BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KURA THELUTHI MBILI ZAKWIMISHA KUPITISHA MAAMUZI KATIKA VIFUNGU VYA RASIMU YA KATIBA MPYA NGAZI YA KAMATI ZA BUNGE MAALUM LA KATIBA DODOMA.

HATUA ya kufanya uamuzi wa kupitisha vifungu vya rasimu ya Katiba mpya katika ngazi ya kamati za Bunge, ilifikiwa jana huku changamoto ya kutopatikana kwa theluthi mbili ya kura kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, ikijitokeza katika kamati nyingi. Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Kamati Namba Kumi, Anna Abdallah, alisema katika baadhi ya ibara za Sura ya Kwanza na Sura ya Sita, walishindwa kupata kura, zinazokidhi masharti ya Kanuni za Bunge Maalumu na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Masharti hayo ni yanayotaka kila ibara na sura, zipitishwe kwa kupata theluthi mbili ya kura kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

“Kwa bahati mbaya wajumbe wa Zanzibar wako 15, sasa ili kupata theluthi mbili, tunapaswa kupata kura kumi na Tanzania Bara tupo 35, ili kupata theluthi mbili tunapaswa kupata kura 23. “Sasa ibara nyingi tulizopiga kura, hatupati theluthi mbili, tulipofikia katika masuala ya serikali tatu au mbili, wengi walisema serikali mbili na kila mtu alitoa sababu zake na wachache walisema shirikisho,” alisema.

Alisema kwa upande wa Tanzania Bara katika suala la muundo wa Muungano, theluthi mbili ilipatikana, lakini kwa Zanzibar haikupatikana.

Kutokana na utata wa Ibara ya Kwanza ya Sura ya Kwanza, kuwa na neno shirikisho na nchi, Anna alisema walipiga kura kuwa anayetaka neno shirikisho hilo libaki, ieleweke wazi kuwa anataka serikali tatu na anayetaka liondoke, anataka serikali mbili.

Sehemu ya Ibara hiyo inayobishaniwa katika rasimu ya Katiba inasema; “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi na Shirikisho lenye mamlaka kamili…”.

Mwenyekiti wa Kamati Namba Moja, Ummy Mwalimu, alisema pia katika kamati anayoiongoza, walipata changamoto hiyo ya kukosa theluthi mbili ya kura.

“Katika Ibara ya kwanza tu, tulipopiga kura matokeo yalipotoka, hatukupata theluthi mbili kutoka Zanzibar wala Tanzania Bara,” alisema Ummy.

Katika mjadala huo, pia waliotaka neno Shirikisho liondolewe walikuwa na hoja ya serikali mbili na waliotaka lisiondolewe ni wajumbe waliokuwa na hoja ya serikali tatu.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati Namba Moja, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, alisema katika kamati hiyo kuna idadi ndogo ya wajumbe ambayo inasababisha upatikanaji wa theluthi mbili ya kura kuwa mgumu.

“Theluthi mbili ina ugumu, kwa mfano hapa kwetu wajumbe kutoka Zanzibar wapo 19, ili upate theluthi mbili unapaswa kupata kura 13, sasa unaweza kupata 12 na saba zikakataa, hapo umekosa mjumbe mmoja tu kupata theluthi mbili. “Nadhani hili la theluthi mbili, tuliangalie kwa watu wengi kule kwenye ukumbi mkubwa (bungeni),” alisema Profea Mbarawa.

Mwenyekiti wa Kamati Namba Tano, Hamad Rashid Mohamed, alisema hata katika Kamati hiyo, hawakupata theluthi mbili ya kura kutoka kila upande wa Muungano katika baadhi ya ibara.

Alitoa mfano wa Ibara ya Kwanza ya Sura ya Kwanza kuhusu Tanzania ni Shirikisho, ambapo wengi walitetea ibaki kama ilivyo, lakini Zanzibar hawakupata theluthi mbili kwa kura.

Bungeni, Muda
Kutokana na hali hiyo, Ummy alisema uamuzi wa Kamati si wa mwisho, uamuzi wa mwisho utapatikana Bungeni baada ya yeye kutoa taarifa ya Kamati.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta jana aliongeza muda kwa kuruhusu Kamati kuendelea kujadili, badala ya Kamati ya Uandishi kufanya kazi yake.

Katika maelekezo yake ya awali, Sitta alizitaka Kamati hizo kujadili na kuamua ibara za Sura ya Kwanza na Sura ya Sita kwa siku mbili, yaani Jumanne na Jumatano wiki hii na jana ilikuwa siku ya Kamati ya Uandishi kuandika yaliyokubaliwa katika kamati husika.

Leo Bunge lilitarajiwa kupokea taarifa za wenyeviti wa kamati zote 12 na baada ya hapo kuanza mjadala wa pamoja ndani ya Bunge, ambapo sura hizo mbili zingepitishwa kwa kura ya theluthi mbili ya wajumbe wote wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Hata hivyo, kutokana na Kamati nyingi kushindwa kumaliza kazi katika siku mbili, na kujikuta zikipeleka taarifa kwa Sitta ya kuomba kuongezewa muda, Sitta alitoa nafasi ya kuendelea kujadili mpaka jana.

Mwenyekiti wa Kamati Namba Kumi, Anna alisema Mwenyekiti aliwaruhusu kuendelea kujadili mpaka jana, wakati awali walipaswa kuwa wamemaliza na kuruhusu Kamati ya Uandishi kufanya kazi yake.

“Nimemwandikia Mwenyekiti atuongezee siku mbili, Sura ya Sita tumeanza kuijadili leo (jana) na tunatarajia kufunga mjadala saa mbili na kesho (leo) tutapiga kura…sasa kesho asubuhi Bunge litaitishwa lakini mimi sitakuwa na taarifa ya kuwasilisha,” alisema Ummy.

Alikumbusha kuwa kabla ya kuanza kujadili rasimu ya Katiba, Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalumu, iliagiza Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge kubadili baadhi ya kanuni, lakini baadhi ya wajumbe kutoka vyama vyaa upinzani, walikataa.

“Mtakumbuka hapa, mabadiliko ya kanuni yaliyotarajiwa kuletwa yaliitwa takataka na vyama vya upinzani, mabadiliko yale yalikuwa na hili suala la muda, lakini wapinzani wakakataa, haya sasa tunasubiri busara za Mwenyekiti (Sitta),” alisema Ummy akifafanua kuhusu suala la muda.

Muungano
Mwenyekiti wa Kamati namba nane ya Bunge Maalum la Katiba, Job Ndugai alisema kamati yake haikuchukua muda mwingi katika kujadili uhalisi wa hati ya Muungano, iliyosainiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amaan Karume kwa vile suala hilo si muhimu.

Alisema badala yake Kamati yake ilijikita katika kujadili ili kuona kama vyombo muhimu, likiwemo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania viliridhia kuundwa kwa Muungano huo kuona kama kulikuwa na ushirikishwaji mpana wa wananchi baada ya Nyerere na Karume jambo ambalo wameridhika nalo.

Ndugai aliyasema hayo jana, wakati akitoa taarifa ya kilichofikiwa na Kamati yake katika kujadili sura hizo mbili za rasimu, ambapo pia alieleza majadiliano hayo kuwa makali na yenye mvutano ingawa hakukuwa na vurugu kama zinazotokea bungeni.

Akizungumzia mwenendo wa majadiliano, alisema katika baadhi ya vipengele kuliibuka mjadala mkali na kwamba wajumbe waligawanyika katika mitazamo na yeye kama Mwenyekiti atawasilisha kwenye Bunge maoni ya wajumbe walio wengi na yale ya wajumbe wachache, ambao hawakukubaliana na kila Ibara.

Hata hivyo alisema hadi jana mchana, Kamati yake ilikuwa haijapiga kura ili kupitisha vifungu vya Ibara za Sura ya Kwanza na ya Sita, kutokana na muda kuwa mfupi na kutawaliwa na mjadala mpana na mkali, hatua ambayo alisema itamlazimisha kuomba muda zaidi kutoka kwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta leo.

Hata hivyo alisema kulingana na mwenendo wa mjadala huo, ni vigumu kwa theluthi mbili za kura kupatikana na hasa kwa upande wa Zanzibar na hivyo njia pekee watakayoifanya ni kuwasilisha maoni ya wajumbe walio wengi na walio wachache kama yalivyo ili Bunge zima liweze kutolea uamuzi.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: