BAJETI YAKE YABANA HUDUMA ZA UZAZI WA MPANGO, FEDHA ZA VIBURUDISHO CHAI, VITAFUNWA ZATENGWA.http://www.mtanzania.co.tz
WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii imeshutumiwa kwa kushindwa kutenga fungu katika bajeti yake ya mwaka huu wa fedha 2013/ 2014 kwa ajili ya huduma za uzazi wa mpango. Watendaji wa wizara hiyo wanadaiwa kupuuza ahadi ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa Julai 11, 2012 katika mkutano uliohusu uzazi wa mpango uliofanyika London, Uingereza.Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam juzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Uhamasishaji wa Afya Tanzania (HDT), Dk. Peter Bujari alisema bajeti ya wizara hiyo ina upungufu mkubwa.
Dk. Bujari alisema katika bajeti ya mwaka huu, wizara hiyo imeomba kuidhinishiwa Sh bilioni 753.86, lakini hakuna fedha zilizotengwa kwa ajili ya huduma za uzazi wa mpango.
Alisema inashangaza kuona bajeti hiyo imezi
ngatia vitu vya anasa zaidi na kusahau huduma muhimu kama hiyo kwa ajili ya uzazi wa mpango kwa afya bora ya mama na mtoto.
“Suala la kujiuliza ni kwamba inawezekanaje Rais akaahidi kuwa fedha zitaongezwa kisha watekelezaji wakakaidi kutenga bajeti?
“Uchunguzi wa rasimu ya bajeti ya mwaka 2013/2014 ya Wizara ya Afya hauonyeshi ni kiasi gani ambacho wizara inategemea kutenga kwa ajili ya huduma hizi.
“Lakini utashangaa katika bajeti hiyo viburudisho vimetengewa fungu, posho zipo, usafiri, chai na takataka nyingine vimetengewa fedha, lakini fedha kwa ajili ya huduma hizi hakuna,” alisema.
Katika mkutano wa London, Rais Kikwete alisema kuwa Tanzania itaongeza matumizi ya huduma za uzazi wa mpango maradufu kutoka asilimia 34 hadi kufikia asilimia 60 ifikapo mwaka 2015.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi anatarajiwa kuwasilisha bungeni keshokutwa, randama ya makadirio ya bajeti yake kwa mwaka 2013/ 14.
Dk. Bujari alisema ili kutimiza ahadi hiyo, shirika lake linapendekeza Serikali itenge angalau Sh bilioni 15 ambayo ni asilimia 75 ya mahitaji yaliyoombwa na Kitengo cha Afya ya Mama na Mtoto (RCHS).
“Ni mategemeo yetu kuwa bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii itakayosomwa tarehe 8 na 9 Mei, 2013 itazingatia mapendekezo haya ili kuwasaidia akina mama na watoto,” alisema.
Dk. Bujari alisema kwa mtindo huo ni vigumu Tanzania kutimiza malengo ya mileni ambapo lengo la kwanza ni kupunguza vifo vya akina mama kwa asilimia 32.
Lengo la pili ni kupunguza ni kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano kwa asilimia 10, wakati lengo la sita ni kupunguza umasikini uliokithiri kwa familia kuwa na watoto wasioweza kuwahudumia.
Dk. Bujari alisema ili kutimiza ahadi ya Rais Kikwete ya kuongeza mara mbili idadi ya wanaotumia uzazi wa mpango ifikapo 2015, Sh bilioni 147.3 zinahitajika.
0 comments:
Post a Comment