KOCHA Kim
katikati akizungumza na Waandishi mchana wa leo, kulia Nahodha Juma Kaseja na
kushoto, Katibu wa TFF, Angetile Osiah.
|
Na Mahmoud Zubeiry
KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa
ya Tanzania, Taifa Stars, Mdenmark Poulsen amesema kwamba anataka mechi ngumu
zaidi ili kujenga timu imara ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la
Dunia 2014 nchini Brazil.
Akizungumza katika Mkutano na
Waandishi wa Habari mchana huu kwenye ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), Pouslen alisema kwamba yuko tayari kwa mchezo wowote dhidi ya
timu ngumu kwa ajili ya kuimarisha kikosi chake.
Kaseja
akizungumza na Waandishi leo TFF.
|
Poulsen alisema kwamba ameiandaa
vyema timu yake kwa ajili ya mchezo wa kesho na vijana wake wameonyesha kabisa
wako tayari kwa mechi hiyo, inayotarajiwa kuwa kali na ya kusisimua.
“Tulikuwa tuna mazoezi mazuri jana,
wachezaji wote wameripoti na wako vizuri, wanafahamiana na wamecheza baina yao,
Mtibwa Sugar, Yanga na Azam, wanapeana changamoto. Wanapendana. Napenda sana
kaulimbiu ya Umoja ni nguvu, wachezaji ni wamoja, sisi wote ni wamoja”alisema.
Poulsen alisema kwamba wachezaji
wake wanajua wanatakiwa kucheza vizuri kesho, ili kuwapa changamoto Cameroon
katika mchezo huo, ambao mashabiki wanausubiri kwa hamu.
Kim alisema wananawaheshimu Cameroon
ni timu nzuri na kubwa, yenye wachezaji wazuri, lakini hilo haliwazuii kusema
watashinda mechi ya kesho.
“Tunaamini staili yetu ya uchezaji
itatupeleka katika zama nyingine. Mtindo wetu ni kupiga pasi kwa wingi na
kutengeneza nafasi na kufunga, tukicheza kwa haraka.
Na hata tukipoteza mpira,
tunajituma wote kuutafuta. Nina uhakika wachezaji wako tayari kwa
mechi,”alisema.
Kwa upande wake, Nahodha wa timu
hiyo Juma Kaseja amesema kwamba wako tayari kwa mchezo huo na wanaomba
Watanzania wajitokeze kwa wingi uwanjani kesho kuiunga mkono timu yao.
“Sisi wote ni Watanzania, na wote
tunahitaji furaha, wenyewe watakuwa 11 na sisi tutakuiwa 11 na tunatarajia
utakuwa mchezo mzuri, mgumu na tutaonyesha kile tulichokionyesha kwenye mchezo
uliopita na Zambia,”alisema Kaseja.
Wachezaji 21 wapo kambini Stars
katika hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam ambao ni makipa Juma Kaseja (Simba),
Mwadini Ali (Azam) na Aishi Manula (Azam). Mabeki ni Erasto Nyoni (Azam),
Nassoro Cholo (Simba), Aggrey Morris (Azam), Nadir Haroub (Yanga), Kelvin
Yondani (Yanga), Shomari Kapombe (Simba) na Issa Rashid (Mtibwa Sugar).
Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Simon
Msuva (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Salum
Abubakar (Azam), Khamis Mcha (Azam), Athuman Idd (Yanga) na Mwinyi Kazimoto
(Simba). Washambuliaji ni Mrisho Ngasa (Simba), na Mbwana Samata na Thomas
Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo
(DRC).
Cameroon ilianza kutua jana kwa
mafungu, kundi la kwanza lenye watu 13 likiingia nchini saa 4.40 usiku, kundi
la pili linaloongozwa na Nahodha, Eto’o linatarajiwa kutua leo saa 3.45 asubuhi
kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Eto’o anayechezea timu ya Anzhi
Makhachkala ya Urusi atatua kwa ndege ya Kenya Airways akiwa na Herve Tchami wa
Budapest Honved ya Hungary, beki Nicolas Nkoulou wa Marseille ya Ufaransa,
mshambualiji Jean Paul Yontcha wa SC Olhanense ya Ureno na daktari wa timu Dk.
Boubakary Sidik.
Saa moja baadaye baada ya Eto’o
kutua na wenzake, Kocha wa timu hiyo Jean Paul Akono na msaidizi wake Martin Ndtoungou
watawasili saa 4.40 asubuhi kwa ndege ya Kenya Airways wakitokea Afrika Kusini.
Leo pia kuna kundi lingine
litakaloingia saa 4.40 usiku kwa ndege ya KLM ambalo lina beki Jean Kana Biyick
wa Rennes ya Ufaransa, mshambuliaji Fabrice Olinga wa Malaga FC ya Hispania,
beki Allan Nyom wa Udinese ya Italia ambaye yuko kwa mkopo Granada ya Hispania
na beki wa kushoto Henri Bedimo wa Montpellier ya Ufaransa.
Taifa Stars inayodhaminiwa na
Kilimanjaro Premium Lager itacheza na Morocco, Machi 24 mwaka huu Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam, ikiwa inashika nafasi ya pili katika kundi lake kuwania
tiketi ya Brazil mwakani, nyuma ya Ivory Coast inayoongoza. Timu nyingine
katika kundi hilo ni Gambia.
http://bongostaz.blogspot.com
0 comments:
Post a Comment