HAPA JOSEPH MSOFE AKILANDA MBAO WAKATI AKITENEZA MLANGO WA NYUMBA KATIKA ENEO LA KALAKANA YAKE ILIYOPO MTAA WA MINDU MANISPAA YA MOROGORO. PHOTO/ MTANDA BLOG.
FUNDI seremala mkazi wa Manispaa ya Morogoro, Joseph Msoffe ameibuka mshindi wa gari jipya aina ya Tata Safari lenye thamani ya Sh70 milioni kwenye droo ya mwisho ya promosheni ya Chomoka na Mwananchi iliyochezeshwa Makao Makuu ya Ofisi za Mwananchi, Tabata Relini jijini Dar es Salaam, jana.
Mshindi huyo aliibuka katika droo hiyo
iliyosimamiwa na Bodi ya Taifa ya Michezo ya Kubahatisha, baada ya
kupigiwa simu kujulishwa kuwa ameshinda alilipuka kwa furaha na kueleza
kuwa haamini.
“Tunapenda kukufahamisha kuwa wewe ndiye mshindi
wetu wa zawadi ya gari jipya aina ya Tata Safari katika droo ya
promosheni ya Chomoka na Mwananchi,” alisema Meneja Masoko wa Mwananchi
Communications Ltd (MCL), Bernard Mukasa.
MCL ndiyo wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi, Mwanaspoti na The Citizen.
Msoffe alisema haamini kwani katika maisha yake hajawahi kushinda bahati nasibu yoyote.
“Sijawahi kushinda bahati nasibu yoyote katika maisha yangu, nipo naungua na jua... hivi sasa napiga randa,” alisema.
Fundi seremala huyo alitoa sauti ya mshangao na
kuamsha kicheko baada ya meneja masoko huyo kumweleza kuwa, gari
aliloshinda lina thamani ya Sh70 milioni.
Alisema ana furaha isiyo kifani na haamini kama ni kweli.
Awali, akizungumza baada ya droo hiyo, Ofisa
Mtendaji Mkuu wa MCL, Francis Nanai alisema droo hiyo ambayo ilianza
Agosti mwaka huu ni ya aina yake nchini na Afrika Mashariki na kwamba,
ililenga kutoa shukrani kwa wasomaji wa Mwananchi.
“Mwakani wasomaji wetu watarajie ubunifu mwingine mkubwa zaidi na wa kipekee,” alisema na kuongeza.
“Zaidi ya Sh250 milioni zilitumika kwa ajili ya
zawadi za magari na Sh1 milioni zilizokuwa zinatolewa kila siku kwa siku
100 za promosheni.”.
Gari hilo ni la tatu kutolewa na Mwananchi katika
droo hiyo ya Promosheni ya Chomoka na Mwananchi, mshindi wa gari jipya
la kwanza aina ya Tata Vista alikuwa ni Benedict Ngoo, mfanyakazi wa
Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkoa wa Dodoma. MWANANCHI.
0 comments:
Post a Comment