MWENYEKITI
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete katika hali
inayoashiria kumjibu rafiki yake, Edward Lowassa ameponda makada wa
chama hicho ambao wamekuwa wakipanda jukwaani kuhubiri kuwa ajira ni
tatizo pasipo kupendekeza suluhisho la tatizo hilo.
Rais
Kikwete ambaye alikuwa akifungua semina ya siku mbili ya Wajumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM mjini Dodoma jana, alisema
kusimama jukwaani na kusema kwamba ajira ni tatizo hakuna maana ikiwa
mhusika hatoi pendekezo la jinsi ya kumaliza tatizo hilo.
Ingawa
hakutaja majina ya wanasiasa ambao wamekuwa wakizungumzia suala hilo
lakini Lowassa, ambaye alijiuzulu wadhifa wa Waziri Mkuu mwaka 2008,
amenukuliwa mara nyingi akiitaka Serikali kuchukua hatua za kukabiliana
na tatizo la ajira kwa maneno kwamba ‘ni bomu linalosubiri kulipuka’.
Lowassa,
ambaye ni Mbunge wa Monduli kupitia CCM, aliwahi kuingia hata kwenye
malumbano makali na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka.
Kabaka
akiwa bungeni mjini Dodoma, Machi 21, 2012 alilazimika kutoa takwimu za
namna Serikali ilivyokuwa inatengeneza ajira kwa nia ya kumjibu Lowassa,
ambaye alikuwa ameeleza tatizo la ajira linavyowaathiri vijana kwenye
moja ya hafla.
Lowassa ameendelea kuzungumzia suala hilo mara kwa mara kila anapopata fursa ya kuhutubia.
“Ndiyo
ajira ni tatizo, hapa mkakati ni ajira itapatikana vipi? Ni tatizo
kweli, tunafanyaje na tunalitatua vipi? Tunataka mtu anayesema kwamba ni
tatizo na apendekeze pia suluhu yake,” alisema Rais Kikwete, ambaye
aliwahi kutamka kuwa Lowassa ni rafiki yake na anafahamika kuwa
alishirikiana naye katika harakati zake za kuwania urais mwaka 2005, na
baadaye akamteua kuwa Waziri Mkuu.
Lowassa,
ambaye ni miongoni wa makada wa CCM wanaotajwa kuwania urais mwaka 2015,
alikaririwa akisema Oktoba 19, 2011 kuwa; “Sijakutana na Rais Kikwete
barabarani, watu waache kunichonganisha naye.” Ilikuwa katika mkutano na
waandishi wa habari jimboni kwake Monduli.
Suala la
ajira nchini ni moja ya mada zinazotarajiwa kuwasilishwa kisha
kujadiliwa katika semina hiyo ya CCM, na Rais Kikwete aliwataka wajumbe
kupendekeza jinsi ya kuongeza ajira nchini wakati mjadala husika
utakapowadia.
Hata
hivyo, Rais Kikwete alisema hivi sasa ajira katika sekta ya umma ni kama
hakuna, kwani zimebaki sekta za afya na elimu na kwamba hivi sasa
suluhu ni kukuza sekta binafsi ili kuongeza ajira.
Alitoa
mfano kwamba wakati yeye alipohitimu kidato cha nne, cha sita na chuo
kikuu hakukuwa na tatizo la ajira kwa kuwa idadi ya wasomi ilikuwa ndogo
ikilinganishwa na mahitaji ya sasa ya soko hilo.
Kikwete
alisema wakati huo Serikali ilikuwa haijajitosheleza, tofauti na sasa
ambapo imefikia ukomo wa kuajiri isipokuwa kwa sekta mbili tu. MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment