BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

JWTZ LAAHIDI KUZIDISHA UCHAPAJIKAZI.



JESHI la Wananchi Tanzania (JWTZ) limeahidi kuzidisha nidhamu, uzalendo, weledi na uchapakazi katika kipindi cha mwaka huu mpya kwa lengo la kukuza misingi na uwajibikaji inayoliongoza jeshi hilo katika utekelezaji wa majukumu yake mbalimbali ya ulinzi na usalama wa Taifa.

Ahadi hiyo ilitolewa juzi na Mkuu wa Kamandi ya vikosi chini ya Makao Makuu ya Jeshi hilo, Meja Jenerali Hassan Vuai Chema wakati akitoa salamu zake za Mwaka mpya kwa maofisa na askari mbalimbali wa Kamandi ya anga, hafla iliyoandaliwa na kamandi hiyo kwa lengo la kuuaga mwaka 2013 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2014.

Katika salamu zake hizo, Meja Jenerali Chema pia alisema jeshi hilo lipo katika mikakati ya kuendelea kujiimarisha katika upande wa wataalamu mbalimbali hususani katika maeneo ya teknolojia huku akiwataka maofisa pamoja na askari wake wote kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao ipasavyo.

“Nidhamu na uzalendo pamoja na uadilifu ndiyo silaha kubwa ndani ya jeshi letu, ndani ya mwaka huu mpya,tunapaswa kuimarisha uhusiano uliopo kati yetu na raia kwa kuhakikisha tunakuwa karibu yao zaidi na hii ndiyo misingi ya uwajibikaji ninayoamini itaendeleza weledi tulionao katika kulitumikia Taifa” alisema Meja Jenerali Chema.

Aidha, alisema taarifa za kipolisi ndani ya jeshi hilo zinaonesha kupungua kwa matukio ya uhalifu huku akisisitiza kuwa vikosi vyote vya jeshi hilo vipo salama na kwamba hakuna tishio lolote linalohatarisha amani huku pia akiwataka wanajeshi hilo kujilinda dhidi ya gonjwa hatari la Ukimwi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kamandi ya anga ya JWTZ, Meja Jenerali Joseph Kapwani, aliwataka askari na maofisa kujiendeleza kielimu ili kulifanya jeshi hilo kuwa na weledi zaidi ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko mbalimbali ya sayansi na teknolojia.

Aidha alisema katika kukabiliana na suala hilo pia jeshi hilo lipo katika mikakati ya kuwasomesha askari wake ndani na nje ya nchi huku akitoa rai kwa wanawake kujitokeza kwa wingi na kujiunga na jeshi hilo hususani katika fani za urubani na ufundi wa ndege za kijeshi.

Alisema kamandi hiyo kama ilivyo kwa kamandi zingine za kijeshi inajivunia mafanikio na utendaji mzuri wa kazi pamoja na nidhamu safi kutoka kwa maofisa na askari wake ikiwemo ya ushiriki wao katika majukumu ya kitaifa zikiwemo operesheni mbalimbali. HABARILEO.

Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: