MGOGORO wa uongozi unaoendelea ndani ya Chadema, umemlazimisha
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, kukemea na
kutaka pande zinazopingana kuzuia wafuasi kujihusisha na vurugu na
uvunjifu wa amani.
Jaji Mutungi alitoa kauli hiyo jana katika taarifa yake kwa vyombo
vya habari kuhusu mgogoro huo, ambao uongozi wa Mwenyekiti Freeman
Mbowe, umepiga marufuku viongozi, wanachama na mashabiki wa chama hicho
kumwunga mkono aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe.
“Nachukua fursa hii kukemea vurugu na vitendo vya uvunjifu wa amani
uliofanywa na wafuasi wa pande zote mbili katika maeneo ya Mahakama Kuu
Kanda ya Dar es Salaam. “Pia kila kiongozi, mwanachama au shabiki wa
chama cha siasa aelewe kuwa anawajibika yeye binafsi kwa uvunjifu wowote
wa sheria,” alisema Jaji Mutungi.
Demokrasia Mbali na kuwakemea, pia Jaji Mutungi alitoa kauli ya
kutilia shaka ukomavu wa kisiasa na kidemokrasia ndani ya chama hicho.
“Migogoro ndani ya vyama vya siasa ni mojawapo ya vyanzo vya uvunjifu
wa amani, hivyo nawaasa wadau wote, kwamba migogoro hiyo inapaswa
isivuke mipaka na kuwa uhasama na uadui wa kufanya wafuasi wa pande
mbili kupigana, kwani hiyo si demokrasia.
“Nasisitiza, kwamba ni vema viongozi na wanachama wa vyama vya siasa
waoneshe ukomavu wa kisiasa kwa kushughulikia tofauti zao na migogoro
baina yao kwa ustaarabu, utulivu na amani, huku wakizingatia sheria zote
za nchi... hiyo ndiyo demokrasia ya kweli,” alisema.
Alisema moja ya majukumu ya ofisi yake ni kusimamia utekelezaji wa
Sheria ya Vyama vya Siasa ya Mwaka 1992 na kanuni za Maadili ya Vyama
vya Siasa za Mwaka 2007, zinazokataza vyama kuruhusu wanachama au
mashabiki kujihusisha na vurugu na uvunjifu wa amani.
Wanahabari.
Aidha, Mutungi aliasa waandishi wa habari kujiepusha kushabikia
migogoro ndani ya vyama vya siasa na kutaka watafakari kwa undani athari
za taarifa zao kwa jamii, kabla ya kuzitoa hasa kuhusu mgogoro wa ndani
ya chama chochote cha siasa.
Wakati wa kusubiri hukumu ambayo uongozi wa Chadema ulishindwa, nje
ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kulikuwa na mvutano kati ya wana
Chadema wanaomwunga mkono Zitto na upande wa akina Mbowe.
Wanachama hao walikuwa wakifurika mahakamani hapo na kujigawa katika makundi mawili na mara kadhaa walipigana na kutoana damu.
Aliyeshambuliwa
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Chadema wa Wilaya ya Temeke, Josephat
Yona, amehama nyumbani alikokuwa akiishi kwa sababu za kiusalama.
Akizungumza jana na mtandao wa millardayo.com, Yona ambaye
alishambuliwa Jumatatu na watu wasiojulikana baada ya kutekwa na kupigwa
na kutelekezwa, hivi sasa baada ya kutoka hospitalini alikokuwa
amelazwa kwa matibabu anaishi kusikojulikana.
“Ni kweli nimehama kwa sababu za kiusalama … wale watu
walivyonichukua walinipiga nikawa sijisikii vizuri nilipokuwa naongea na
waandishi, lakini leo (jana) niko vizuri, mtu kama (anamtaja jina)
alikuwa akiwapigia simu nawasikia kabisa, walikuwa wanawasiliana naye …
kuna mtu kama k-two,” alisema Yona.
Aliendelea kulalamika, kwamba kama ameumizwa yeye kiongozi wa chama
itakuwaje kwa watu wa chini … “vyombo vya usalama inabidi viangalie hata
walionifungia ofisi yangu saa 10 kabla ya mimi kutekwa, kwa sababu ni
saa chache tu kabla ya kutekwa”.
Alisema maendeleo yake sasa ni mazuri zaidi ila kichwa na mgongo bado
vinamuuma na walikubaliana aondoke hospitali saa 12 jioni siku ya tukio
kwa sababu ya mambo ya kiusalama.
Kuhusu madaktari alisema kulingana na vipimo vyao anaendelea vizuri
na yamebaki maumivu kwa sababu ya vidonda na walimpa dawa za kumeza
zingine akanunue mtaani.
Umeme
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chama
hicho, John Mnyika ametoa taarifa ya kutafuta maoni kuhusu bei mpya ya
umeme.
Mnyika ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, alitoa mwito
kwa wenye kuathirika na uamuzi huo ndani ya wiki moja kuanzia sasa
watume maoni na mapendekezo yao kwa barua pepe kupitia anuani
mbungeubungo@ gmail.com.
Pia alipendekeza maoni hayo yatumwe kwa njia nyingine za kuwasiliana
na Ofisi ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na Chadema.HABARILEO.
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment