BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

UKIMYA WATAWALA WAKATI JENEZA LENYE MWILI WA TATA MADIBA LIKIKABIDHIWA KUTOKA MIKONO YA SERIKALI KWENDA KWA VIONGOZI WA KIMILA KABILA LA abaTHEMBU JIMBO LA EASTERN CAPE AFRIKA YA KUSINI TAYATI KWA MAZISHI.

Maofisa wa Jeshi la Afrika Kusini wakipiga saluti baada ya kushusha kaburini mwili wa Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela katika ibada ya mazishi iliyofanyika Qunu, jana.Picha na AFP  


QUNU: 
YAMETIMIA, Saa 6:45 kwa saa za Afrika Kusini (sawa na saa 7:45 za Afrika Mashariki) ni muda ambao pengine hautasahaulika katika historia ya nchi hiyo, kwani wananchi wake walishuhudia ukomo wa maisha ya Rais wao wa kwanza mzalendo, Mzee Nelson Mandela.


Ukimya ulitawala katika makaburi ya familia ya Mandela, Qunu, katika Jimbo la Eastern Cape, wakati mwili wa Mandela ukiwa umewekwa ndani ya jeneza lililotengenezwa kwa mbao na kwa ustadi mkubwa lilipokabidhiwa kwa viongozi wa mila za Kabila la abaThembu kwa ajili mazishi.

Mwili huo ulishushwa kaburini katika tukio la mazishi ambalo halikuwa wazi kwa waombolezaji wengine, isipokuwa kwa familia ya Mzee Mandela, Rais Jacob Zuma na viongozi wa kimila katika jamii hiyo ya Waxosa ambako Mandela anatoka. Hata hivyo, mazishi hayo yalionyeshwa moja kwa moja na Kituo cha Televisheni ya SABC.

Kwa mujibu wa mila na desturi za kabila hilo alipaswa kuzikwa mchana wakati jua likiwa utosini, muda ambao kama angekuwa hai, kivuli chake kingekuwa kifupi kuliko muda mwingine.

Mwili wa Mandela ulikabidhiwa kwa viongozi wa kimila na Majenerali wa Jeshi la Afrika Kusini (SANDF) baada ya kumpa kiongozi huyo heshima kubwa, sawa na ile ambayo hupewa kiongozi ambaye hufariki akiwa madarakani.

Kabla ya kukabidhi mwili huo, waliondoa bendera ya Taifa ya Afrika Kusini ambayo ilikuwa imefunika jeneza pamoja na vifaa vingine, ili kutoa mwanya kwa jeneza hilo kufunikwa kwa ngozi ya chui kama mila zinavyotaka.

Bendera na vifaa vilivyoondolewa vilikabidhiwa kwa familia ya Mandela.

Ni watu 450 tu kati ya zaidi ya 5,000 walioshiriki katika ibada ya mazishi, ambao walipata kibali cha kwenda makaburini na majina yao yalisomwa mmoja baada ya mwingine.

Mara baada ya mwili wa Mandela kukabidhiwa, Askofu Don Dabula, alifanya sala ya mwisho na alipohitimisha anga la Qunu lilishamiri sauti za helikopta tatu za kijeshi ambazo zilikuwa zimening’iniza bendera za Afrika Kusini.

Helikopta hizo zilifuatiwa na ndege nyingine sita ambazo zilikuwa zimerushwa zikitengeneza umbo la pembe tatu, matukio ambayo yalifanywa kwa heshima ya kiongozi huyo.

Kulikuwa na ukimya na wakati ndege hizo zikitokomea, baragumu lilipigwa wakati ambao mazishi rasmi ya Mandela yalikuwa ya kianza kwa taratibu za kimila.

Mapema Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma alisema wiki iliyopita imekuwa ni wiki ya uchungu, kwani kwa siku tisa za maombolezo watu wameomboleza kwa ukimya, vilio na nyimbo ikionyesha kuwa walifurahishwa na kumpenda Mzee Mandela. MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: