WAZIRI Mkuu wa zamani wa Tanzania, Frederick Sumaye amewataka
wananchi na wadau wa demokrasia kutochoka kukemea rushwa katika kupata
viongozi kwani inawafanya kuwa wapofu na kudumaza maendeleo.
Aliyasema hayo wakati akishiriki harambee ya kuchangia ujenzi wa
ukumbi wa parokia ya Mawella, Jimbo Katoliki la Moshi, mkoani
Kilimanjaro.
“Ndugu Paroko, naomba usichoke kukemea rushwa na ufisadi na maovu
mengine yote yaliyokatazwa katika Biblia Takatifu maana huo ni wajibu
wako kama ulivyo wajibu wangu na wajibu wa kiongozi yeyote mwingine ...”
alisema Sumaye.
Alisema anashangazwa na kauli za sasa ambazo zinaonesha dhahiri
kwamba baadhi ya maeneo na hata katika baadhi ya makundi kuna mwenendo
unaonesha kujipanga kwa wanaowania uongozi kwa staili ya matumizi ya
fedha.
“Fadhila zimeanza kuwa nyingi katika baadhi ya sehemu na kwa baadhi
ya nafasi hasa nafasi za juu; na wapiga kura tayari wameanza kupigwa
mnada na kupangiwa bei kulingana na uhodari au umuhimu wa nafasi
aliyonayo mhusika,” alisema Sumaye na kuongeza kuwa mambo hayo machafu
hayatakiwi kufumbiwa macho.
Alisema kwamba vita dhidi ya rushwa katika uongozi ni kali na
Watanzania wasipoangalia sauti za wanaopigana inaweza ikafifishwa na
kelele za wanaonufaika na rushwa hizi za nyakati za uchaguzi.
Sumaye alisema pamoja na watu kukerwa na hotuba zake za kukumbusha
umuhimu wa demokrasia kutobanwa na fedha, hazungumzi hivyo kwa kuwa
anataka uongozi mwaka 2015, lakini anasema hivyo kwa kuwa ni jukumu lake
na la Watanzania wote kupambana na rushwa kwani hata kwenye vitabu
vitakatifu imeelezwa dhahiri kuwa rushwa hupotosha viongozi.
Akinukuu kifungu cha Biblia, alisema: “Biblia katika Kutoka 23:8
inasema, “Nawe usipokee rushwa; kwani hiyo rushwa huwapofusha macho hao
waonao, na kuyapotoa maneno ya wenye haki.”Hivi hao wanaotakiwa kuona ni
wakina nani? Hao bila shaka ni viongozi wetu kwa sababu kuongoza ni
kuonyesha njia.
Kama sote tunaamini Biblia Takatifu na inasema rushwa hupofusha macho
hao waonao na wewe na mimi tukamchagua kiongozi mla rushwa, au mtoa
rushwa au anayewanunua wapiga kura, hivi huyo kweli atatuongoza tukafike
tunakotaka kufika?”
Aliongeza kusema; “Ukikemea tu rushwa basi utapachikwa sababu nyingi
zisizohusika ikiwemo ya kugombea urais mwaka 2015.
Nasema katika hili,
suala la kugombea au kutogombea urais mwaka 2015 si sababu. Vita yangu
dhidi ya rushwa siyo ya leo. Rekodi zangu zinaonesha nimepambana na
rushwa wakati wote nikiwa madarakani, nilipotoka madarakani na sasa
naendelea na vita hii na sitachoka.“
Katika kuelezea ubaya wa rushwa, Sumaye alitoa mfano wa kejeli
inayotupwa kwake na kundi moja la wanasiasa kwamba hafai kushika
madaraka kwa kuwa ni masikini.
“Kuna jamaa moja, kiongozi mwanasiasa aliwakuta watu wapenzi wangu
wananizungumza tu akawaambia huyo Sumaye ni maskini atawapa nini?
Jiungeni na kambi ya fulani atawapeni fedha nyingi na shida zenu
zitaisha. “
Alisema ingawa umasikini si sifa ya kuwa rais, rushwa si mbadala
wake. “Kama tunafika sasa kwenye utaratibu wa kusifiana kwa viwango vya
rushwa vinavyotolewa na tunavyopokea, tunaipeleka nchi pabaya,“ alisema
Sumaye na kuongeza kuwa yeye hajawahi kutangaza kugombea urais ingawa
yeye si masikini ila hawezi kukana ukweli kuwa hana fedha za kuwanunua
wapiga kura wala utaratibu wa kuwanunua hautaki kwa maana ni rushwa.
Aidha alisema pamoja na kejeli hizo, anaona cha muhimu watu hao ambao
wanaibia taifa kwa ufisadi ni vyema wakishaiba wasiseme, kwani
Watanzania hawafurahishwi na hali hiyo, inawaudhi na inawauma na ipo
siku wataikataa.
Sumaye alisisitiza kuwa utaratibu wa kuwekwa au kuchaguliwa katika
nafasi bila vishawishi vya rushwa uliotumika tangu enzi za kale ndiyo
unaotakiwa kutumika hadi leo, labda kwa kuboreshwa kutegemeana na
mazingira lakini siyo kudhoofishwa au kuchakachuliwa kwa rushwa.
Waziri huyo akizungumza kwa umakini alisema kuwa kama taifa litakiuka
taratibu sahihi za kuwapata viongozi na badala yake wapiga kura
wakanunuliwa kwa kupewa rushwa, basi wajue na wakubali kuwa watapatikana
viongozi waliopofuliwa na ama utoaji au upokeaji wa rushwa.
Aliwataka Watanzania kuungana na Rais Jakaya Kikwete katika juhudi
anazofanya za kupambana na uozo wa rushwa katika jamii yetu, hasa rushwa
nyakati za chaguzi.
Licha ya kuelezwa kuna kampeni za chini kwa chini kwa watu wanaotaka
madaraka katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, taifa pia linajiandaa kwa
uchaguzi wa Serikali utakaofanyika mwaka kesho, yaani mwaka 2014.
Katika harambee hiyo, jumla ya milioni 83 zilipatikana kwa ajili ya ujenzi wa ukumbi huo wa Parokia.HABARILEO
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / Uncategories / WAZIRI MKUU AKERWA NA KASI YA RUSHWA, RUSHWA SASA HIVI IMEKUWA IKIPIGIWA MNADA KUPATA VIONGOZI WA NGAZI ZA JUU.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment