WANAKIJIJI WA QUNU WAILALAMIKIA SERIKALI YA ZUMA KWA KUWANYIMA HAKI YA KUMZIKA MZEE NELSON MANDELA.
WAKAZI wa kijiji cha Qunu ambako kiongozi wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela anatarajia kuzikwa kesho, wameelezea masikitiko yao dhidi ya taarifa kuwa hawatahudhuria maziko hayo. “Inauma sana kukosa kuhudhuria maziko hayo,” alisema Simesihle Soyaye juzi.
“Sisi ni watu wa hapa, mahali ambako alikulia, tulikuwa tukiishi naye,” aliongeza.
Alisema kuangalia tu shughuli za maziko kupitia televisheni ni jambo litakaloumiza sana wenyeji wa kijiji hicho. Bibi yake, Nomvula, alisema maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kuangalia shughuli hiyo yako mbali hasa kwa wazee kuweza kuyafikia.
Akimzungumzia Mandela, alisema atajisikia mnyonge sana akisikia wakazi wa Qunu hawaruhusiwi kuhudhuria maziko hayo. “Yeye alipendelea sote tuwepo. Alipohamia Johannesburg, alitwambia kwamba ingawa ameondoka, tutaweza kumwona tena hata kama amefariki dunia,” alisema Nomvula.
Mwanamke huyo, ambaye anaishi karibu na nyumba ya Mandela, alisema kama hakuna usafiri ulioandaliwa kwa ajili ya watu kwenda maeneo ya kuangalia shughuli hiyo itakavyokuwa ikiendelea, ni afadhali hata abaki akiangalia nyumbani kwake.
Sinazo Mfanase, ambaye anaishi kijijini hapo, alisema ameumia sana kusikia kwamba hataweza kumzika Mandela. Alisema angependa asaidie kufanya chochote katika shughuli hiyo.
“Ningeweza hata kujitolea kufanya usafi, lakini hatukupewa fursa hiyo. Hakika inatuumiza sisi wenyeji wa hapa,” alisema. Juzi na jana kulikuwa na helikopta mbili za kijeshi zikiruka katika anga la nyumba ya Mandela. Kulikuwa pia na polisi wa farasi kijijini hapo. Msafara wa magari ya ving’ora yenye vimulimuli ulionekana ukielekea iliko nyumba hiyo.
Hata hivyo, haikufahamika mara moja nani alikuwa kwenye msafara huo, kwa kuwa vyombo vya habari havikuruhusiwa kuisogelea nyumba hiyo. Mapema asubuhi juzi, zaidi ya mabasi 20 na malori yalijipanga nje ya nyumba ya Mandela huku wanajeshi wakionekana kuranda katika eneo hilo. Wanahabari walizuiwa kupiga picha eneo hilo. Ofisa wa Polisi alisema:
“Tumeambiwa tusiwaruhusu kuingia hapo au kupiga picha. Mnaweza kwenda kwenye lile hema jeupe (akimaanisha kituo cha habari kilichosimikwa kilimani). Jumatano, Waziri wa Ofisi ya Rais, Collins Chabane alisema vyombo vya habari vimekiuka itifaki.
“Tumebaini kwamba baadhi ya wanahabari wamekiuka itifaki na mipango iliyoandaliwa Qunu, na hiyo imesababisha mkanganyiko kwa mamlaka husika na familia ya Mandela na jamii ya Qunu.” Alivitaka vyombo vya habari kuheshimu mahali ambako kutakuwa na mapumziko ya milele ya Mandela.
“Mahali atakapopumzika milele Mandela ni muhimu kimila hasa kwa ukoo wa Wathembu,” alisema Chabane.
Barabara ziliendelea kufanyiwa marekebisho ya hapa na pale huku njia ya N2 ikisafishwa. Katika jumba la makumbusho la Nelson Mandela lililoko Qunu, watoto wamekuwa wakigawiwa peremende, matunda na wanasesere.
Wakati hayo yakitokea Qunu, mtalaka wa Mandela, Winnie, amesema anajihisi mwenye bahati sana kwa kuwa na mume wake huyo wa zamani hadi kifo chake.
Aliiambia televisheni ya ITV ya Uingereza juzi, kwamba kuna hisia kali zinazohusu kufariki dunia kwa mumewe huyo wa zamani, akisema hakuna anayeweza kujiandaa kwa kifo.
“Nilimsogelea na kutambua kuwa alikuwa akipumua kidogo sana … nilijaribu kumgusa ili kujua joto lake nikahisi ubaridi. Ndipo alipopumua pumzi yake ya mwisho na kukata roho …alikuwa ameondoka.”
Winnie alisema familia yake itamkumbuka mumewe huyo wa zamani kutokana na urithi aliouacha na maridhiano aliyoyasimamia na kwa kutokuwa mchoyo katika kujitoa maisha yake “kwa Taifa na dunia”.
Aliongeza: “Ndivyo tutakavyomkumbuka, kwamba hata mara moja hakujifikiria yeye binafsi. Alitoa kila kitu kwa Taifa.” Alisema kwamba kipindi kigumu cha wiki iliyopita kilikuwa ni pale alipoona wanajeshi wanakuja kuondoa mwili nyumbani ndipo alipotambua kuwa “alikuwa anaondoka nyumbani moja kwa moja.”
Pia alielezea uchungu alioupata alipomwona Mandela amelala katika majengo ya Serikali ya Union, akisema: “Ni vigumu sana kwa familia kushiriki naye kifo baada ya kushiriki naye dunia nzima na nchi nzima wakati akiwa hai.”
Mkalimani bandia achunguzwa Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Wizara ya Walemavu Afrika Kusini amesema Serikali inachunguza jinsi mkalimani wa lugha za alama katika ibada ya kitaifa ya kumkumbuka Mandela alivyoruhusiwa na vyombo vya usalama kuwa pale.
Thamsanqa Jantjie, ambaye alisimama sambamba na viongozi wa dunia katika tukio hilo la Jumanne kwenye uwanja wa FNB jijini Johannesburg, amekanusha kufanya udanganyifu na kusema aliingiwa na hofu alipoanza kuona maluweluwe.
Alisema alikuwa na uchizi, ambao zamani ulimfanya awe anachanganyikiwa na kufanya fujo. Shirika lililomwajiri la SA Interpreters, linadaiwa nalo kutoweka.
Naibu Waziri huyo, Hendrietta Bogopane-Zulu alikiri kwamba kukodiwa kwa mkalimani wa lugha ya alama asiye na sifa ni kosa, lakini akakana kauli kuwa serikali itakuwa imefedheheshwa.
Hata hivyo, Waafrika Kusini wengi, watu wenye ulemavu wa kusikia duniani na bila shaka hata kikosi cha usalama cha Rais wa Marekani hakitakubaliana na hilo. Mwajiri wake atoweka Bogopane –Zulu alisema kampuni ya Jantjie ‘imetoweka’ baada ya kutoa huduma duni kwa miaka mingi- wateja wa zamani wa shirika hilo inadaiwa walikuwa ni pamoja na taasisi zingine za serikali na ANC.
Mpaka sasa hakuna mtu au chombo kinachokubali kuikodi SA Interpreters na Jantjie, lakini yeyote anayehusika bila shaka atatakiwa kujieleza.
Kashfa hii kwa kiasi fulani inatia doa maombolezo ya kitaifa ya Mandela. Afrika Kusini inasubiri kupata majibu ya maswali hayo kabla ya maziko yake kesho. Hata hivyo, ANC imesema imekuwa ikimtumia Jantjie kama mkalimani katika matukio mengi, na “haijapata kusikia malalamiko yoyote kuhusu kiwango cha huduma, sifa au ugonjwa wake.”
Lakini ilisema shughuli ya Jumanne iliandaliwa na Serikali, na si ANC, hivyo chama hicho tawala hakiwezi kuzungumzia lolote kuhusu mipango ya usalama iliyokuwapo siku hiyo. Taasisi ya Wakalimani wa Afrika Kusini ilisema mapema kwamba kulipata kuwa na malalamiko dhidi ya kazi ya Jantjie kabla, lakini ANC haikuchukua hatua.
ANC ilisema itafuatilia “mawasiliano yaliyowasilishwa kwetu kuhusu tatizo hilo na kuona kama kuna haja ya kuchukuliwa hatua.”
Siku ya ibada ya kumkumbuka Mandela Jantjie (pia inatamkwa Dyantyi) alisimama jukwaani karibu na wasemaji wakuu akiwamo Rais Barack Obama wa Marekani, Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini na wajukuu wa Mandela huku yeye akitafsiri hotuba zao kwa ajili ya wasiosikia.
Vitendo vya Jantjie vilishuhudiwa na mamilioni ya watu duniani kote na viliiudhi jamii ya wasiosikia wa Afrika Kusini.
Shinikizo limeongezeka dhidi ya Serikali itoe maelezo ya kwa nini alikodiwa katika tukio muhimu kama hilo. Bogopane-Zulu aliwaambia waandishi wa habari juzi, kwamba:
“Kwanza, sidhani kama Afrika Kusini kama nchi ingeweza kuweka hatarini usalama wa mtu yeyote, hususan wakuu wa nchi.
“Pili, mtu yeyote anapotoa huduma ya ukalimani wa lugha ya alama, sidhani … mtu yeyote anaweza kuuliza: “Kichwa chako kizuri? Una matatizo yoyote ya akili? Nadhani suala lilikuwa ni juu ya: “Unaweza kutafsiri kwa alama? Unaweza kutoa huduma?’” Lakini akasema:
“Kwa masuala ya usalama, hayo yamo kwenye mchakato, tunahitaji kujua nani alimpitisha kufanya kazi hiyo.” Bogopane-Zulu aliomba radhi kwa jamii ya wasiosikia, lakini akasema hakuna sababu ya nchi kufedheheka. “Kuna lahaja takriban 100 za lugha ya alama,” alisema, akielezea kuwa Jantjie anazungumza Kixhosa na kwamba “Kiingereza kilikuwa kigumu kwake.”
Pia aliwashutumu waajiri wa Jantjie kwa kuwa ‘waongo’ na kusema wakurugenzi wa SA Interpreters tangu hapo wametoweka.
Naibu Waziri alisema kampuni hiyo imekuwa kwa muda mrefu ikitoa huduma duni. Akiri uchizi Jantjie aliiambia AP kwamba mara kwa mara siku za nyuma alikuwa akijikuta anafanya fujo, alikuwa akitarajiwa kufanyiwa vipimo siku ya ibada ya kumbukumbu, kuangalia kama alikuwa akihitaji kulazwa hospitali.
Aliiambia hata BBC siku ya tukio, kwamba alipata matatizo wakati akitafsiri na kuanza kuona njozi kuwa malaika walikuwa wakishukia umati wa watu waliokusanyika uwanjani hapo siku hiyo.
“Ndipo nilipoanza kutambua kuwa siko katika hali ya kawaida, kwa sababu ni kitu ambacho hakiwezekani. Lakini niamini niliwaona wakija jukwaani. Kuanzia hapo, sikuwa mimi,” alisema, akiongeza kuwa alianza kuwa na wasiwasi na usalama wa watu uwanjani hapo na bila shaka alijua hakuwa anatoa ishara vema. Kikosi cha Usalama cha Marekani kilisema “kilikubaliana na hatua za kiusalama” kwamba zilikuwa sawa kwa Rais Obama kujitokeza pale na kwamba wanausalama wa Marekani “mara zote walikuwa karibu naye” kokote alikokwenda.
Msemaji Brian Leary alisema lilikuwa ni jukumu la Afrika Kusini kufuatilia historia ya watu waliohusika na shughuli hiyo.
“Zaidi ya hapo hatuwezi kuzungumza lolote juu ya uamuzi uliochukuliwa kati ya kikosi chetu cha usalama na mamlaka za Afrika Kusini,” alisema.
Mwili wasafirishwa Katika hatua nyingine, mwili wa Mandela ulisafirishwa jana kutoka Pretoria kwenda Eastern Cape kutoka uwanja wa ndege wa kijeshi wa Waterkloof.
Gwaride la kijeshi liliupokea mwili huo na jeneza kuwekwa kwenye gari maalumu lenye mitutu na kupelekwa kwenye gari lingine la kupeleka mwili mazikoni.
Kisha mwili huo ulipelekwa kijijini kwake Qunu, ambako jamii ya Wathembu waliendesha sherehe za kimila tayari kuzikwa rasmi kesho. Siku ya Taifa ya Maridhiano itaadhimishwa Desemba 16 ambapo mnara wa Mandela utazinduliwa katika majengo ya Union, Pretoria. HABARILEO.
0 comments:
Post a Comment