BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MELI YA KILIMANJARO YAIBUKA MAJONZI UPYA KWA WATUMIAJI WA USAFIRI WA MAJINI DAR ES SALAAM-ZANZIBAR.


ASALAMU Alaykum. Kwa masikitiko makubwa tunapokea taarifa nyengine za maafa ya usafiri baharini hii ni mara ya tatu kutokea maafa kama haya au yanayofanana na haya katika kipindi cha miaka mitano ya mwanzo ya Serikali ya Umoja wa kitaifa inayoongozwa na Dk Ali Mohammed Shein na Makamo wake wawili mmoja akitokea katika Chama Cha (CCM), Balozi Seif Ali Idd na mwengine akitokea Chama Cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad.



Ni hali ya kusikitisha na kutia simanzi sana ikiwa hadi leo bado tunaendelea na utaratibu wa kusahau yaliopita na ikiwa bado misiba ile ya kupoteza roho za watu kadhaa haijatugusa jee tutaguswa na lipi katika suala zima la usafiri baharini? Jee wananchi wote wangonye wasafiri kwa ndege jee wana uwezo huo? Kwa nini serikali haiweki mazingira mazuri ya usafiri wakati inajua kwamba kuna hatari ?.


Kwa nini Mamlaka zinazohusika haziwezi kuchukua hatua za dharura na za haraka inapotokea hatari kama hii jee watendaji na wenye kumiliki usafiri baharini nao wanakaguliwa na kuadhibiwa wanaposababisha maafa na kufanya uzembe kama huu? Jee Mamlaka ya Hali ya Hewa inatoa taarifa na kama inatoa jee wahusika wanapokiuka na wasipozingatia uhai wa wananchi wanyonge waache tu kila siku wakisababisha vifo vya watu kadhaa ?.

Kwa taarifa za leo jioni ni kwamba tayari miili ya watu watano imeshaokotwa ikiwa inaelea baharini kwa maana ya kupoteza maisha tokea asubuhi wakiwa katika chombo cha usafiri kilichokuwa kikitokea Pemba na kuelekea Unguja kilipofika katika mkondo wa Nungwi kikapigwa na dhuruba kali ya upepo na watu waliokuwa mbele ya boti hiyo ya Kilimanjaro 2 wakaingia baharini na kuzama hali ambayo ikaleta mtafaruku mkubwa kwa abiria waliokuwemo ndani ya chombo hicho lakini pia kwa wananchi waliokuwepo majumbani wakipeana taarifa mbali mbali za maafa hayo na vifo huku wengine wakiwa na taharuki kubwa baada ya kujua ndugu na jamaa zao wamo ndani ya chombo hicho.

Naomba kwa heshima na taadhima nisema mambo mawili matatu ambayo muyachukulie kama ni changamoto ambayo ipo mbele yetu na inahitaji kufanyiwa utafiti na kupatikana usumbuzi wa kina ili makosa kama haya yanayoweza kuepukwa ya kuhatarisha maisha ya wenzetu yasitokee tena hapa kwetu.

Kwa uchunguzi mdogo nilioufanya tokea asubuhi ilipotokea khitilafu Boti ya Kilimanjaro 2 ni kuwa nimegundua kuna udhaifu fulani katika mamlaka zinazosimamia usafiri nchini kuanzia serikalini hadi kwa wamiliki wa boti hizo kama ufuatavyo:

Serikali ya Zanzibar kwa maoni yangu imezembea kwa kiasi fulani katika suala zima la uokoaji wa watu ambao walipotea kufuatia upepo mkali uliotokea leo asubuhi katika chombo kinachomilikiwa na Azam Marine boti ya Kilimanjaro 2 iliyokuwa ikitokea Pemba kuja Unguja na kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya uhakika. Uzembe ulitawala katika maeneo yote yanayohusika.

Kwa upande wa serikali nao mamlaka zinazohusika kwanza wizara kupitia Naibu wake Issa Gavu mara kadhaa alipigiwa simu na kutakiwa kutolewa kwa helikopta lakini akasema haina mafuta imekwenda kutiwa mafuta alipopigiwa simu mara ya pili akasema kuwa mafuta bado na kuchukua zaidi ya saa moja na baadae akapigiwa tena akasema kwamba helikopta haiwezi kuruka kwa kuwa kiwanjani kuna ndege nyingi hata pale alipotakiwa kutoa dharura hiyo ya maafa akasema tumo katika utaratibu na akawa kila akihimizwa anasema wapo katika utaratibu hadi nyakati za jioni ndio helikopta imetolewa kwenda kuokoa wakati tayari maiti tatu zimeshaokolewa na wananchi wa kawaida. Kama nasema uongo basi akatae hili nililoandika.

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu kwanza upande wa wamiliki wa boti ya Kilimanjaro ambao ni akina Bakhressa kwanza walikataa kutoa taarifa na walisema awali kwamba watu waliochukuliwa na wimbi wakati boti ilipopigwa na dhuruba ya bahari hawafiki hata 10 kama wanne au watano hivi ndio walivyosema wakati watu zaidi ya hao kumi walipotea mbele walichukuliwa na wimbi na kupotea baharini. lakini walipotakiwa wapewe msaada inasemekana kwamba walikataa na kusema wanashughulikia wenyewe.

Waziri wa Mawasiliano na Miundombinu naye alipotoshwa kwa kupewa taarifa zisizo sahihi naye akawawaambia waandishi wa habari kwa njia ya simu taarifa hizo hizo alizopewa na watendaji wake ambazo sio sahihi hata kidogo aliwaambia waandishi kwamba hakuna mtu aliyepotea wala kufa wote wapo salama jambo ambalo ni upotoshaji wa taarifa unaotolewa na taasisi au mamlaka ya serikali kama hiyo. Kama nasema uongo na akanushe jee hakupotoshwa?

Kwa upande wa waandishi wa habari wa wizara ya mawasiliano na miundombinu nao walipopigiwa simu wakawa wanatoa information zisizofahamika kila mmoja akijibu vyake wengine wakisema hakuna chombo kilichopata khitilafu wengine wakisema ni uzushi wengine wakisema ndio imetokea lakini hakuna tatizo chombo kimo safarini ni wimbi dogo tu.

Kwa upande wa kitengo cha maafa nacho kinapaswa kubeba lawama kwa upande wake kwani hakijaonesha kujifunza chochote kupitia ajali zile mbili zilizouwa mamia ya watu maana hawana utaratibu mzuri wa uokozi na hawana mikakati madhubuti ya kuonesha kuweza kukabiliana na jambo hilo wakisikia jambo wanapata mfadhaiko badala ya kushughulikia haraka. Kuna mengi lakini na hilo wakatae kama hawajafadhaika na watwambie nini wamefanya na tokea kupata hizo taarifa ni muda gani wamejizoa na kushughulikia ?.

Ni miaka 50 ya Mapinduzi maandamano yalikuwa uwanja wa Maisara takriban mawaziri na watendaji wengi wa serikali walikuwa hapo kulikuwa na mkutano ambao umehutubia na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jakaya Kikwete kwa hivyo watendaji walipopata hiyo taarifa hawakujuchukua jitihada za dharura na badala yake walizembea na kuendelea kukaa na huku maafa yanaendelea kutokea.

Amma kwa upande wa haki ya kupata habari na kutulizwa wananachi waliokuwa na khofu kubwa mitaani na majumbani ambao walikuwa na kiu ya kupata habari ili kupunguza khofu yao ambayo walikuwa wakitegemea chombo cha serikali Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) ambacho ndio pekee kilichopo na ambacho serikali ingepaswa kujivunia nacho lakini nacho kilikuwa kikirusha matanganzo ya moja kwa moja ya mkutano wa hadhara wa Jakaya Kikwete. 



ZBC haikuweza kukatisha matangazo yake na kutoa taarifa hizo, sio kwenye taarifa ya habari ya saa 9 mchana wala katika taarifa ya habari ya saa 2.15 usiku. Na ikatubidi sisi wengine tuwatulize watu tukiwaambia hakuna taarifa mbaya hali ya kuwa tunajua taarifa zipo lakini kwa kuwa hazijathibitishwa hatukuweza kutoa taarifa hizo kwa umma hadi pale mamlaka zinazohusika zilipokuwa tayari kutoa taarifa ambapo ni nyakati za jioni tena. Haya wenye kusimamia shirika la habari watwambia taarifa wamewapa umma au wamewakosesha haki ya msingi wananchi?

Baada ya maelezo hayo Serikali inapaswa kujifunza tena na tena kwa maafa yanayotokea na ufike wakati sasa kusafisha kitengo cha maafa na kuwekwa watu ambao wana uwezo wa kushughulikia mambo hayo serikali ikubali kuingiza watu wa sekta binafsi ili watoe msaada kwani tulishuhudia wakati wa maafa ya meli za mwanzo zilizotokea na watu kufariki watu binafsi walisaidia na pamoja na wawekezaji waliowekeza hapa Zanzibar kwa kushirikiana na wananchi wa kawaida hivyo basi serikali ione mchango wao huo na kuweza kuuthamini ili kuokoa maisha na wananchi wake ambao wamekuwa wakifikwa na maafa kama haya ambapo matukio yamekuwa yakijirudia.

La mwisho ushauri wangu kwa serikali ifike pahala iamini kwamba usafiri wa boti haufai tena na sasa ijikite katika kuharakisha meli kubwa na yenye uwezo wa kuhimili mkondo wa bahari ya Nungwi ili kuwashushia pumzi wasafiri wanaokwenda na kurudi Pemba, Unguja na Dar es Salaam.

SALMA SAID.
Shukran
Asalamau Alaykum
Maiti ni wawili wanawake na watatu wanaume kwa mujibu wa taarifa za sasa hivi kutoka kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri Bw. Abdi Omar amesema usiku huu katika taarifa yake na waandishi wa habari huko Bandarini Malindi. Mkurugenzi anasema bado wataendelea kesho asubuhi kuwatafuta watu waliopotea baharini katika maeneo ya Nungwi.

Maiti wote wameletwa mjini kwa ajili ya kutambuliwa wapo katika hospitali ya Mnazi Mmoja baadae serikali itaanda utaratibu wa kawaida kwa maiti hizi kuzikwa kama ni kupewa jamaa zao.

Kempteni Nassor Abubakar Khamis ameshikiliwa na jeshi la polisi kwa mahojiano.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi anasema baada ya kupata hizo taarifa waliwahoji wahusika wa boti lakini Manahodha wa boti hiyo alisema hajaona kama kuna watu wamepotea lakini wao waliona mizigo tu imeanguka.

Mkurugenzi Abdi aliwaambia waandishi wa habari kwamba Manahodha hao walipofika Nungwi kuna watu waliwauliza ikiwa kuna tatizo baada ya kuona boti yao inazunguka zunguka hapo hapo lakini walijibu kwamba hawana tatizo na wanaendelea na safari lakini pia wakaulizwa na KMKM iwapo wanahitaji msaada lakini walikataa na kusema hawana tatizo na wakaendelea na safari.

Mkurugenzi huyo amesema juhudi za serikali zilichukuliwa lakini alikubali kwamba wananchi ndio waliosaidia kwa kushirikiana na vyombo vya usalama kusaidia kuwatafuta waliopotea.

Mkurugenzi Abdi anasema kwa kufichwa taarifa hizi kumesbabisha matatizo na kiukweli wangepewa taarifa mapema na Manahodha basi wangeweza kuchukua juhudi za haraka kufanikisha uokozi huo lakini wamepata taarifa kutoka kwa wananchi na sio kwa wahusika wa boti hiyo.

Anasema jumla ya abiria 396 walisafiri na chombo hicho huku watoto wakiwa ni 60 lakini baada ya kufanya hesabu wakakuta idadi hiyo imepunguwa kuna watu kama 20 wamekosekana ndani ya chombo hicho na ndipo walipolazimika kufanya uchunguzi na kufuatilia huko Nungwi na kweli wamepata miili mitano na waliookolewa wakiwa hai ni watatu.

Naomba kuwasilisha Salma Said. Bandarini Zanzibar
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: