LICHA ya kuwa ni siku ya huzuni kwa dunia nzima, hotuba ya Rais
wa Marekani, Barack Obama imewagusa maelfu ya watu waliokuwa kwenye
Uwanja wa FNB katika ibada ya kitaifa kumwaga Rais wa zamani wa Afrika
Kusini, Nelson Mandela.
Obama aliyetumia dakika 20 katika hotuba yake
iliyokuwa ikikatizwa na kelele za kumshangilia, aliwataka vijana wa
Afrika na dunia nzima kuiga maisha aliyoishi Mandela kama yeye
alivyojifunza mambo mengi kutoka kwa mzalendo huyo.
“Miaka 30 iliyopita nikiwa mwanafunzi, nilisoma
Kitabu cha Mandela na tangu siku hiyo nilijifunza, nikajenga roho ya
uthabiti. Iliamsha uwajibikaji kwa ajili yangu na kwa ajili ya watu
wangu... hakika Mandela amenifanya niwe hivi nilivyo leo. Michelle na
mimi tumenufaika sana na Mandela,” alisema Obama na kuongeza:
“Mandela alinifanya niwe mtu ninayesimama mbele
yenu leo, alichangia kunifanya kuwa kiongozi bora. Nitaendelea kuiga
mfano wake,”
Katika sherehe hizo, Obama alipokewa kwa shangwe
na kushangiliwa kila alipopita na kila alipozungumza tofauti na
ilivyokuwa kwa Rais wa nchi hiyo, Jacob Zuma ambaye alikuwa akizomewa.
Obama alimtaja Mandela kama kiongozi anayefaa
kuigwa kwani pamoja na kukaa gerezani kwa miaka 27 akipigania uhuru,
hakutaka kung’ang’ania madaraka na badala yake alistaafu kwa hiari yake,
tofauti na viongozi wengi wa Afrika.
“Mandela alionyesha uongozi wa vitendo na
kujaribu, alikuwa ni mwanamume, binadamu wa kawaida, mume, baba na
kiongozi shupavu,” alisema Obama.
Pia Obama alisema, Mandela aliachiwa huru kama
mfungwa, lakini kama mwalimu ambaye alitumika kutuonyesha kuwa, ni
lazima kuwaamini wenzako ili nao wakuamini.
“Kufundisha upatanisho, hakuhitaji kudharau
historia mbaya ya nyuma bali ni kuikabili kwa umakini, ukweli na
uhalisia wake. Mandela alibadili sheria, lakini alibadili mioyo yetu
pia,” alisema.
Katika risala hiyo, Obama alimtaja Mandela kama
mwanamapinduzi mkubwa wa karne ya 20 aliyeibadilisha mioyo ya watu wake,
akaimarisha mapatano na maelewano kwa wazungu na weusi.
“Amezaliwa kipindi cha Vita Kuu ya Kwanza ya
Dunia, kijana aliyekuwa akichunga ng’ombe na kuteswa na wakubwa zake wa
kikabila, lakini ameibuka na kuwa mwanamapinduzi mkuu wa karne ya 20,”
alisema Obama.
Vilevile, Obama alimfananisha Mandela na Abraham
Lincoln, Rais wa zamani wa Marekani kwa kuiunganisha nchi yake pale
ilipokuwa inataka kuvurugika. MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment