SPIKA wa Bunge, Anne Makinda, amesema kama kungekuwa na utaratibu wa kubadilishana kifo, basi angetafuta mtu ambaye angebadilishana na Waziri wa Fedha na Uchumi, marehemu William Mgimwa ili amalizie kazi aliyoianza.
Spika alitoa kauli hiyo jana kwenye viwanja vya Karimjeee jijini Dar es Salaam wakati wa kuuaga mwili wa marehemu Mgimwa aliyefariki hivi karibu nchini Afrika Kusini.
Huku akijawa na majonzi, Spika Makinda alisema anatamani kuona Mgimwa yuku hai ili akamilishe kazi aliyokuwa ameianza.
“Kutokana na mchango wake wa kazi, bado tulikuwa tukimhitaji sana katika kukamilisha kazi aliyokuwa ameianza ya kuwa na mfumo mmoja wa bajeti, lakini hata hivyo aliugua ghafla, ingawa ni mtihani kwa Rais Kikwete, naamini atampata waziri mwingine,” alisema Makinda.
Alisema Waziri Mgimwa ataendelea kukumbukwa kutokana na utekelezaji wa majukumu yake ambapo pia ni matunda waliyopewa na Mungu.
Msemaji wa familia, Joachim Mgimwa, aliwashukuru viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali ambao alisema walipiga simu zaidi ya 1,260 za kumjulia hali Waziri Mgimwa wakati akiwa nchini Afrika Kusini kwa matibabu.
Alisema familia ya marehemu Mgimwa, inamshukuru zaidi Rais Jakaya Kikwete kwa upendo wake wa kuwasaidia Watanzania kwani alimtembelea Mgimwa mara mbili Afrika Kusini alikokuwa amelazwa.
“Tunamshukuru Balozi wa Afrika Kusini kwa kufuatilia kwa karibu matibabu ya Mgimwa alipokuwa nchini kwake,” alisema.
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alisema Mgimwa ni miongoni mwa mawaziri wachache waliokuwa wakifanya kazi kwa waledi bila ubaguzi.
“Tunatoa pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete kwa kuondokewa na Waziri Mgimwa, zaidi familia na wananchi wa Jimbo la Kalenga kwa kuondokewa na mtu muhimu,” alisema Mbowe.
Alisema kwa muda mfupi aliofanya kazi, Mgimwa hakuwahi kukwaruzana na wabunge wenzake.
Aliongeza kuwa waziri huyo kwa muda wake huo mfupi hakuweza kukubali kutumika vibaya, hivyo ni vema kwa atakayeshika nafasi hiyo akaiga tabia yake.
Waziri wa Fedha wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mohamed Abood, alisema kifo cha Mgimwa ni pengo kubwa na sio kwa familia yake tu, bali pia kwa Serikali ya Rais Kikwete.
Alisema taifa limeondokewa na kiongozi imara, muadilifu na mpenda maendeleo ya nchi yake kwa ujumla.
Kaimu Waziri wa Fedha na Uchumi, Saada Mkuya, alisema katika miezi 20 aliyoishi na waziri huyo, amejifunza mengi kutoka kwake, hivyo aliahidi kumuezi kwa kutenda aliyowafundisha.
Mwakilishi wa Kamati ya Fedha (CCM), Mwigulu Nchemba, alisema mengi yamekwishasemwa, lakini aliwashangaa wanasiasa pindi wanaposikia serikali idhibitiwe katika matumizi ya fedha, wao wanafikiria kuwa ni CCM na serikali huku wakishindwa kuelewa kuwa na wao ni sehemu ya serikali katika kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za serikali.
Mara baada ya kuagwa mwili huo, ulielekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa safari ya kwenda mkoani Iringa, tayari kwa mazishi yanayotarajiwa kufanyika leo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi, William Lukuvi, alisema baada ya kufika Iringa mwili utapelekwa kwenye ukumbi wa Siasa ni Kilimo kwa ajili ya wakazi wa huko kutoa salamu zao za mwisho na kisha kupelekwa moja kwa moja kijijini kwake Magunga kwa ajili ya maandalizi ya mazishi leo.
Mgimwa alifariki Januari Mosi mwaka huu katika Hospitali ya Kloof Med-Clinic, Pretoria nchini Afrika Kusini ambako alilazwa tangu Novemba mwaka jana kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya figo. TANZANIA DAIMA.
0 comments:
Post a Comment