Mwendesha pikipiki katika Manispaa ya Morogoro akiwa amebeba abiria wake zaidi ya mmoja kinyume na sheria za usalama barabarani wakati akiwasafirisha kutoka sehemu moja kwenda nyingine katika eneo la njiapanda ya Veta Kihonda mjini Morogoro.
KANUNI mpya za uendeshaji usafiri wa pikipiki na bajaj maarufu bodaboda, zimeainishwa zikisisitiza waendeshaji wa vyombo hivyo, kutekeleza masharti, ikiwemo linalokataza kupakia mtoto mwenye umri wa miaka tisa na chini yake.
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), imesisitiza kutumiwa kwa kanuni hizo na kusema mtoto wa umri huo, anapaswa awe na mtu mzima aliyeongozana naye, ndipo apakiwe kwenye vyombo hivyo.
Meneja Mawasiliano wa Sumatra, David Mziray alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi juu ya kanuni hizo za usafirishaji wa bajaj na pikipiki za mwaka 2010, zilizoanza kutumika Julai mosi, 2011. Sumatra imesema imebaini madereva wengi hawajui na hawatekelezi kanuni hizo zilizo chini yake.
Katika kutekeleza, Sumatra imekasimu madaraka ya kutoa leseni ya waendesha vyombo hivyo vya usafiri kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo ni pamoja na Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya.
Mamlaka hizo zina majukumu ya kubaini maeneo yatakayokuwa vituo vya watoa huduma za usafiri wa vyombo hivyo.
Katazo hilo la kupakia mtoto mwenye umri wa miaka tisa na chini yake, ambalo Sumatra imehimiza lizingatiwe, pamoja na kuwepo limekuwa likikiukwa kutokana na wimbi la wazazi na walezi kutumia vyombo hivyo kusafirisha watoto hususani kwenda shule.
Gazeti hili limebaini katika jiji la Dar es Salaam, ikiachwa wanafunzi wenye usafiri wa shule wa magari, baadhi ya wazazi huingia makubaliano na waendesha pikipiki au bajaj ya kupeleka watoto wao wakiwemo wenye umri unaokatazwa na Sumatra.
Sare kwa bodaboda Masharti mengine yaliyo kwenye kanuni ni pamoja na dereva wa pikipiki na bajaj, kutakiwa kuvaa sare zinazotumika katika eneo lake la kazi.
Hata hivyo, hilo pia utekelezaji wake haujafanyika katika eneo lolote nchini. Wameaswa kufuata sheria zote za usalama barabarani na hawaruhusiwi kutumia simu au kifaa chochote cha mawasiliano wakati wa kuendesha chombo husika.
Kanuni hizo pia zinakataza dereva wa bodaboda kutumia lugha chafu na matusi. Zinazuia pia dereva kusababisha usumbufu kwa mtoa huduma mwingine, kuendesha kwa kasi kuzidi mwendo ulioruhusiwa, kukatisha safari, kuendesha wakati akiwa amelewa pombe na kutomsumbua abiria.
Dereva wa pikipiki atakayekiuka masharti hayo, anapaswa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Akibainika kukiuka, atatozwa faini kati ya Sh 50,000 na 100,000 au kwenda jela kati ya mwaka na miaka miwili.
Mziray alifafanua zaidi mambo muhimu yaliyojitokeza katika kanuni hizo kuwa ni maombi ya leseni ambapo hakuna mtu atakayeruhusiwa kuendesha biashara ya kubeba abiria kwa pikipiki za magurudumu mawili na matatu bila ya kuwa na leseni ya usafirishaji.
Alisema anayetaka kufanya biashara ya kubeba abiria kwa pikipiki za magurudumu mawili na matatu, atatakiwa kupeleka maombi ya leseni kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo zinajumuisha Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya.
Kadhalika alisema pikipiki na bajaj zinazotoa huduma za usafiri wa abiria zitakuwa na vibao vyenye namba ya usajili vilivyoandikwa kwa maandishi meusi na vibao vyeupe. Vile vile leseni zitatolewa tu kwa muombaji ambaye ni mwanachama wa umoja uliosajiliwa.
Atakayefanya biashara ya kubeba abiria kwa pikipiki au bajaj bila kuwa na leseni ya usafirishaji atakuwa amevunja Sheria na atashitakiwa na kutozwa faini kati ya Sh 50,000 hadi 100,000 au kufungwa jela kati ya miezi sita na mwaka mmoja.
Kuhusu masharti ya leseni, alisema pikipiki husika lazima ikidhi viwango vya TBS, itatakiwa kutoa huduma katika eneo lililoruhusiwa kwa mujibu wa sheria, dereva kutoruhusiwa kubeba abiria zaidi ya mmoja na dereva wa bajaj haruhusiwi kubeba idadi ya abiria inayozidi idadi iliyoidhinishwa katika leseni.
Alisema masharti mengine ya leseni ni dereva wa pikipiki kutakiwa kuvaa kofia ya kujikinga na kuwa na alama ya eneo analofanyia biashara ya kubeba abiria, abiria wa pikipiki kutakiwa kuvaa kofia ngumu ya kujikinga wakati wote, na kofia ya kujikinga inatakiwa kuwa na alama ya eneo la utoaji huduma ya usafiri.
Mziray alisema dereva wa vyombo husika wanatakiwa kusoma na kuzielewa Kanuni hizo zinazopatikana katika ofisi ya Sumatra na kutakiwa kuanzisha vyama au ushirika katika maeneo wanayofanyia biashara ya kusafirisha abiria ili kuweza kuomba leseni kama ilivyoainishwa katika kanuni.
Mnyika na bodaboda Katika hatua nyingine, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika amelia na agizo agizo la kupiga marufuku pikipiki na bajaj kuingia katikati ya Jiji la Dar es Salaam akisema limesababisha mgogoro baina ya madereva na vyombo vya ulinzi na usalama.
Machi 3 mwaka huu, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik alipiga marufuku uingizaji wa vyombo hivyo katikati ya jiji; amri ambayo Mnyika anasema limeathiri pia abiria ambao wanategemea usafiri huo wakati huu ambao ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo kwa haraka (BRT) unafanyika.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Mnyika alisema pia upo utata kuhusu mipaka ya eneo la katikati ya mji linaloguswa na amri hiyo.
Alisema amemwandikia ujumbe Mkuu wa Mkuu wa Mkoa kuomba kusitishwa muda utekelezaji wa agizo hilo kupisha mazungumzo baina ya Serikali, wahusika wa bodaboda na wadau wengine muhimu kupata ufumbuzi.
Kadhalika alisema anahitaji kupata nakala ya kanuni na maagizo kutafakari iwapo misingi ya ushirikishwaji, haki na uhuru wa kisheria na kikatiba imezingatiwa katika mchakato mzima.
Awali, Meneja Mawasiliano wa Sumatra, David Mziray aliainisha mipaka ya eneo la katikati ya jiji kwa upande wa Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, ni Mwenge.
Kwa Barabara ya Morogoro, mpaka ni Ubungo, Barabara ya Uhuru ni Buguruni, Barabara ya Nyerere ni Tazara na Barabara ya Kilwa ni eneo la chuo cha Uhasibu. Zaidi ya maeneo hayo, hakuna bodaboda inayoruhusiwa kuvuka.
0 comments:
Post a Comment