sasa haliwezi kupambana na ufisadi wakati lenyewe linafanya vitendo vya kifisadi kwa wabunge wa upinzani.
Wakati huo huo, viongozi wa Chama cha Wazee wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wamejiunga na CHADEMA wakisema kwamba wanachama wao wapo mbioni kuwafuata.
Makinda kama Ndugai
Baada ya Naibu Spika kuzomewa na wabunge wa upinzani akidaiwa kupindisha kanuni wakati wa kujadili hoja binafsi ya Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), Spika Makinda naye alilazimika kuliahirisha Bunge jana baada ya kupatwa na rabsha kama hizo.
Kufuatia hatua hiyo, Makinda alitangaza kuwa Bunge limeamua kuondoa hoja nyingine binafsi ya Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (CHADEMA) iliyokuwa ijadiliwe jana.
Makinda aliwaeleza wabunge kuwa hatua hiyo ilifikiwa na Kamati ya Uongozi ya Bunge iliyokutana kwa dharura juzi kujadili vurugu zilizojitokeza juzi bungeni.
Alisema tangu Januari 30 hadi jana, Bunge liliamua kuwasilisha bungeni hoja binafsi za wabunge ambazo ziliahirishwa katika mkutano wa tisa wa Bunge kwa nia njema ya kujadiliana masuala makubwa ya kitaifa na kuishauri serikali nini kifanyike ili kukabiliana na matatizo mbalimbali yanayowahusu wananchi.
“Hata hivyo, imelazimu kuahirisha mijadala ya hoja binafsi kutokana na tabia iliyojitokeza ya utovu wa nidhamu kwa baadhi ya wabunge, na hivyo kuamua kwa makusudi kuanzisha vurugu na hivyo kulifanya Bunge lianze kupoteza heshima yake ya kibunge,” alisema.
Alisema hoja binafsi za wabunge zinaongozwa na kanuni za Bunge kuanzia kanuni ya 53 hadi 58, na kanuni za majadiliano zinaongozwa na Kanuni kuanzia 59 hadi 71 ambazo kwa ujumla wake zikifuatwa kama inavyotakiwa vurugu haiwezi kutokea bungeni.
Makinda ambaye alionekana kuzungumza kwa jazba, alisema katika mkutano huu imeonesha waziwazi baadhi ya wabunge kwa makusudi na kwa nia ya kupotosha wananchi wakitumia vibaya kanuni hizo na wakati mwingine kuwadanganya wananchi ambao kwa bahati mbaya kanuni hizi hawazifahamu.
“Tumeshuhudia mbunge analazimisha na kuhoji mamlaka ya spika kutoa nafasi kwa mawaziri kuzungumza mara baada ya mtoa hoja na kuonyesha kwamba hilo ni kosa, hivyo kuonyesha umma wa Tanzania kuwa kiti kinapendelea.
“Kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na kanuni ya 53(6) (c) ya Bunge, imewekwa bayana utaratibu utakaotumika kwenye hoja hizi kama hoja inayohusika sio ya serikali, msemaji wa serikali atapewa nafasi ya kutoa maoni ya shughuli za serikali juu ya hoja hiyo,” alisema.
Aliongeza kuwa kanuni ya 62 ya kanuni za Bunge imebainisha muda utakaotumiwa na waongeaji kwamba anayetoa hoja anazo dakika 30 na anayetoa maoni ya upande wa pili anapewa muda wa dakika 30.
Alisema spika hataruhusu hoja yoyote inayokiuka katiba au sheria au kanuni za Bunge na katibu atairudisha hoja hiyo pamoja na vielelezo vyake vyote kwa mbunge mhusika na maelezo ya sababu za kukataliwa kwa hoja hiyo yako katika Kanuni 55(9).
Kwa mujibu wa Makinda, iwapo mbunge anapenda kufanya mabadiliko ya maneno aliyotumia katika hoja anayokusudia kuitoa, anaweza kufanya hivyo kwa kutoa taarifa ya kufanya mabadiliko kabla au wakati wa kuwasilisha hoja yake.
Akizungumzia hoja ya Mnyika, alisema ilikidhi vigezo na alipewa nafasi ya kuiwasilisha bungeni.
“Baada ya hoja hiyo kuwasilishwa kwa mujibu wa kanuni ya 53(6) (c) Waziri wa Maji ambaye ndiye msemaji wa serikali kuhusu maudhui ya hoja husika, alipewa nafasi ya kuwa mchangiaji wa kwanza na kutoa maoni ya shughuli za serikali juu ya hoja ya John Mnyika,” alisema.
Alisema maoni ya Waziri wa Maji yalizingatia kanuni ya 57(1) (c) inayoruhusu kuingiza au kuongeza maneno mapya kwenye hoja iliyotolewa.
Kwamba kimsingi Waziri wa Maji aliongeza maneno katika azimio jipya lililoomba hoja ya msingi iondolewe, kwa sababu alizozieleza.
“Hata hivyo, kwa kuwa kanuni za Bunge haziweki ufafanuzi wa maneno gani yatumike katika kuongeza au kupunguza maneno mapya katika kuifanyia mabadiliko hoja iliyowasilishwa, hivyo maneno yaliyoongezwa na waziri ya kuondoa hoja hiyo yalikuwa sahihi na yalikidhi matakwa ya kanuni za Bunge.
“Waheshimiwa wabunge, kwa masikitiko makubwa sote tulishuhudia vurugu zilizojitokeza katika Bunge hili, hasa wakati wa mjadala wa hoja binafsi za wabunge, kimsingi huu ulikuwa ni utovu wa nidhamu wa hali ya juu kutokea katika historia ya Bunge letu.
“Taasisi ya Bunge inalaani vitendo vilivyojitokeza jana vilivyovunja kanuni ya 60(2) inayokataza mbunge kuzungumza kabla ya kuruhusiwa na spika na kanuni ya 60(12) inayowataka wabunge kukaa chini wakati wowote spika anaposimama kutaka kuzungumza,” alisema.
Kutokana na hali hiyo, Spika Makinda alisema Kamati ya Uongozi iliyokutana juzi, iliamua mambo matatu; mosi, kukemea kwa nguvu zote vitendo hivyo na kubainisha kwamba endapo vitaachiwa viendelee, vinaweza kusababisha madhara makubwa kama kupigana ndani ya Bunge.
Pili, kamati ilikubaliana kwamba suala hilo lipelekwe kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili ilichunguze na kuleta mapendekezo bungeni kabla ya mkutano huu wa kumi kumalizika, na kamati ilikubaliana kuwa hoja zote binafsi za wabunge zisiwasilishwe bungeni kutokana na utovu wa nidhamu.
"Mimi naipongeza sana TBC (Televisheni ya Taifa), kuonyesha mjadala wa jana moja kwa moja ili wananchi wawaone wabunge wao waliowachagua. Napendekeza TBC waongezewe fedha ili waweze kufanya kazi vizuri zaidi.
"Mmechaguliwa na maelfu ya watanzania kuingia bungeni, lakini mambo mnayofanya hayaendani kabisa na hadhi yenu," alisema Makinda huku baadhi ya wabunge wakimzomea na wengine kushangilia.
Baada ya kutoa tangazo hilo, Nassari alikuwa mbunge wa kwanza kuomba mwongozo ambapo alisoma kanuni inayoeleza mwenye haki ya kuondoa hoja ni mbunge mwenye hoja.
"Kwa mujibu wa kanuni, mwenye uwezo wa kuondoa hoja binafsi ya mbunge ni mbunge mwenyewe.
Hoja yangu imekidhi vigezo na leo ilipaswa kuja kusomwa, wananchi wangu wamejiandaa kunisikiliza. Kamati ya Uongozi haina mamlaka ya kuiondoa, naomba mwongozo wako," alisema.
Akijibu mwongozo huo, Spika Makinda alisema Kamati ya Uongozi ndiyo inayopanga ratiba za Bunge na ndiyo yenye uwezo wa kuondoa hoja yoyote bungeni.
Alisema mbunge asiporidhika na uamuzi huo, anaweza kukata rufaa kwenye Kamati ya Kanuni.
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu naye aliomba mwongozo kuhoji rufaa zilizokatwa na wabunge kwenye Kamati ya Kanuni, hazijatolewa uamuzi na tatizo ni yeye spika, hivyo lini rufaa hizo zitaamuliwa.
Akijibu mwongozo huo kwa kifupi, Makinda
alisema rufaa hizo bado zinashughulikiwa.
0 comments:
Post a Comment