Na Mtanda Blog, Morogoro.
Zaidi ya miche 325,678 ya miti ya aina mbalimbali imepandwa katika eneo la Mbete,Morogoro, baada ya Kituo cha Elimu ya Uhifadhi wa Mazingira na Roots & Shoots kugawa miche hiyo kwa wananchi na taasisi, ili kurejesha hali ya uoto wa asili katika safu ya Milima ya Uluguru.
Miti hiyo ilianza kupandwa mwaka 2009.
Akizungumza na gazeti hili wakati wa tukio la upandaji miche hiyo, Mratibu wa kituo hicho, Erasto Njavike, alisema uamuzi wa kutoa miche hiyo umekuja baada ya eneo hilo kupoteza uoto wake wa asili kutokana na shughuli za kibinadamu zikiwemo za kilimo na uchomaji moto misitu ili kurahisisha uwindaji wa wanyama aina ya ndezi hasa nyakati za kiangazi.
Njavike alisema mwaka 2008 eneo hilo lilikumbwa na uharibifu mkubwa wa mazingira na kulifanya kuwa katika hali mbaya iliyosababisha mito na chemchem kukauka.
Kwa mujibu wa mratibu huyo, kitendo hicho kilikifanya kituo kugawa miche kwa shule za msingi, sekondari, vyuo vikuu, mashirika ya kiserikali na yasiyokuwa ya kiserikali pamoja na watu binafsi.
“Miaka ya 1980 kurudi nyuma hali ilikuwa nzuri na ya kuvutia lakini katika miaka ya 2000 iligeuka baada wananchi kuanza kuchoma misitu ovyo ili kutafuta wanyama aina ya ndezi kwa ajili ya kitoweo na mkaa na hivyo na kufanya Safu ya Milima ya Uluguru, kupoteza uoto wa asili,”alisema Njavike.
Njavike alisema tangu mwaka 2009 hadi sasa kituo kimeotesha zaidi ya miche 325,678 na kuigawa kwa wananchi miche 298,106 huku kitalu ikiwa na akiba ya miche 27,572.
Akizungumza katika tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Said Amanzi, ambaye alikuwa mgeni rasmi, aliwataka wakazi wa maeneo ya vijijini kuiga mfano wa wananchi wa Wilaya ya Lushoto, mkoani Tanga, ambao wana utaratibu unaomtaka kila mmoja kupanda miti sita kuzunguka nyumba yake.
0 comments:
Post a Comment