Kwa ufupi
Kiemba alifunga bao lake kwa shuti la umbali wa mita 25 katika dakika ya 14, ambapo Shooting walisawazisha bao hilo katika dakika ya 52 kupitia Abdulrahman Musa kabla ya Kiemba kutengeneza bao la tatu lililofungwa na Rashid Mkoko katika dakika ya 89, wakati Christopher Edward alipachika bao la pili la Simba akimalizia mpira uliotemwa na kipa Benjamani Haule katika dakika ya 87.
KIUNGO Amri Kiemba alifunga bao moja na kutengeneza moja wakati
Simba ilipoisambaratisha Ruvu Shooting kwa mabao 3-1 jana kwenye Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam katika harakati zake za kusaka nafasi ya tatu.
Kiemba alifunga bao lake kwa shuti la umbali wa mita 25 katika dakika ya 14, ambapo Shooting walisawazisha bao hilo katika dakika ya 52 kupitia Abdulrahman Musa kabla ya Kiemba kutengeneza bao la tatu lililofungwa na Rashid Mkoko katika dakika ya 89, wakati Christopher Edward alipachika bao la pili la Simba akimalizia mpira uliotemwa na kipa Benjamani Haule katika dakika ya 87.
Kwa matokeo hayo Simba imepanda hadi nafasi ya tatu ikiwa na pointi 42 na kuiacha Kagera Sugar katika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo.
Kocha wa Simba, Patrick Liewig akizungumza baada ya mechi hiyo aliwasifu wachezaji wake kwa kucheza vizuri na kufanikiwa kupata matokeo hayo mazuri.
“Vijana wangu wanafuata maelekezo yangu vizuri, nadhani hiyo ndiyo siri ya mafanikio yetu kwa sasa,” alisema Liewig.
Ruvu Shooting waliianza mechi ya jana kwa kasi na kufika langoni kwa Simba katika dakika ya saba baada ya shuti la Musa kutoka sentimita chake katika lango la Simba.
Simba walijibu mapigo katika dakika ya 14 na kufanikiwa kupata bao la kuongoza lililofungwa na Kiemba kwa shuti la umbali wa mita 25, akimalizia vizuri pasi ya Felix Sunzu aliyempokonya mpira beki wa Shooting, Shaaban Suzan.
Kama hiyo haitoshi, Sunzu nusura aipatie Simba bao baada ya kuunganisha kwa kichwa krosi ya Kiemba na kugongesha mwamba katika dakika ya 21.
Katika mechi hiyo kipa wa Shooting, Benjamin Haule alifanya kazi ya ziada kuokoa shuti la Haruna Chanongo katika dakika ya 34.
Pia beki Said Madega wa Shooting alionyeshwa kadi ya njano kwa kumchezea vibaya Chanongo katika dakika ya 45.
Simba katika mechi hiyo walitumia zaidi winga zao mbili zinazoongozwa na Chanongo na Ramadhan Singano kupitisha krosi za juu kwa Sunzu, wakati Shooting wenyewe walicheza pasi fupifupi kwa kasi, lakini walikosa umakini kwenye umaliziaji.
Kurejea kwa Sunzu kunazidi kuimarisha safu ya ushambuliaji ya Simba kabla ya mchezo wao wa mwisho wa msimu huu dhidi ya mahasimu wao Yanga hapo Mei 18.
0 comments:
Post a Comment