NIMEVUTIWA na utaratibu anaoutumia Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi wa kutoa taarifa ya matukio mbalimbali ya uhalifu mkoani mwake. Tangu ahamishiwe hapo, ameanzisha utaratibu wa kutoa taarifa ya hali ya usalama kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano ya mitandao ya kompyuta.
Anachokifanya kwa hakika kinasawiri harakati na mipango ya kulifanya Jeshi la Polisi kuwa la kisasa. Nakumbuka kuwahi kuandika makala siku za nyuma kuhusu mabadiliko na uboreshaji wa utendaji wa jeshi hilo.
Mojawapo ya maeneo makuu ya kulipa jeshi sura mpya kiutendaji yaliyoainishwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi Mstaafu, Saidi Mwema, ilikuwa ni pamoja na kutumia teknolojia za kisasa, ikiwamo Tehama.
Wakati baadhi ya makamanda wa mikoa wakiendelea na utaratibu wa kuwaita wanahabari na kuzungumza nao kuhusu matukio ya uhalifu na masuala mengine ya usalama, Kamanda Msangi kaamua kutoka ‘kidigitali’ zaidi.
Amekuwa mara kwa mara kama siyo kila siku akitoa matukio ya uhalifu kupitia mitandao ya kijamii. Kinachovutia zaidi ni kuwa taarifa zake pia hujumuisha utoaji mafunzo na onyo dhidi ya vitendo vya uhalifu.
Tofauti na kuita wanahabari, ambao baadaye huripoti taarifa hizo kwa kuzingatia taaluma yao, utumaji wa taarifa kwenye mitandao unampa msomaji nafasi ya kupata picha halisi ya matukio yote, badala ya kujua moja au mawili tu kupitia vyombo vya habari vya kawaida.
Faida nyingine ya kutumia teknolojia hii ni kuwa inarahisisha uhifadhi wa kumbukumbu, utafutaji wake na hata kuzitumia. Kwa watafiti na wengineo wanaotafuta takwimu za uhalifu na hali ya usalama mkoani humo, njia hii inawawezesha kupata matukio yote hata yale madogo ambayo kwa kawaida yanapewa kisogo na vyombo vikubwa vya habari.
Sisemi kwamba jeshi halina utaratibu mwingine mzuri wa kuhifadhi taarifa zake, la hasha. Uwekaji wa taarifa hizi mitandaoni unarahisisha mambo mengi, ikiwamo kutafuta taarifa kwa haraka.
Kwa mfano, mtu anayehitaji taarifa za hali ya usalama Mbeya akiwa jijini Dar es Salaam, hana haja ya kwenda Mbeya au hata makao makuu ya jeshi hilo Dar es Salaam. Mtandao unatosheleza kukidhi haja zake.
Bila shaka huu ni ubunifu unaopaswa kuigwa na watendaji wengine wa jeshi hasa wakuu wa polisi wa mikoa. Uzuri ni kuwa jeshi hilo sasa linaelezwa kufanya mambo yake kisasa.
Usasa huo ujionyeshe pia katika mifumo ya utoaji taarifa kama za uhalifu na nyinginezo muhimu kwa wananchi na hata wadau wengine wa masuala ya usalama.MWANANCHI
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment