NCHINI Afrika Kusini, hakuna eneo la kivutio cha kitalii
linalotembelewa na wageni wengi kama Kisiwa cha Robben. Umaarufu wa eneo
hili umekuwa ukiongezeka mwaka mpaka mwaka.
Lakini hakuna shaka kwamba, kiini cha kutembelewa
sana kwa kisiwa hiki ni kutoka na kuwa kituo maalumu cha kuwafunga
wapigania uhuru wa Afrika Kusini wakati huo, akiwamo Nelson Mandela.
Mandela, Rais wa kwanza Mwafrika nchini Afrika
Kusini, ndiye mhimili wa kivutio cha utalii kwenye jela ya wafungwa wa
kisiasa iliyojengwa ndani ya kisiwa hicho.
Kati ya wafungwa wengi wa kisiasa waliowahi
kufungwa kwenye jela ya Robben, alikuwamo Govan Mbeki, baba mzazi wa
Rais wa zamani wa Afrika Kusini aliyempokea madaraka Mandela, Thabo
Mbeki. Ni Mandela pekee ndiye aliyekaa hapo muda mrefu.
Mpiganaji Mandela aliyehukumiwa kifungo cha maisha
jela, alitumia miaka 17 kwenye jela hiyo kati ya miaka 28 aliyosota
kabla ya kuachiwa huru mwaka 1990.
Kufariki kwa Mandela wiki iliyopita, kumechochea
kwa kiasi kikubwa kuongezeka umaarufu wa Kisiwa cha Robben
kinachoendelea kuwa na historia ya pekee kwa aina yake duniani.
Jela ya kisiwa hiki, pia aliwahi kufungwa mwasisi
wa Chama cha Pan Africanist Congress (PAC), Robert Mangaliso Sobukwe na
mwanaharakati mwingine wa ANC, Walter Sisulu.
Mwanaharakati mwingine aliyekuwa akipinga ubaguzi
wa rangi wakati huo, Jeff Masemola ameweka historia kwa kuwa mfungwa wa
kwanza kuhuhumiwa kwenda jela maisha.
Mbali na kufungwa Jela ya Robben, Mandela pia
alitumikia kifungo kwenye Magereza ya Pollsmoor (1982–1988) na Victor
Verster (1988–1990) kabla ya kuachiwa huru pamoja na wafungwa wengine.
Rais wa mwisho mzungu Afrika Kusini, F. W. de Klerk ndiye aliyemtoa Mandera katika Gereza la Victor Verster.
Umaarufu wa Robben Island hauishii hapo tu, kwani
kisiwa hicho ni kitovu cha makazi ya ndege aina mbalimbali zaidi ya 100,
wakiwemo ndege aina ya Penguin wa Afrika wanaofikia idadi ya 140,000.
Kisiwa hiki chenye historia ndefu tangu wakoloni
wa Uholanzi walipoingia kwa mara ya kwanza katikati ya miaka 1600, kiko
umbali wa kilomita 6.9 kutoka Bloubergstrand, Cape Town. MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment