Waziri Asiye na Wizara Maalum wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Machano Othman akimkabidhi zawadi ya mfano wa Hundi ya shilingi milioni kumi kwa timu ya KMKM kulia ni Meneja masoko wa Kinywaji cha GrandMalt Fimbo Mohamed Buttal na kushoto ni meneja wa GrandMalt Consolata Adam
Nahodha wa timu ya KMKM akipokea kombe na mfano wa hundi ya Shilingi milioni kumi toka kwa mgeni Rasmi Waziri Asiye na Wizara Maalum wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Machano Oth
man mara baada ya kuwa mabingwa wa ligi kuu ya soka ya GrandMalt.
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
LIGI Kuu ya Zanzibar maarufu zaidi kwa jina la ‘Grand Malt Premier League’ msimu wa 2012/2013 imemalizika rasmi mwishoni mwa wiki kwa kishindo kikubwa, huku KMKM wakiwa mabingwa wapya na Chuoni ikikamata nafasi ya pili.
Waliokuwa mabingwa watetezi Super Falcon limewakuta balaa zaidi kwani ilishindwa kuhimili mikikimikiki ya Ligi Kuu ya Grand Malt na kujikuta ikiteremka daraja.
Kutokana na kufanikiwa kutwaa ubingwa, KMKM itaiwakilisha Zanzibar katika Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati Chuoni wao watakuwa na kibarua kizito katika michuano ya Kombe la Shirikisho.
KMKM wamefanikiwa kuandikia historia mpya ya Ligi Kuu hiyo, kwani wamekuwa mabingwa wa kwanza kutwaa taji toka kinywaji cha Grand Malt ambacho hakina kilevi kilipoamua rasmi kujitosa kuidhamini.
Wakati wanakabidhiwa kombe hilo na Waziri Asiye na Wizara Maalum wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Machano Othman, kulikuwa na shamrashamra za aina yake kutoka kwa mabingwa hao wapya.
Grand Malt waliamua kufanya kweli zaidi, pale mshindi alipokabidhiwa kombe, medali ya dhahabu kwa timu nzima, pamoja na fedha taslimu Sh milioni 10, huku mshindi wa pili Chuoni akipata Sh milioni 5 pamoja na medali ya fedha kwa kila mchezaji.
Golikipa bora bora alikuwa ni Khamis Uzidi wa Zimamoto ambaye alikabidhiwa kikombe pamoja na fedha taslimu Sh 500,000 huku mfungaji bora wa ligi hiyo, Juma Mohd Juma wa Chuoni akiondoka na Sh milioni 1 na kikombe.
Mchezaji bora wa Grand Malt premier League ni Abdullah Juma wa Jamhuri ya Pemba aliyekabidhiwa Sh milioni 1 taslimu pamoja na kikombe.
Mbali na hilo Grand Malt pia ilizikumbuka timu za madaraja mengine ambayo mshindi wa kwanza na wa pili katika Ligi Daraja la Kwanza ambazo ni Miembeni na Polisi zilikabidhiwa seti ya jezi na vikombe.
Zawadi hizo pia zilitolewa kwa mshindi wa kwanza na wapili wa Ligi Daraja la Pili ambazo ni Kimbunga na Bweleo.
Jioni kulikuwa na hafla maalumu iliyofanyika katika hoteli ya Zanzibar Ocean View, ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Waziri Uvuvi na Mifugo, Abdillahi Hassan Jihad, huku burudani ikitolewa na kundi la Mafunzo Taarab.
Kama ilivyokuwa kwa Waziri Machano alivyosifia udhamini wa Grand Malt, ndivyo pia Waziri Jihad alivyoshukuru kwa kinywaji hicho kuidhamini Ligi Kuu ya Zanzibar.
Waziri Jihad ambaye wakati akiwa anasimamia wizara ya michezo alihusika na mchakato mzima wa kupata wadhamini wa ligi hiyo, aliishukuru Grand Malt na kusema imesaidia kwa kiwango kikubwa kuinua soka la Zanzibar.
“Nilianza mchakato wa kupata wadhamini wa ligi na leo ninashukuru kwamba tumefikia malengo yetu na ninaamini tutazidi kusonga mbele,” alisema.
Akizungumza kuhusu ligi hiyo, Meneja Masoko wa Grand Malt, Fimbo Butallah alisema, wao wamefurahishwa kwa kiasi kikubwa na udhamini wa kinywaji chao kwani kwa kiasi kikubwa imesaidia kukuza soka la Zanzibar.
“Tunataka kuhakikisha tunalikuza soka la Zanzibar na kufika mbali zaidi, hivyo Grand Malt itaendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na ZFA (Chama cha Soka Zanzibar), katika kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa.
“Ila tumekutana na changamoto nyingi mno ikiwa pamoja na mashabiki kutopenda kujitokeza kwa wingi uwanjani, lakini kwa jambo hili tutaendelea kushirikiana na ZFA kuhakikisha tunaukuza mchezo huu,” alisema Butallah,
Meneja huyo alisema, wanachokifanya kwa sasa ni kujaribu kuikutanisha KMKM walio mabingwa wa Ligi Kuu ya Zanzibar kwa kukwaana na Yanga, walio mabingwa wa Tanzania Bara.
“Hatujafikia mahali pa kusema mchezo huo utafanyika lini, lakini mazungumzo yanaendelea na naamini KMKM watathibitishia Watanzania kuwa Ligi Kuu ya Grand Malt ni bora zaidi.”
Kaimu Rais wa ZFA, Haji Amir Haji naye aliishukuru Grand Malt kwa udhamini wake huo na kusema, imesaidia kwa kiwango kikubwa katika kukuza soka la Zanzibar.
“Nataka niwaambie mapema KMKM na Chuoni kwamba wao ndio wawakilishi wa Zanzibar katika mashindano ya Afrika, hivyo tunataka zijiandae mapema ili ziweze kufanya vema katika michuano hiyo,” alisema.
Meneja wa Grand Malt, Consolata Adam naye alisema anashukuru mno kwa kinywaji hicho kuwa sehemu ya mafanikio ya soka Zanzibar, kwani msimu wa 2012/2013 umemalizika salama bila kuwepo kwa vurugu za aina yoyote ile.
“Tunashukuru msimu wa kwanza wa Ligi Kuu ya Grand Malt umemalizika salama kabisa bila kuwepo na vurugu za aina yoyote ile, hii changamoto ya mashabiki tutaifanyia kazi na ninawaomba watu wa Zanzibar wazipende timu zao na kuzishabikia,” alisema.
Akizungumza kwa niaba ya timu zilizoshiriki ligi hiyo, Afisa Michezo wa Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo (KMKM), Ramadhan Hassan ‘Mabio’ naye aliishukuru Grand Malt na kusema imeitoa kimasomaso Ligi Kuu ya Zanzibar.
“Kwa muda mrefu kulikuwa hakuna wadhamini, sisi tunasema wazi hatutaiangusha Grand Malt na katika misimu mitatu yote tunaahidi tutaendelea kulitwaa kombe hili,” alisema.
Ligi Kuu ya Zanzibar kwa sasa inadhaminiwa na kinywaji cha Grand Malt, ambayo imekubali kuidhamini ligi hiyo kwa misimu mitatu mfululizo, huku ikisema itahakikisha inazidi kuibioresha.
Kwa muda mrefu Ligi Kuu ya Zanzibar ilikosa msisimko kutokana na kukosekana mdhamini, hadi Grand Malt ilipoamua kuibeba.
0 comments:
Post a Comment